6

Barua ya Yeremia
1 Hii ni nakala ya barua ambayo Yeremia aliwapelekea Waisraeli, muda mfupi tu kabla ya kuchukuliwa kwao mateka huko Babuloni na mfalme wa Babuloni. Barua yenyewe ina ujumbe ambao Mungu alimwamuru Yeremia awatangazie watu.

Uhamishoni muda mrefu
2 Kwa sababu ya dhambi mlizomtendea Mungu, sasa mfalme Nebukadneza atawachukua mateka Babuloni.
3 Baada ya kuwasili, mtabaki huko kwa muda wa miaka mingi; naam, kwa muda wa vizazi saba. Lakini baadaye, Mungu atawatoeni humo mje nyumbani kwa amani.
4 Huko Babuloni, mtajionea wenyewe miungu iliyotengenezwa kwa fedha, dhahabu na miti; miungu ambayo hubebwa mabegani na watu na kuwatia hofu watu wasiomjua Mungu.
5 Jihadharini sana, msije mkaiga mitindo ya hao watu wa mataifa ya kigeni. Miungu hiyo isiwatie hofu mtakapowaona watu wakiiabudu katika maandamano yao.
6 Ila, jisemeeni moyoni: “Wewe peke yako, ee Bwana, ndiwe tunayepaswa kukuabudu!”
7 Malaika wa Mungu yu pamoja nanyi; yeye atawalinda.

Miungu ya uongo haina nguvu
8 Kwa kweli, miungu hiyo inayo midomo, lakini imechongwa na mafundi; kweli imepakwa dhahabu na fedha, lakini si miungu ya kweli na haiwezi kuongea.
9 Watu hao hutengeneza taji za dhahabu na kuivisha miungu hiyo kichwani, sawa na vile wamfanyiavyo msichana apendaye johari.
10 Hutokea pia kwamba makuhani wao huiba kwa siri fedha na dhahabu hiyo, kwa matumizi yao wenyewe;
11 tena hata huwapa malaya wa hekalu dhahabu na fedha hiyo. Miungu hiyo ya fedha, dhahabu na miti, huvishwa mavazi kana kwamba ni binadamu;
12 lakini haiwezi kujiepusha na kutu au kuliwa na mchwa.
13 Vumbi ya hekalu ikiangukia usoni, watu hulazimika kuipangusa.
14 Miungu hiyo hushika mikononi fimbo ya kifalme, lakini haina uwezo wowote wa kumwangamiza anayeikosea.
15 Hushika sime na shoka mikononi mwao, lakini haiwezi kujilinda vitani au dhidi ya wanyang'anyi.
16 Hiyo hudhihirisha kwamba hiyo miungu si miungu ya kweli. Basi, msiiogope!
17 Kama vile chungu kilichopasuka, ndivyo ilivyo hiyo miungu ya watu wasiomjua Mungu, miungu iliyowekwa mahekaluni; macho yao yamejaa vumbi linalotifuliwa na watu waingiao hekaluni.
18 Na kama vile anavyofungwa mtu anayekabiliwa na hukumu ya kifo kwa kumkosea mfalme, ndivyo makuhani wanavyolinda mahekalu ya miungu hiyo kwa malango yenye makufuli na makomeo ya chuma ili kujikinga na wanyang'anyi.
19 Miungu hiyo huwashiwa taa nyingi kuliko wanavyohitaji wenyewe, lakini haiwezi kuona chochote.
20 Inafanana na mojawapo ya maboriti ya hekalu yaliyogugunwa toka ndani na mchwa iliyotoka ardhini na kuyala na kuharibu pia mavazi yao mazuri. Lakini yenyewe haina habari hata kidogo.
21 Nyuso zao zimekuwa nyeusi kutokana na moshi hekaluni.
22 Popo, mbayuwayu na ndege wengineo hurukaruka na kutua juu ya miili yao na vichwa vyao; hata paka huikalia.
23 Hayo yote yatawadhihirishieni kwamba hiyo si miungu ya kweli. Basi, msiiogope!
24 Na, kuhusu hiyo dhahabu ambayo hiyo miungu imepakwa kuifanya ipendeze, dhahabu yenyewe isiposuguliwa na mtu, haiwezi kung'aa. Ilipokuwa inatengenezwa, yenyewe haikuhisi chochote!
25 Hata ikinunuliwa kwa fedha ya thamani kubwa kiasi gani, haiwezi kabisa kupumua.
26 Hubebwa na watu mabegani kwa sababu haiwezi kutembea kwa miguu yake yenyewe. Hiyo inaonesha watu wazi kwamba haina faida yoyote.
27 Hata hao wanaoihudumia huionea aibu wakati inapoanguka chini, maana hulazimika kuinuliwa tena. Mtu akiisimamisha mahali fulani haiwezi kusogea, na ikikaa kombo haiwezi kujisimamisha wima. Kuipa zawadi ni sawa na kumpa maiti!
28 Makuhani huchukua matambiko yaliyotolewa kwa hiyo miungu na kuyauza kwa faida yao, na wake zao huhifadhi sehemu ya matambiko hayo kwa kuyatia chumvi, badala ya kuwagawia maskini na wasiojiweza.
29 Hata wanawake walio katika hedhi na waliojifungua karibuni huruhusiwa kugusa matambiko hayo. Mambo hayo yawahakikishieni kwamba hiyo si miungu. Basi, msiiogope!
30 Basi, itaitwaje miungu, hali wanawake ndio wanaoitumikia miungu hiyo ya fedha, dhahabu na miti?
31 Hata makuhani hufanya maombolezo yao huko hekaluni wakiwa wamevaa mavazi yaliyotatuka, wamenyoa nywele zao na vichwa wazi.
32 Makuhani hao hupaaza sauti na kupiga kelele mbele ya miungu yao kama watu wafanyavyo kwenye karamu za matanga.
33 Baadhi yao huchukua mavazi ya miungu hiyo na kuwavisha wake zao na watoto wao.
34 Kuitendea miungu hiyo mema au mabaya si neno; yenyewe haiwezi kujilipiza kisasi. Haiwezi kutawaza mfalme wala kumwondoa madarakani.
35 Hali kadhalika haiwezi kumpa mtu utajiri au fedha. Mtu akiiwekea nadhiri, lakini asiitimize, miungu hiyo haiwezi kumdai aitimize.
36 Haiwezi kamwe kumwokoa mtu katika kifo, wala kumlinda mtu dhaifu dhidi ya mwenye nguvu.
37 Haiwezi kamwe kumjalia kipofu kuona wala kumwondoa mtu taabuni.
38 Haiwezi kuwahurumia wajane au kuwasaidia yatima.
39 Madude haya yaliyotengenezwa kwa miti na kupakwa fedha na dhahabu ni kama mawe tu yaliyochongwa kutoka milimani; watu waitumikiao wataaibika.
40 Watu wanawezaje, basi, kuifikiria kuwa miungu au kuiita miungu?

Upumbavu wa kuabudu sanamu Licha ya hayo, hata Wakaldayo wenyewe huidharau miungu hiyo yao.
41 Ikiwa mtu ni bubu, wao humpeleka hekaluni mbele ya Beli na kumwomba amwezeshe kuongea, kana kwamba mungu Beli ana kipawa cha kufahamu chochote.
42 Watu hao hawawezi kufikiri kiasi cha kutosha kuamua kuachana na hiyo miungu isiyo na akili. 43Isitoshe, wanawake hujifunga mishipi na kukaa barabarani wakijifukizia ubani na kufanya umalaya wao. Mmoja wao akichukuliwa na mwanamume na kulala naye, hurudi na kumcheka mwenziwe aliyebaki, eti kwamba si mzuri kama yeye, ndio maana hakuchaguliwa. 44Kila kitu kuhusu miungu hiyo ni uongo mtupu; yawezekanaje, basi, kuifikiria au kuiita miungu?
45 Miungu hiyo imetengenezwa na maseremala na wafua dhahabu; haiwezi, basi, kuwa kitu kingine mbali na kile ambacho mafundi hao walitaka iwe.
46 Hata hao walioitengeneza wenyewe hawaishi muda mrefu! Yawezekanaje basi, vitu hivyo walivyotengeneza watu hao kuwa miungu?
47 Hivyo ndivyo watu wanavyowaachia wazawa wao uongo na aibu. 48Vita au balaa likitokea, makuhani hushauriana wao kwa wao watajificha wapi pamoja na miungu yao hiyo.
49 Vitu hivyo haviwezi kujiokoa vyenyewe wakati wa vita au balaa lifikapo. Kwa nini, basi, watu hawawezi kutambua kwamba sanamu hizo si miungu?
50 Miungu hiyo ni vitu tu vilivyotengenezwa kwa miti, vikapakwa dhahabu na fedha. Zaidi ya hayo, itadhihirika siku moja kwamba yote ni uongo mtupu.
51 Mataifa yote na wafalme watatambua kwamba sanamu hizo si miungu, ila ni vitu tu vilivyotengenezwa kwa mikono ya wanaadamu. Ndani yake hamna utendaji wowote wa Mungu.
52 Nani, basi, asiyeweza kukubali kwamba sanamu hizo si miungu?
53 Hiyo miungu haiwezi kumtawaza mfalme wala kuwapa watu mvua.
54 Haiwezi kutoa kauli juu ya mambo yao yenyewe wala kumsaidia mtu aliyedhulumiwa; haiwezi kabisa kufanya lolote; ni kama kunguru tu wanaorukaruka angani.
55 Patokeapo moto hekaluni, makuhani hutimua mbio kujisalimisha, huku miungu iliyotengenezwa kwa miti na kupakwa fedha na dhahabu huachwa ikateketea kama maboriti. 56Isitoshe, haiwezi hata kupingana na mfalme wala kupigana na adui. Yawezekanaje, basi, kuamini au kuifikiria hiyo kuwa miungu?

Udhaifu wa miungu ya uongo
57 Miungu ya miti iliyopakwa fedha na dhahabu haiwezi kujikinga na wezi au wanyang'anyi
58 ambao huiba fedha na dhahabu na kujiendea zao, huku wamechukua pia mavazi iliyovishwa. Naam, haiwezi kujilinda kabisa!
59 Afadhali mfalme hodari au chombo cha matumizi nyumbani kinachomfaa mwenyewe, kuliko miungu hii ya uongo. Hata afadhali mlango wa nyumba ambao hulinda vitu vilivyomo nyumbani, kuliko hiyo miungu ya uongo. Nguzo moja ya mti katika ikulu ya mfalme ni bora kuliko hiyo miungu ya uongo.
60 Jua, mwezi na nyota, hutii na kutoa mwanga kufuata mwongozo wa Mungu.
61 Hali kadhalika umeme na upepo. Umeme utokeapo huonekana kwa urahisi kila mahali, nao upepo huvuma pande zote.
62 Mungu anapoamuru mawingu kutanda juu ya dunia yote, mawingu hutekeleza amri yake.
63 Mungu anapoteremsha moto kutoka mbinguni kuteketeza milima na misitu, moto hutii amri hiyo. Lakini sanamu za miungu ya uongo haziwezi kufanya mambo hayo, haziwezi hata kuiga mambo hayo.
64 Kutokana na hayo, na kwa vile haziwezi kumhukumu mtu wala kumfaa, haziwezi kamwe kufikiriwa kuwa ni miungu.
65 Basi, nyinyi mwajua kwamba sanamu hizo si miungu. Kwa hiyo, msiziogope!
66 Kwa kweli, miungu hiyo haiwezi kuwalaani wafalme wala kuwabariki.
67 Haiwezi kuyafanyia mataifa ishara angani; haiwezi kuangaza kama jua au mwezi.
68 Hata wanyama wa porini ni bora kuliko hizo sanamu za miungu maana wao wanaweza angalau kukimbia hatari ili kujiokoa.
69 Basi, kwa vyovyote vile, hakuna ushahidi wowote kwamba hiyo ni miungu. Kwa hiyo, msiiogope hata kidogo!
70 Hizo sanamu za miungu zilizotengenezwa kwa miti na dhahabu na fedha, ni kama kinyago cha kufukuzia kunguru katika shamba la matango. Haziwezi kumlinda mtu yeyote.
71 Kadhalika, miungu hiyo ya miti iliyopakwa dhahabu na fedha ni kama kichaka bustanini; badala ya kuwazuia ndege wasije bustanini, huwapatia ndege hao mahali pa kutua. Naam, ni kama mzoga uliotupwa gizani.
72 Mavazi ya kitani ya zambarau na mng'ao wake huozea juu ya miungu hiyo; hivyo mtatambua kwamba, hiyo si miungu hata kidogo. Hatimaye, huliwa na mchwa na kuwa kitu cha kudharauliwa nchini.
73 Basi, afadhali mtu mwadilifu asiye na sanamu za miungu; huyo hatadharauliwa.

Generic placeholder image