3

1 “Ee Bwana, Mungu Mwenye Nguvu, Mungu wa Israeli, tunakulilia wewe kwa moyo uliotaabika na hoi.
2 Usikilize ee Bwana, na utuhurumie, maana sisi tumetenda dhambi mbele yako.
3 Wewe wadumu milele, lakini sisi, tumeangamia milele!
4 Ee Bwana, Mwenye Nguvu, Mungu wa Israeli! Usikilize sasa sala ya Waisraeli walio kama wafu, sala ya hao waliokukosea, waliokataa kutii sauti yako wewe Bwana Mungu wao, hata balaa zikatuandama.
5 Usikumbuke maovu ya wazee wetu, bali ukumbuke uwezo wako na jina lako.
6 Wewe ni Bwana Mungu wetu, nawe ndiwe tutakayekusifu peke yako.
7 Wewe umeweka mioyoni hali ya uchaji wako ili tupate kukuomba kwa jina lako. Sisi tutakusifu huku uhamishoni tuliko, maana tumeweka mbali nasi uovu wote wa wazee wetu waliokukosea.
8 Tazama, sisi sasa tumo uhamishoni ambamo wewe umetutawanya, tudharauliwe, tulaaniwe na kuadhibiwa kwa sababu ya maovu yote ya wazee wetu ambao walikuacha wewe Bwana Mungu wetu.”

Hekima mwongozo wa Israeli
9 Sikiliza amri za uhai, ewe Israeli! Tega sikio, ukajifunze hekima!
10 Imekuwaje, ee Israeli, imekuwaje uko nchini mwa maadui zako; kwamba umezeeka katika nchi ya kigeni na kutiwa unajisi kwa maiti?
11 Imekuwaje umehesabiwa pamoja na walio kuzimu?
12 Wewe umeiacha chemchemi ya Hekima.
13 Kama ungalifuata njia ya Mungu ungalikuwa unaishi kwa amani milele.
14 Jifunze palipo na Hekima, mahali penye nguvu, mahali penye maarifa, upate kugundua penye maisha marefu na uhai, penye mwanga wa kuangazia macho na penye amani.
15 Nani amewahi kugundua alipo Hekima, Nani aliyefaulu kuingia katika ghala zake?
16 Wako wapi watawala wa mataifa, wale watawalao wanyama duniani kwa mabavu?
17 Wako wapi wale wachezao na ndege wa angani, wenye kurundika fedha na dhahabu ambazo watu huzitegemea, hata hawatosheki kuzitafuta?
18 Wapi waliopanga na kuhangaika kupata fedha tu na ambao kazi zao hazikuacha alama yoyote?
19 Wote hao watoweka na kuishia chini kuzimu, na wengine wamezuka mahali pao.
20 Kizazi kipya kimeikalia nchi, nacho pia kikauona mwanga wa mchana, lakini hakikujifunza njia ya maarifa wala hakikuzijua njia zake, wala hakikufaulu kumpata Hekima.
21 Wazawa wake walipotoka njiani mwa Hekima.
22 Hekima hajapata kusikika Kanaani, wala kuonekana katika Temani.
23 Wazawa wa Hagari watafutao maarifa duniani, wafanyabiashara wa Merani na Temani, wasimulizi wa visa na wenye kutafuta maarifa, hawajajifunza njia ya Hekima, hawajui chochote juu ya njia zake.
24 Ee Israeli, jinsi gani ilivyo kubwa nyumba ya Mungu! Na jinsi gani ilivyo kubwa nchi anayomiliki!
25 Ni kubwa na haina mipaka, haina kimo na haipimiki.
26 Majitu maarufu ya kale yalizaliwa humo; watu wakubwa kwa kimo na stadi vitani.
27 Mungu hakuwateua hao wala kuwajulisha njia ya maarifa.
28 Hivyo waliangamia kwa kutokuwa na hekima; waliangamia kwa upumbavu wao wenyewe.
29 Nani aliyepanda mbinguni akamchukua Hekima, akamleta chini kutoka mawinguni?
30 Nani aliyewahi kusafiri baharini na kumpata? Nani awezaye kumnunua kwa dhahabu?
31 Hakuna mtu ajuaye njia ya kwenda kwake, wala anayejali njia iendayo kwake.
32 Lakini yeye ajuaye kila kitu anamjua Hekima, alimpata kutokana na maarifa yake. Yeye aliyeitayarisha dunia tangu milele aliijaza viumbe vyenye miguu minne.
33 Yeye huutuma mwanga nao huenda; aliuita nao ukamtii kwa hofu.
34 Nyota huangaza mahali pao kwa furaha, yeye huziita nazo husema, “Tupo hapa”. Huangaza kwa furaha kwa ajili yake yeye aliyeziumba.
35 Huyu ni Mungu wetu, hakuna awezaye kulinganishwa naye.
36 Mungu aliigundua njia yote ya maarifa akampatia Yakobo mtumishi wake, naam, akampatia Israeli aliyempenda.
37 Baadaye Hekima alitokea duniani akaishi pamoja na binadamu.

Generic placeholder image