1

Shabaha ya kitabu hiki
1 Haya ni maneno yaliyoandikwa na Baruku mwana wa Neria, mjukuu wa Maaseya, wa ukoo wa Sedekia, Hasadia na Hilkia. Baruku aliandika haya huko Babuloni
2 mnamo siku ya saba ya mwezi katika mwaka wa tano baada ya Wakaldayo kuuteka mji wa Yerusalemu na kuuteketeza.
3 Baruku aliyasoma maneno haya aliyoandika mbele ya mfalme Yekonia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, na mbele ya watu wote waliokuja kusikiliza,
4 na mbele ya wakuu na wana wa wafalme, na wazee; aliyasoma mbele ya watu wote, wakubwa kwa wadogo, ambao waliishi huko Babuloni pande za mto Sudi.
5 Baada ya kuyasikia, waliomboleza, wakafunga chakula na kuomba dua kwa Bwana.
6 Kisha wakachanga fedha, kila mtu akatoa kadiri ya uwezo wake,
7 wakizipeleka Yerusalemu kwa kuhani Yoakimu mwanawe Hilkia, na mjukuu wa Shalumu, na kwa makuhani wengine pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye huko Yerusalemu.
8 Siku ya kumi ya mwezi wa Siwani, Baruku alitwaa vyombo vitakatifu vilivyokuwa vimetolewa katika nyumba ya Mungu, akavirudisha nchini Yuda. Vyombo hivyo vya fedha vilikuwa vimetengenezwa na mfalme Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda,
9 baada ya Nebukadneza mfalme wa Babuloni kumwondoa mfalme Yekonia huko Yerusalemu na kumpeleka Babuloni yeye pamoja na wakuu, wafungwa, wenye mamlaka na watu wengine wa kawaida.

Barua kwa watu wa Yerusalemu
10 Basi, watu waliandika hivi: Hizi ndizo fedha tunazowapelekeeni. Kwa fedha hizo tafadhali, nunueni wanyama wa sadaka za kuteketezwa na za kuondolea dhambi na ubani, mtayarishe na tambiko za nafaka, mzitoe juu ya madhabahu ya Bwana Mungu wetu;
11 mwombeeni Nebukadneza mfalme wa Babuloni na mwanawe Belshaza waishi maisha marefu kama vile mbingu.
12 Hapo Bwana atatujalia nguvu na kuyaangaza macho yetu. Tutakaa chini ya ulinzi mwema wa Nebukadneza mfalme wa Babuloni na mwanawe Belshaza na kuwatumikia kwa muda wa siku nyingi na kupata kibali mbele yao.
13 Hali kadhalika, mtuombee na sisi kwa Bwana Mungu wetu, maana tumetenda dhambi dhidi yake Bwana Mungu wetu na mpaka hivi sasa ghadhabu na hasira yake bado vinatukabili.
14 Tafadhali, someni kitabu hiki tunachowapelekeeni, mkaungame dhambi zenu nyumbani mwa Bwana siku ya sikukuu ya vibanda na katika sikukuu nyingine. Kuungama dhambi
15 Hivi ndivyo mtakavyosema: “Bwana Mungu wetu ni mwadilifu, lakini sisi tulivyo leo tumejaa aibu! Sisi sote, watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu,
16 wafalme wetu, wakuu wetu, makuhani wetu, manabii wetu na wazee wetu.
17 Sisi tumetenda dhambi dhidi ya Bwana.
18 Tulimwasi, wala hatukutii sauti ya Bwana Mungu wetu aliposema tuishi kufuatana na amri alizotupa sisi.
19 Tangu siku ile Bwana alipowatoa wazee wetu nchini Misri mpaka leo, tumeendelea kukosa utii kwa Bwana Mungu wetu, tukawa wazembe kuhusu jambo la kusikia sauti yake.
20 Kwa hiyo, mpaka leo hii tumekabiliwa na balaa na laana zile alizotamka Mose mtumishi wa Bwana kwa amri yake, siku ile alipowatoa wazee wetu nchini Misri ili kutupa nchi inayotiririka maziwa na asali.
21 Sisi hatukusikiliza maneno ya manabii ambao Bwana Mungu wetu aliwatuma kwetu.
22 Badala yake, kila mmoja wetu amepania kufuata mipango ya moyo wake mwovu, kwa kutumikia miungu mingine na kufanya yaliyo maovu mbele ya Bwana Mungu wetu.

Generic placeholder image