2

Uaminifu wa Matathia
1 Wakati huo, Matathia mwana wa Yohane na mjukuu wa Simeoni, kuhani wa ukoo wa Yoaribu, alitoka Yerusalemu akaenda kukaa Modeini.
2 Alikuwa na watoto watano wa kiume: Yohane aliyeitwa pia Gadi,
3 Simoni aliyeitwa Thasi,
4 Yuda aliyeitwa Makabayo,
5 Eleazari aliyeitwa Avarani, na Yonathani aliyeitwa Afusi.
6 Matathia alipoona kufuru zote zilizotendwa huko Yudea na Yerusalemu,
7 akasema: “Maskini mie! Kwa nini nilizaliwa nione maovu haya, kuharibiwa kwa watu wangu, kuangamizwa kwa mji mtakatifu? Nikae mie hapa naangalia tu, ambapo mji mtakatifu unatiwa mikononi mwa adui, na hekalu linaachiwa watu wageni?
8 Hekalu limekuwa kama mtu asiye na heshima.
9 Vyombo vyake vya fahari vimetekwa na kuchukuliwa. Watoto wake wadogo wameuawa barabarani, vijana wake wamechinjwa kwa upanga wa adui.
10 Kila taifa ulimwenguni limeukalia mji wetu, na kuzipora mali zake!
11 Mapambo yake yote yameondolewa na kuchukuliwa; sasa ni mtumwa, si mji huru tena.
12 Litazameni hekalu letu; halina uzuri wala utukufu wowote, watu wa mataifa wamelikufuru.
13 Kwa nini tuendelee kuishi?”
14 Ndipo Matathia na wanawe wakararua mavazi yao, wakavaa magunia na kulia kwa majonzi na uchungu mkali.
15 Halafu maofisa wa mfalme, wale waliokuwa wanawalazimisha watu kumwasi Mungu, wakafika mjini Modeini kuwashurutisha wakazi wake kutambika.
16 Waisraeli wengi wakawajia hao maofisa, wakiwamo miongoni mwao Matathia na wanawe.
17 Maofisa wa mfalme wakamwambia Matathia, “Wewe ni kiongozi unayeheshimiwa katika mji huu, na unaungwa mkono na wanao na jamaa zako.
18 Kwa nini usiwe wa kwanza sasa kutekeleza amri ya mfalme? Watu wote wa mataifa mengine, wananchi wote wa Yudea, na watu wote waliobaki Yerusalemu wamekwisha tekeleza hilo. Kama utatimiza amri ya mfalme, wewe na wanao mtapewa heshima kubwa na kuitwa ‘Marafiki wa Mfalme,’ na mtatunukiwa fedha na dhahabu na zawadi nyingine nyingi.”
19 Matathia akajibu kwa sauti kubwa, “Hata kama mataifa yote yaliyo chini ya utawala wa mfalme yametii na kushika amri yake, na hivi kuachana na dini zao za jadi,
20 mimi na wanangu na ndugu zangu tutaendelea kushika agano ambalo Mungu alifanya na wazee wetu.
21 Kwa msaada wa Mungu, kamwe hatutaitupa sheria yake, wala kuzivunja amri zake Mungu.
22 Amri ya mfalme hatutaishika kamwe, na hatutabadili chochote katika ibada zetu!”
23 Wakati Matathia anamalizia kusema haya, Myahudi mmoja wa Modeini alijitokeza mbele ya wote, akataka kutoa tambiko juu ya madhabahu iliyokuwa hapo, kufuatana na amri ya mfalme.
24 Matathia alipomwona, akawaka ghadhabu na moyo kulipuka. Huku anatetemeka kwa hasira, akamwendea mbio na kumuua papo hapo juu ya madhabahu.
25 Pia akamuua ofisa wa mfalme aliyekuwa anawalazimisha watu kutoa tambiko, akaibomolea mbali madhabahu hiyo.
26 Kwa namna hiyo Matathia alionesha ari yake kwa sheria, kama vile Finehasi alivyokuwa ameonesha alipomuua Zimri, mwana wa Salu.

Vita chini ya uongozi wa Matathia
27 Halafu Matathia akapita mjini akisema kwa sauti kubwa: “Kila aliye na ari kwa ajili ya sheria ya Mungu, na anayeliunga mkono agano lake, na anifuate!”
28 Matathia mwenyewe na wanawe wakakimbilia milimani na kuviacha vyote walivyokuwa navyo mjini.
29 Wakati huo Waisraeli wengi waliotaka kushikilia dini yao na sheria wakateremka na kufanya maskani yao nyikani,
30 wao pamoja na wana wao, wake zao, na mifugo yao, maana mateso yao yalikuwa yamewasonga.
31 Basi, taarifa ikawafikia maofisa wa mfalme na wanajeshi waliokuwa Yerusalemu, mji wa Daudi, kwamba watu waliokataa kutii amri ya mfalme walikuwa wamekimbilia chini mafichoni nyikani.
32 Wanajeshi wengi wakawaandama, wakawakuta na kujitayarisha kuwashambulia siku ya Sabato.
33 Basi wakawaambia, “Yatosha sasa! Tokeni nje na kutekeleza amri ya mfalme, nanyi mtaishi.”
34 Lakini wao wakasema, “Kamwe hatutatoka nje! Wala amri ya mfalme hatutaishika na kuitia unajisi siku ya Sabato.”
35 Basi, mara moja maadui hao wakaanza kuwashambulia Wayahudi.
36 Lakini wao hawakurudisha mashambulio, wala kuwatupia jiwe, wala kuwazuia wasiingie katika maficho yao,
37 maana walisema, “Na tufe sote tukiwa wenye dhamiri safi. Mbingu na dunia zitushuhudie kwamba mnatuua bila haki.”
38 Hivi wakawashambulia siku ya Sabato na kuwaua watu 1,000, wanaume, wanawake na watoto. Mifugo pia wakaiteketeza.
39 Matathia na rafiki zake walipopata habari hiyo, waliwalilia sana wenzao.
40 Na kila mmoja wao akamwambia mwenzake: “Kama sote tutafanya walivyofanya hawa ndugu zetu na kukataa kupambana na maadui ili kutetea maisha yetu na dini yetu, punde si punde watatufutilia mbali kutoka duniani.”
41 Basi, siku hiyo wakaamua kwamba kama yeyote yule atawashambulia siku ya Sabato, watajitetea, wasije wakauawa wote kama Wayahudi wenzao walivyouawa mafichoni mwao.
42 Ndipo walipojiunga nao watu wa kikundi cha Wahasidi ambao walikuwa mashujaa wa vita katika Israeli na walio tayari kabisa kuitetea sheria.
43 Tena kila mmoja aliyeamua kukimbia na kujiepusha na dhuluma hiyo alijiunga nao na kuzidi kuwaimarisha.
44 Basi, walikusanya jeshi, na kwa hasira yote wakawashambulia Wayahudi ambao hawakujali sheria. Wale walioponea chupuchupu wakakimbilia usalama kwa watu wa mataifa mengine.
45 Matathia na rafiki zake wakapita huko na huko wakibomoa madhabahu za miungu,
46 na kuwatahiri kwa nguvu wavulana wote waliowakuta hawajatahiriwa nchini Israeli.
47 Pia walifanikiwa kuwatia nguvuni maofisa mafidhuli wa mfalme.
48 Hivi wakaiokoa sheria ya Mose makuchani mwa watu wa mataifa mengine na wafalme wake, na hawakumwacha mwenye dhambi ashinde.

Kifo cha Matathia
49 Matathia alipoona kwamba siku yake ya kufa imekaribia, aliwaambia wanawe: “Sasa kiburi na dharau vimepamba moto. Sasa ni wakati wa maangamizi na ghadhabu kali!
50 Hata hivyo, nyinyi, wanangu, lazima mjitoe mhanga kwa ajili ya sheria, na kutoa maisha yenu kwa ajili ya agano la wazee wetu.
51 “Kumbukeni waliyofanya wazee wetu nyakati zao, nanyi mtatunukiwa taji ya utukufu na sifa milele.
52 Kumbukeni jinsi Abrahamu alivyokuwa mwaminifu pale alipojaribiwa, akakubaliwa kuwa mwadilifu.
53 Yosefu, alipokuwa katika matatizo, alitii amri za Mungu, akawa mtawala wa nchi ya Misri.
54 Mzee wetu Finehasi, kwa sababu ya uchaji na ari yake kuu, aliahidiwa kwamba wazawa wake daima watakuwa makuhani.
55 Yoshua alifanywa mwamuzi katika Israeli kwa sababu alitii amri.
56 Kalebu alileta taarifa nzuri kwa jumuiya, akapewa zawadi sehemu ya ardhi.
57 Daudi kwa kuwa alikuwa na huruma alirithi kiti cha enzi cha ufalme milele.
58 Elia, kwa sababu ya ari yake kuu kwa ajili ya sheria, alichukuliwa juu mbinguni.
59 Hanania, Azaria na Mishaeli waliokolewa katika moto kwa sababu walikuwa na imani.
60 Danieli alikuwa mtu mwadilifu, naye Bwana akamwokoa kinywani mwa simba.
61 Kila mmoja wa hao wazee wetu ni kielelezo wazi kwamba kila anayemtumainia Mungu hakosi msaada.
62 “Msiogope vitisho vya mtu mwovu. Kumbukeni ya kwamba huyo naye atakufa, na fahari yake yote itakoma, na mwili wake utaoza na kuliwa na wadudu.
63 Leo anaweza akatukuzwa na kusifiwa, lakini kesho atatoweka; mwili wake utarudi mavumbini, na mipango yake itaishia hewani.
64 Lakini nyinyi, wanangu, pigeni moyo konde, simameni imara katika kushika sheria, maana kwa sheria mtajipatia utukufu na sifa.
65 “Kaka yenu Simoni ana busara na hekima. Hivi, msikilizeni yeye daima kama vile mngenisikiliza mimi baba yenu.
66 Yuda Makabayo amekuwa shujaa wa vita tangu ujana wake; atakuwa kamanda wenu wa jeshi, na kuongoza mapambano dhidi ya maadui.
67 Yeyote anayeshika sheria, mwalikeni ajiunge nanyi; halafu lipeni kisasi kwa maovu waliyotendewa watu wenu.
68 Walipeni watu wa mataifa mengine kadiri ya walivyowatendeni; daima shikeni maagizo ya sheria.”
69 Kisha, Matathia akawabariki, akaaga dunia.
70 Alizikwa katika kaburi la babu zake kule Modeini, na watu wote wa Israeli wakalia na kuomboleza kwa kifo chake. Hayo yalitukia katika mwaka wa 146.

Generic placeholder image