7

Kuhani mkuu Alkimo na kampeni ya Nikanori
(2Mak 14:1-36; 15:1-36)
1 Mwaka 151, Demetrio mwana wa Seleuko aliondoka Roma, akawasili katika mji mmoja wa mwambao wa Bahari ya Mediteranea akiwa na watu wachache. Huko akajitangaza mfalme.
2 Alipokuwa anaelekea kwenye ikulu ya wazee wake, askari waliwakamata Antioko wa Tano na Lisia ili wawapeleke kwa Demetrio.
3 Lakini Demetrio aliposikia mpango huo, akasema: “Sitaki kuwaona.”
4 Basi, askari wakawaua Antioko wa Tano na Lisia, naye Demetrio akakalia kiti cha ufalme.
5 Ndipo Wayahudi wote waasi na wasiomjali Mungu, wakiongozwa na Alkimo aliyetamani kuwa kuhani mkuu, wakamwendea Demetrio.
6 Wakawalaumu Wayahudi wenzao na kusema: “Yuda na ndugu zake wamewaua rafiki zako wote, na wametufukuza sisi kutoka katika nchi yetu.
7 Sasa, umtume mtu unayemwamini aende akaone jinsi mali yetu ilivyoteketezwa, na nchi ya mfalme ilivyoharibiwa, akawaadhibu Yuda na nduguze na wasaidizi wao wote.”
8 Basi, mfalme akamchagua Bakide, mmoja wa washauri wake, ambaye alikuwa mkuu wa mkoa wa Ng'ambo ya Mto. Bakide alikuwa mtu wa maana katika milki, na mwaminifu kwa mfalme.
9 Basi, mfalme alituma pamoja na yule mwovu Alkimo, ambaye alikuwa ameteuliwa na mfalme kuwa kuhani mkuu; akamwamuru kuwalipa kisasi Wayahudi.
10 Hao waliondoka Antiokia, wakawasili Yudea na jeshi kubwa. Bakide akajaribu kuwadanganya Yuda na nduguze kwa kuwatuma kwao wajumbe wenye maneno ya kutaka amani.
11 Lakini Yuda na nduguze walipoona wamekuja na jeshi kubwa, hawakuamini maneno ya wajumbe hao.
12 Kisha kikundi cha waalimu wa sheria kilifika kwa Alkimo na Bakide kutaka masharti ya haki.
13 Hao Wahasidi walikuwa Wayahudi wa kwanza waliojaribu kuomba amani kwa Alkimo na Bakide.
14 Walifikiri kwamba Alkimo ambaye ni kuhani wa ukoo wa Aroni amekuja na jeshi, asingewadhuru kwa vyovyote.
15 Alkimo aliongea nao maneno ya amani, na akaahidi kwa kiapo, akisema: “Hatutajaribu kuwadhuru wala nyinyi wenyewe, wala rafiki zenu.”
16 Basi, wakamwamini. Lakini mara akawashika watu 60 miongoni mwao na kuwaua siku hiyohiyo, kama ilivyoandikwa:
17 “Damu ya watu wako waaminifu ilimwagwa, maiti zao zilitupwa ovyo Yerusalemu; hapana aliyebaki kuwazika wafu.”
18 Watu wote wakawaogopa Alkimo na Bakide, wakasema: “Hawaelewi ukweli au haki maana yake nini. Waliahidi kwa kiapo, kisha wakavunja ahadi yao!”
19 Bakide akaondoka Yerusalemu na kufanya makao yake huko Beth-zaithi. Akaamuru wasakwe na washikwe baadhi ya Wayahudi waliomwasi, na baadhi ya wengine, akawaua na kutupa maiti zao shimoni.
20 Halafu akamkabidhi Alkimo utawala wa nchi, akamwachia vikosi vya askari wa kumsaidia, akarejea kwa mfalme.
21 Ndipo Alkimo akaanza harakati za kuimarisha ukuhani wake mkuu.
22 Wachokozi wote nchini wakajiunga naye. Waliikamata na kuitiisha nchi ya Yudea, wakasababisha hasara kubwa katika Israeli.
23 Yuda aliyaona maovu yote ambayo Alkimo na wenzake walikuwa wametenda miongoni mwa Waisraeli; yalikuwa zaidi kuliko yale yaliyotendwa na watu wa mataifa mengine.
24 Basi, Yuda akazunguka katika nchi nzima ya Yudea, akilipa kisasi kwa wote waliomtoroka yeye na kujiunga na Alkimo, akawazuia wasiondoke mijini na kwenda shamba.
25 Alkimo alipoona Yuda na watu wake wanaongezeka nguvu, na alipotambua kwamba asingeweza kushindana nao, akarudi kwa mfalme na kuwasingizia mabaya akina Yuda.
26 Ndipo mfalme akamtuma Nikanori, mmoja wa maofisa wake wastahiki na ambaye aliwachukia sana Wayahudi, akimwamuru akawaangamize na kuwafutilia mbali Wayahudi.
27 Basi, Nikanori akafika Yerusalemu na jeshi kubwa. Akajaribu kuwadanganya Yuda na nduguze kwa ujumbe wa amani,
28 akisema: “Hapana haja yoyote ya kuwa na mapambano kati yenu na sisi. Nitafika kwenu na watu wachache kwa mazungumzo ya amani, ya ana kwa ana.”
29 Nikanori akamwendea Yuda, wakaamkiana kirafiki. Kumbe, maadui walikuwa wanajiandaa kumkamata Yuda.
30 Alipogundua kwamba ujio wa Nikanori ulikuwa na hila dhidi yake, Yuda alimwogopa, akakataa kukutana naye tena.
31 Nikanori akatambua kwamba mpango wake ulikuwa umegunduliwa. Basi, akaondoka Yerusalemu na kwenda kupigana na Yuda karibu na Kafar-salama.
32 Yapata watu 500 wa jeshi la Nikanori waliuawa, na walionusurika wakakimbilia kwenye ngome ya mji wa Daudi.
33 Baada ya matukio hayo, Nikanori akaenda Mlimani Siyoni. Baadhi ya makuhani na wazee wa watu wakamlaki kwa maneno ya amani, wakamwonesha na sadaka ya kuteketezwa iliyokuwa inatolewa kwa ajili ya mfalme.
34 Lakini Nikanori akawadharau na kuwatia unajisi, na kuongea kwa majivuno.
35 Kwa hasira akaapa: “Kama Yuda na jeshi lake hawajisalimishi kwangu sasa, nitalichoma moto hekalu hili mara nitakaporudi baada ya kushinda vita.” Akaondoka kwa hasira.
36 Kwa hiyo, wale makuhani wakaingia ndani, wakasimama kuelekea madhabahu na hekalu, wakalia na kusema:
37 “Bwana, ulichagua hekalu hili liitwe kwa jina lako, na liwe nyumba ya sala na maombi kwa ajili ya watu wako.
38 Sasa, mpe adhabu mtu huyu na jeshi lake; wote na wauawe kwa upanga. Kumbuka kufuru zao; usiwaache waishi tena.”
39 Nikanori akaondoka Yerusalemu, akapiga kambi yake Beth-horoni. Jeshi la Siria likajiunga naye hapo.
40 Yuda naye akapiga kambi Adasa, akiwa na watu 3,000. Kisha akasali, akisema:
41 “Bwana, wajumbe waliotumwa na mfalme walipokutukana, malaika wako aliwaulia mbali Waashuru 185,000.
42 Sasa, kwa namna hiyohiyo, ulipondeponde jeshi hili leo mbele yetu, na kila mtu ajue kwamba Nikanori anaadhibiwa kwa sababu alilidharau hekalu lako takatifu. Mwadhibu kulingana na uovu wake.”
43 Siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari, majeshi yalipambana vitani. Jeshi la Nikanori likashindwa. Nikanori mwenyewe alikuwa wa kwanza kuuawa vitani,
44 na askari wake walipoona ameuawa, walitupa chini silaha zao, wakakimbia.
45 Wayahudi wakawafuatia hao maadui mchana kutwa, kutoka Adasa hadi Gazara. Wakati wanawaandama hao, waliendelea kupiga tarumbeta za mbiu ya vita.
46 Watu wakajitokeza kutoka vijiji vyote vya jirani nchini Yudea, wakawashambulia maadui waliokuwa wanakimbia. Maadui wakalazimika kurudi nyuma, walikokumbana na jeshi lililokuwa linawafuatia. Maadui wote waliuawa katika mapigano hayo; hakusalia hata mmoja wao.
47 Kisha Wayahudi wakachukua nyara na mateka, wakamkata Nikanori kichwa na ule mkono wake wa kuume aliokuwa ameunyosha kwa ufidhuli, wakavipeleka Yerusalemu na kuvitundika nje.
48 Wayahudi walifurahi sana, wakaiadhimisha siku hiyo kama siku ya furaha kubwa,
49 na kuagiza iadhimishwe kila mwaka, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari.
50 Kwa kitambo nchi ya Yudea ikawa na amani.

Generic placeholder image