D

Esta anamwendea mfalme
1 Malkia Esta alimwomba Mungu kwa siku tatu. Kisha akavua mavazi aliyokuwa amevaa wakati huo, akavalia mavazi yake ya kifahari.
2 Akajiremba kimalkia. Baada ya kumwomba Mungu Mwokozi, aonaye yote, akawachukua vijakazi wake wawili, akaondoka chumbani mwake,
3 amejiegemeza na mmoja wao amtegemeze,
4 hali mjakazi mwingine aliwafuata nyuma akiwa ameshika mwisho wa shela la malkia Esta.
5 Malkia alionekana mwenye uso unaong'aa kwa uzuri. Alionekana mwenye furaha kama mwanamke anayependwa, lakini moyoni alijaa hofu kubwa.
6 Alipokwisha kupita milango yote, alisimama mbele ya mfalme. Mfalme alikuwa ameketi kwenye kiti chake cha enzi, akiwa amevaa mavazi yake rasmi ya kifalme ambayo yalikuwa yametariziwa kwa dhahabu na vito vya thamani. Alionekana wa kutisha sana.
7 Basi, mfalme aliinua macho yake yaliyojaa fahari, akamwangalia malkia Esta kwa hasira kali. Esta akanyong'onyea na rangi yake ikageuka; na karibu azimie, hivyo akalazimika kuinamisha kichwa chake kwenye bega la mtumishi mwanamke.
8 Hapo, Mungu akaibadili roho ya mfalme yenye hasira kuwa yenye huruma kwa Esta. Haraka, mfalme akanyanyuka kutoka kwenye kiti chake cha enzi, akamshika Esta mkono mpaka Esta alipoweza kusimama wima mwenyewe. Mfalme akamtuliza Esta kwa maneno matamu na laini,
9 akamwuliza, “Una nini Esta? Mimi ni mumeo, usiniogope.
10 Sheria zetu zinawahusu raia wa kawaida tu; wewe hutauawa. Njoo karibu.”
11 Kisha mfalme akainua fimbo yake ya dhahabu ya kifalme na kumgusa nayo malkia shingoni.
12 Akamkumbatia na kumwambia, “Niambie unachotaka.”
13 Malkia akasema, “Nilipokutazama ee bwana wangu, nilijiona kama natazama malaika wa Mungu, na moyo wangu ukanidunda kwa hofu kwa sababu ya utukufu wako.
14 Kweli unastaajabisha sana na uso wako umejaa neema.”
15 Lakini malkia alipokuwa anaongea akazimia tena.
16 Mfalme akafadhaika sana kwa hali hiyo ya Esta, na matowashi wote wa mfalme wakajaribu kumfariji Esta.

Generic placeholder image