5

1 Ee Yerusalemu, vua vazi lako la huzuni na mateso, ukavae milele uzuri wa utukufu wa Mungu.
2 Jivike joho la uadilifu utokao kwa Mungu; vaa kichwani taji la utukufu wa Mungu wa milele.
3 Maana Mungu atadhihirisha fahari yako kila mahali duniani.
4 Mungu atakupa jina hili milele: “Amani kwa uadilifu; fahari kwa uchaji wa Mungu.”
5 Inuka, ee Yerusalemu, usimame milimani, tazama upande wa mashariki, uwaone watoto wako wamekusanywa kutoka mashariki na magharibi, kwa amri ya Mungu Mtakatifu. Wanashangilia kwani Mungu amewakumbuka.
6 Waliondoka kwako kwa miguu, wakichukuliwa na maadui zako. Lakini Mungu atawarejesha tena kwako wakiwa wamebebwa kwa fahari kama juu ya kiti cha enzi cha mfalme.
7 Mungu ametoa amri: Milima na vilima visawazishwe, na mabonde yafukiwe, nchi yote iwe tambarare, Waisraeli watembee salama kwa utukufu wa Mungu.
8 Kwa amri ya Mungu, vichaka na miti itoayo harufu nzuri itawapa kivuli Waisraeli.
9 Mungu atawaongoza Waisraeli kwa furaha; kwa mwanga wa utukufu wake, kwa uadilifu utokao kwake mwenyewe.

Generic placeholder image