4

1 Hekima ni kitabu cha amri za Mungu, yeye ni sheria idumuyo milele. Wanaomshikilia Hekima wataishi, lakini watakaomwacha watakufa.
2 Geuka, ewe Yakobo, umchukue Hekima; tembea kuelekea mng'ao wa mwanga wake.
3 Usimpe mtu mwingine fahari yako; usiwape mataifa ya kigeni mapato yako.
4 Heri yetu sisi, ee Israeli, kwa maana tumejulishwa yampendezayo Mungu.

Ombolezo na matumaini ya Yerusalemu
5 Jipeni moyo enyi watu wangu; watu mnaolidumisha jina la Israeli.
6 Nyinyi hamkuuzwa kwa watu wa mataifa muangamie, bali mlitiwa mikononi mwa maadui zenu kwa sababu mlimkasirisha Mungu.
7 Mlimchokoza yeye aliyewaumba nyinyi, kwa kutoa tambiko kwa pepo badala ya Mungu,
8 Mlimsahau Mungu wa milele aliyewalea mkauhuzunisha mji wa Yerusalemu uliowatunzeni.
9 Mji huo uliiona ghadhabu iliyokujia kutoka kwa Mungu, ukasema: “Sikilizeni enyi jirani za Siyoni. Mungu ameniletea huzuni kubwa,
10 kwa maana nimeuona uhamisho wa watoto wangu, ambao Mungu wa milele amewaletea.
11 Mimi niliwalea kwa furaha, lakini nikawaacha waende kwa machozi na huzuni.
12 Mtu na asifurahie mkasa wangu mimi mjane, mimi niliyefiwa na watoto wengi. Niliachwa mkiwa kwa sababu ya dhambi za wanangu, kwa sababu waligeuka wakaiacha sheria ya Mungu.
13 Hawakuzijali kanuni zake, hawakufuata njia za amri za Mungu, wala kupita katika njia ya uadilifu uliowaonesha.
14 “Enyi jirani zake Siyoni, njoni. Kumbukeni uhamisho wa wanangu, wa kiume na wa kike, uhamisho aliowaletea Mungu wa milele.
15 Maana alileta dhidi yao taifa la mbali, taifa la watu katili na wa lugha ngeni, wasio na heshima kwa wazee wala huruma kwa watoto.
16 Waliwachukua mbali wavulana wapenzi wa mjane, wakaniacha pweke nimefiwa na binti zangu.
17 Lakini mimi nawezaje kuwasaidieni?
18 Ni yule tu aliyewaleteeni balaa hilo ndiye awezaye kuwaokoeni mikononi mwa maadui zenu.
19 Nendeni, watoto wangu, nendeni tu! Mimi nimeachwa mpweke.
20 Nimevua vazi la amani, nimevaa vazi la gunia la kuomba. Nitamlilia Mungu wa milele siku zangu zote.
21 Jipeni moyo enyi watoto wangu! Mlilieni Mungu naye atawaokoeni makuchani mwa maadui.
22 Maana namtumainia Mungu wa milele awaokoeni, na furaha imenijia kutoka kwake huyo Mtakatifu, kwa sababu ya huruma itakayowajia karibuni, kutoka kwa Mwokozi wenu, Mungu wa milele.
23 Kwa huzuni na machozi niliwaacheni mwende, lakini Mungu atawarejesha kwangu kwa shangwe na furaha ya milele.
24 Kama jirani za Siyoni walishuhudia kutekwa kwenu, sasa wataona mkipata wokovu kutoka kwa Mungu, wokovu utakaowajieni kwa utukufu mkubwa, kwa fahari ya Mungu wa milele.
25 Wanangu, vumilieni ghadhabu hiyo iliyowajieni kutoka kwa Mungu. Maadui zenu wamewatesa, lakini mtashuhudia karibuni kuangamizwa kwao, nanyi mtakanyaga shingo zao kwa miguu yenu.
26 Wanangu wapendwa, mmetembea katika njia za taabu; mlichukuliwa kama kundi la kondoo lililochukuliwa na maadui wakali.
27 Jipeni moyo, wanangu, na kumlilia Mungu, kwani yeye aliyewaleteeni jambo hilo atawakumbukeni.
28 Kama vile mlivyokusudia kwenda mbali na Mungu, vivyo hivyo rudini na kumtafuta kwa hamu mara kumi zaidi.
29 Hivyo, huyo aliyewaleteeni balaa hizi atawaokoeni na kuwaleteeni furaha ya kudumu milele.”
30 “Jipe moyo, ee Yerusalemu. Mungu aliyekupa jina lako atakufariji.
31 Ole wao wale waliokutesa, na waliofurahia kuanguka kwako!
32 Miji ile waliyoitumikia watoto wako kama watumwa itakuwa hali mbaya; Mji ule uliowapokea watoto wako utapata balaa!
33 Kama mji huo ulivyoshangilia kuanguka kwako, na kufurahia kuangamia kwako, vivyo hivyo nao utapatwa na uchungu kwa kuangamia kwake.
34 Nitaondolea mbali majivuno yake juu ya wingi wa watu wake, na kiburi chake kitageuka kuwa masikitiko.
35 Mimi Mungu wa milele nitamshushia moto utakaowaka kwa siku nyingi; utakuwa makazi ya pepo kwa muda mrefu.
36 “Angalia upande wa mashariki, ee Yerusalemu, uione furaha inayokujia kutoka kwa Mungu!
37 Tazama, watoto wako uliowaacha waende wanakuja nyumbani, wanakuja pamoja kutoka mashariki na magharibi, Kwa amri ya Mungu Mtakatifu, wanakuja wakishangilia utukufu wake.”

Generic placeholder image