2

1 “Kwa hiyo, Bwana ametekeleza sasa jambo lile alilotamka dhidi yetu, na dhidi ya mahakimu wetu wanaoongoza Israeli, dhidi ya wafalme wetu, wakuu wetu na watu wa Israeli na Yuda.
2 Hapana mahali popote pengine duniani palipopata kutukia mambo yaliyotukia huko Yerusalemu, Bwana alipotekeleza yale yaliyoandikwa katika sheria ya Mose.
3 Mambo yalikuwa mabaya kiasi cha mtu kumla mwanawe na mwingine kumla bintiye!
4 Bwana alitutia mikononi mwa tawala zote zilizotuzunguka tukadharauliwa na kuaibishwa kati ya mataifa yote ambako alitutawanya.
5 Kwa vile tulitenda dhambi dhidi ya Bwana Mungu wetu kwa kutokutii sauti yake, basi, taifa letu likashindwa badala ya kuwa mshindi.
6 “Bwana Mungu wetu ni mwadilifu lakini sisi kama tulivyo leo tumejaa aibu kama vile wazee wetu!
7 Maafa yote aliyotutishia nayo Bwana wetu yametupata.
8 Hata hivyo hatukumgeukia na kuomba ili kila mmoja wetu aachane na mawazo ya moyo wake mwovu.
9 Basi, Bwana ameona ni lazima ayalete yale maafa aliyosema, nayo yametupata; maana Bwana ni mwadilifu kuhusu yote yale aliyotuagiza tuyafanye.
10 Lakini sisi hatukutii sauti yake aliposema tuishi kufuatana na amri zake alizotupa.

Maombi
11 “Sasa, ee Bwana, Mungu wa Israeli, wewe ndiwe uliyewatoa watu wako nchini Misri kwa mkono wako wenye nguvu, kwa miujiza, kwa nguvu kuu na kwa mkono wako ulionyoshwa, ukalipatia sifa jina lako hadi leo.
12 Tumetenda dhambi; tumekuwa waovu, tumekosa, ee Bwana Mungu wetu, tukazivunja amri zako zote.
13 Lakini tunakuomba usiendelee kutukasirikia maana humu ulimotutawanya kati ya mataifa mengine tumeachwa na wachache.
14 Usikilize ee Bwana, sala yetu na ombi letu; utuokoe, kwa hisani yako, utujalie tupendeke mbele ya hao waliotupeleka uhamishoni.
15 Hapo dunia yote itatambua kwamba wewe ndiwe Bwana Mungu wetu na kwamba wewe umelichagua taifa la Israeli kuwa watu wako mwenyewe.
16 Ee Bwana, utuangalie hapa chini kwa wema, kutoka makao yako matakatifu. Utege sikio lako ee Bwana, utusikilize.
17 Ufumbue macho yako, ututazame. Wafu walio kuzimu ambao hawana pumzi tena mwilini mwao hawawezi kukutukuza na kutangaza ulivyo mwadilifu wewe Bwana.
18 Lakini watu walio hai, wamelegea, wanyonge, vipofu na wenye njaa ndio hao wanaoweza kukutukuza ee Bwana na kutangaza uadilifu wako.
19 “Ee Bwana, Mungu wetu, maombi yetu hatuyaleti mbele yako tukitegemea matendo yoyote mema ya wazee wetu au ya wafalme wetu.
20 Wewe umeielekeza ghadhabu na hasira yako dhidi yetu kama ulivyoonya hapo awali kwa njia ya watumishi wako manabii waliposema:
21 ‘Bwana asema hivi: Inamisheni mabega yenu mkamtumikie mfalme wa Babuloni nanyi mtaweza kukaa katika nchi niliyowapa wazee wenu.
22 Lakini msipotii sauti ya Bwana, mkakataa kumtumikia mfalme wa Babuloni,
23 basi, nitakomesha ishara yoyote ya furaha na sherehe katika miji ya Yuda na Yerusalemu. Hapatakuwa na sauti za sherehe za harusi. Nchi yote itaachwa ukiwa na mahame!’
24 “Lakini sisi hatukutii sauti yako juu ya kumtumikia mfalme wa Babuloni, nawe umetekeleza yale uliyosema kwa njia ya watumishi wako manabii, uliposema kwamba mifupa ya wafalme wetu na ya wazee wetu itafukuliwa makaburini.
25 Na, kwa kweli imetupwa kwenye joto la mchana na baridi kali usiku. Wao walikufa katika mateso ya njaa, vita na maradhi mabaya.
26 Tena umeifanya nyumba ile ambamo sisi tulikuabudu kuwa uharibifu mtupu kama ilivyo leo hii, kwa sababu ya maovu ya watu wa Israeli na watu wa Yuda.
27 “Hata hivyo, ee Bwana, wewe umetuvumilia kwa wema na huruma yako kuu,
28 sawa kabisa na yale uliyotangaza kwa njia ya Mose mtumishi wako, siku ile ulipomwamuru aiandike sheria yako mbele ya Waisraeli, ukisema,
29 ‘Kama hamtatii sauti yangu, basi, nyinyi mlio jumuiya kubwa mtabaki wachache tu kati ya mataifa ambamo mimi nitawatawanyeni.
30 Najua kwamba hamtanitii maana nyinyi ni watu wenye vichwa vigumu. Lakini mtakapokuwa uhamishoni ndipo mtapata akili,
31 na kutambua kuwa mimi ndimi Bwana Mungu wenu. Mimi nitawapeni moyo wa utii na masikio masikivu.
32 Mtanitukuza na kunikumbuka katika nchi hiyo mtakayohamishiwa.
33 Mtaachana na ukaidi wenu na matendo yenu maovu, maana mtakumbuka yaliyowapata wazee wenu wakati walipotenda dhambi mbele ya Bwana.
34 Kisha nitawarudisheni katika nchi ile niliyoapa kuwapa wazee wenu, ahadi niliyompa Abrahamu, Isaka na Yakobo, nanyi mtaimiliki. Nami nitawafanyeni muwe wengi wala hamtapungua tena.
35 Nitafanya nanyi agano la milele niwe Mungu wenu, nanyi muwe watu wangu. Nami sitawaondoeni tena, nyinyi watu wangu wa Israeli kutoka katika nchi hiyo niliyowapeni.’

Generic placeholder image