A

Ndoto ya Mordekai
1 Katika mwaka wa pili wa utawala wa Ahasuero, mfalme mkuu wa Persia, katika siku ya kwanza ya mwezi wa Nisani, Mordekai mwana wa Yairi, mwana wa Shemi, mwana wa Kishi kutoka katika kabila la Benyamini, aliota ndoto.
2 Mordekai alikuwa Myahudi na aliishi katika mji mkuu wa Susa. Yeye alikuwa mtu maarufu na mtumishi katika ikulu ya mfalme Ahasuero.
3 Mordekai alikuwa mmoja wa mateka ambao mfalme Nebukadneza wa Babuloni aliwahamisha kutoka Yerusalemu akawapeleka hadi Babuloni pamoja na mfalme Yekonia wa Yudea. Ndoto aliyoota Mordekai ilikuwa hivi:
4 Mordekai aliota kuna kelele, ghasia, ngurumo na mtetemeko wa ardhi, pamoja na machafuko duniani. 1e Kisha kukatokea majoka mawili makubwa yaliyokuwa tayari kupigana, nayo yalitoa mlio wa kutisha.
5 Kwa mlio wao huo mataifa yote yakajiandaa kupigana vita na watu wa Mungu, taifa adilifu.
6 Siku hiyo ilikuwa ya giza na huzuni, majonzi na udhia, msiba na fujo duniani kote.
7 Taifa lile lote adilifu lilisumbuliwa, likihofia maovu yatakayolikumba. Watu wakajiandaa kufa.
8 Basi, wakamlilia Mungu, na kwa kilio chao, mto mkubwa uliotiririka maji mengi ukatokea kutoka kitu kilichoonekana kama kijito tu.
9 Kulipopambazuka, jua lilichomoza, na wale wanyonge wakapata nguvu, wakawaangamiza adui zao waheshimiwa.
10 Kwa ndoto hiyo, Mordekai aliona yale aliyodhamiria Mungu kuyafanya. Baada ya kuamka, alikuwa nayo akilini mwake na akatamani kujua kinaganaga maana ya ndoto hiyo siku nzima.

Mordekai ayaokoa maisha ya mfalme
11 Mordekai alipokuwa akipumzika kwenye ua wa ikulu pamoja na Gabatha na Thara, matowashi wawili wa mfalme, walinzi wa uani,
12 aliwasikia hao matowashi wakizungumza. Akasikiliza kwa makini kile walichokuwa wakizungumzia, kumbe, walikuwa wanakula njama kumuua mfalme. Basi, Mordekai akamwendea mfalme Ahasuero na kumweleza njama za matowashi hao wawili.
13 Mfalme akaagiza wahojiwe, na walipokiri njama yao, wakatolewa nje na kunyongwa.
14 Mfalme aliamuru kumbukumbu juu ya tukio hilo iandikwe katika kitabu cha kumbukumbu za kifalme, naye Mordekai ndiye aliyeliandika.
15 Kisha, mfalme akamweka Mordekai kuwa mhudumu kwenye ua na akampa zawadi kutokana na kuzifichua njama hizo.
16 Lakini Hamani mwana wa Hamedatha, wa ukoo wa Bouga, mtu aliyeheshimiwa sana na mfalme, akaanza kutafuta njia ya kumdhuru Mordekai na Wayahudi wengine kwa sababu ndiye aliyehusika na vifo vya wale matowashi wawili wa mfalme.

Generic placeholder image