1

Aleksanda Mkuu
1 Aleksanda wa Makedonia, mwana wa Filipo, aliyetoka nchini Kitimu, alimshambulia na kumshinda Dario, mfalme wa Persia na Media, akawa mfalme badala yake. Wakati huo Aleksanda alikwisha kuwa mfalme wa Ugiriki.
2 Alipigana vita vingi, akateka miji yenye ngome na kuwaua wafalme wa nchi hizo.
3 Akasonga mbele hadi miisho ya dunia, akayateka mataifa yasiyohesabika. Hatimaye, ulimwengu wote ulipotulia chini ya utawala wake, aliona fahari kupita kiasi, akajisikia mkuu.
4 Aliunda jeshi lenye nguvu kupindukia, akatawala nchi, mataifa, na wakuu wao; akawalazimisha kulipa kodi kwake.
5 Kisha, mfalme Aleksanda akawa mgonjwa, akahisi kwamba kifo kimekaribia.
6 Basi, akawaita maofisa wake maarufu ambao walikuwa wamelelewa pamoja naye tangu utoto wake, akawagawia milki yake wakati angali hai.
7 Aleksanda alipofariki dunia alikuwa ametawala kwa miaka kumi na miwili.
8 Maofisa wake wakaanza kutawala, kila mmoja katika eneo lake.
9 Wote hao walitawazwa wafalme, Aleksanda alipokufa, na wazawa wao wakawa wafalme baada yao kwa miaka mingi; wakasababisha maovu chungu nzima duniani.

Antioko Epifane na Wayahudi wasiojali sheria
(2Mak 4:7-17)
10 Mmoja wa wazawa hao ni yule mwovu, Antioko Epifane, mwana wa mfalme Antioko. Kabla ya kutawazwa kuwa mfalme mwaka 137 wa enzi ya Wagiriki, Antioko Epifane alikuwa mateka huko Roma.
11 Wakati huo kikazuka kikundi cha Wayahudi wasiojali sheria huko Israeli, ambacho kiliwapotosha watu wengi, kikisema: “Twende kufanya mkataba na jirani zetu wa mataifa mengine, maana tangu tulipojitenga nao tumepata misiba mingi.”
12 Pendekezo hilo likawapendeza watu,
13 na baadhi yao wakamwendea mfalme kwa hamaki. Mfalme akawaruhusu kuzifuata mila na desturi za watu hao wa mataifa mengine.
14 Basi, wakajenga uwanja wa michezo mjini Yerusalemu kwa mtindo wa mataifa mengine.
15 Wakaondoa miilini mwao alama za kutahiriwa, na kuliacha agano takatifu. Walijiunga na watu hao wa mataifa mengine, wakajizamisha katika kutenda maovu.

Antioko aishambulia Misri
16 Alipoona utawala wake umeimarika, Antioko aliazimu kuiteka Misri na kuwa mfalme wa nchi hiyo pia, licha ya Siria.
17 Kwa hiyo akaivamia Misri kwa jeshi lake kali lenye magari ya kukokotwa, tembo, askari wapandafarasi, na msururu wa vyombo vya baharini.
18 Vita vilipopamba moto, Tolemai, mfalme wa Misri, akarudi nyuma na kukimbilia mbali. Wengi wa askari wake walijeruhiwa na kuuawa.
19 Miji yenye maboma ilikamatwa, na nchi ya Misri ikatekwa.

Antioko awadhulumu Wayahudi
20 Baada ya kuiteka Misri, Antioko, pamoja na jeshi lake lenye nguvu, aliikabili nchi ya Israeli, 143, akawasili mjini Yerusalemu.
21 Kwa majivuno aliingia hekaluni na kujichukulia madhabahu ya tambiko, kinara cha taa na vifaa vyake vyote.
22 Pia alitwaa meza ya mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, vikombe vitakatifu, mabakuli, vyetezo vya dhahabu, pazia, na mataji. Akayabandulia mbali mapambo ya dhahabu katika ukuta wa mbele wa hekalu.
23 Akavichukua vyombo vya fedha na vya dhahabu na vya thamani. Hali kadhalika, akatwaa na vitu vyote vya tunu alivyovikuta vimefichwa.
24 Akabeba hivyo vyote na kwenda navyo nchini kwake. Alikuwa amemwaga damu nyingi sana, na akawa anajigamba sana juu yake.
25 Kilio kilikuwa kikubwa katika Israeli yote;
26 watawala na wazee walilia kwa huzuni wasichana na wavulana wakanyong'onyea; uzuri wa wanawake ukatoweka.
27 Kila bwanaharusi aliomboleza; kila bibiarusi chumbani mwake alilia.
28 Nchi ilitetemeka kwa ajili ya wakazi wake, na jamii yote ya Yakobo ilivikwa fedheha.
29 Miaka miwili baadaye, mfalme Antioko alimtuma mtozaushuru mkuu kwa miji ya Yudea. Huyo aliwasili Yerusalemu, akisindikizwa na jeshi kubwa la askari.
30 Lugha yake ilikuwa tamu, lakini yenye hila. Kwani, mji wote ulipomwamini, ghafla akauvamia na kuupiga vibaya sana. Aliwaua watu wengi wa Israeli,
31 akauteka na kuuchoma moto mji wa Yerusalemu, akazibomoa nyumba na kuta za kila upande,
32 akawachukua mateka wanawake, watoto, na mifugo.
33 Halafu Antioko na majeshi yake wakajenga kuta ndefu na minara imara kuuzunguka mji wa Daudi; ikawa ngome yao.
34 Kisha akaweka hapo watu ovyo, wasiojali sheria, walinde. Hao waliimarisha ulinzi wao;
35 walikusanya na kuhifadhi silaha na chakula, wakaokota nyara zote walizoteka Yerusalemu, wakaziweka ngomeni. Ngome hiyo ilikuwa tishio kubwa kwa mji wa Yerusalemu.
36 Ilikuwa tishio kubwa kwa hekalu, hatari mbaya ya kudumu kwa Israeli.
37 Watu wasio na hatia waliuawa kandokando ya madhabahu; mahali patakatifu pakatiwa unajisi hivyo.
38 Wakazi wa Yerusalemu wakakimbia kwa sababu yao, mji ukawa makao ya wageni, ukawa wa kigeni kwa watu wake, na watoto wake wakauacha.
39 Hekalu lake likawa tupu kama jangwa; sikukuu zake zikageuka kuwa maombolezo, furaha ya Sabato zake ikageuka kuwa lawama, na heshima yake ikawa fedheha.
40 Aibu ya kuanguka kwake ililingana na utukufu wake wa awali; na fahari yake ikageuka kuwa maombolezo.
41 Kisha, mfalme Antioko akaandika agizo kwa watu wote katika milki yake wawe taifa moja,
42 na kwamba kila mtu aachilie mbali mila na desturi zake.
43 Watu wote wa mataifa mengine waliipokea amri hiyo ya mfalme. Watu wengi hata Waisraeli wakaifuata dini yake kwa furaha; wakatambika kwa vinyago vya miungu na kuitia unajisi siku ya Sabato.
44 Naye mfalme akawatuma watu kupeleka barua Yerusalemu na kwenye miji ya Yudea, akiamuru kwamba watu wafuate mila na desturi hizo za kigeni.
45 Aliwakataza wasitoe tambiko za kuteketezwa, tambiko za nafaka wala sadaka za vinywaji hekaluni. Aliamuru Sabato na sikukuu ziwe siku za kawaida.
46 Watu waliamriwa kulitia najisi hekalu na wahudumu wake,
47 kujenga madhabahu, mahekalu na mahali patakatifu kwa ajili ya vinyago vya miungu, kutoa sadaka ya nguruwe na wanyama najisi,
48 na kuwaacha wana wao bila kutahiriwa. Walitakiwa kujitia unajisi kwa kila namna waliyoweza,
49 ili waisahau sheria na kubadili mila na desturi zao zote.
50 Yeyote aliyekaidi amri ya mfalme alihukumiwa kifo.
51 Licha ya kuieneza amri hiyo katika milki yake yote, mfalme Antioko aliwateua wakaguzi wa kusimamia utekelezaji wake, akaamuru watu wa miji yote ya Yudea watoe tambiko kwa miungu.
52 Wengi wa Wayahudi, yaani wale walioiasi sheria, waliwatii wasimamizi hao. Hivi wakaitia unajisi nchi kwa uovu wao,
53 na kuwafanya watu waaminifu wa Israeli watoroke na kujificha popote walipoweza.
54 Siku ya kumi na tano ya mwezi wa Kislevu, mwaka 145, mfalme Antioko aliisimamisha lile Chukizo Haribifu juu ya madhabahu kuu ya sadaka za kuteketezwa hekaluni, na vimadhabahu vya miungu vikajengwa katika miji yote ya Yudea,
55 wakawa wanafukiza ubani milangoni mwa kila nyumba na mitaani.
56 Vitabu vyovyote vya sheria walivyoviona walivichanachana na kuvichoma moto.
57 Yeyote aliyeshikwa ana kitabu cha agano au anaifuata sheria, aliuawa kwa amri ya mfalme.
58 Mwezi hata mwezi, watu hao waovu walitumia mabavu dhidi ya Waisraeli waliokamatwa katika miji mbalimbali.
59 Siku ya ishirini na tano ya mwezi huo huo, watu hao walitoa tambiko katika kimadhabahu kilichosimamishwa juu ya madhabahu kuu ya sadaka za kuteketezwa hekaluni.
60 Kwa mujibu wa amri iliyotolewa, waliwaua wanawake wote waliowaruhusu watoto wao kutahiriwa,
61 na jamaa zao na wale waliowatahiri watoto hao; na watoto wenyewe wakawanyonga kwa kuwaning'iniza shingoni mwa mama zao.
62 Hata hivyo, wengi katika Israeli walisimama imara, wakaamua kwa dhati kutokula chakula najisi.
63 Walikuwa tayari kufa kuliko kuvunja agano takatifu na kula chakula najisi - na kwa kweli, wengi waliuawa.
64 Ghadhabu kubwa iliwapata Waisraeli.

Generic placeholder image