9

Kifo cha Yuda
1 Demetrio aliposikia kwamba Nikanori na jeshi lake wameangamizwa vitani, akawapeleka tena nchini Yudea Bakide na Alkimo, pamoja na vikosi vya kulia vya jeshi lake.
2 Wakapita njia ielekeayo Gilgali na kupiga kambi huko Arbela, mkabala na Mesalothi. Wakauteka mji wa Mesalothi na kuwaua watu wengi.
3 Mwezi wa kwanza wa mwaka 152, wakapiga kambi mkabala na Yerusalemu.
4 Kutoka hapo kambini wakaenda Berea na askari wa miguu 20,000, na wapandafarasi 2,000.
5 Yuda alikuwa amepiga kambi Elasa, akiwa na askari 3,000 waliochaguliwa.
6 Lakini walipoona idadi kubwa ya wanajeshi adui, wakashikwa na hofu vibaya sana. Wengi wakatoroka kutoka kambini, wakabaki askari wa Kiyahudi 800 tu.
7 Yuda alipoona jeshi lake linazidi kupunguka na vita karibu vinaanza, alivunjika moyo, kwa vile hakuwa na muda wa kulikusanya tena jeshi lake.
8 Alikuwa amekata tamaa. Hata hivyo, akawaambia wale waliobaki naye: “Tujiandae kwa mapambano; huenda tukawashinda maadui.”
9 Lakini watu wake wakajaribu kumzuia wakisema, “Hatuwezi kuwashinda. Tukitaka kuokoa maisha yetu, turudi nyumbani sasa. Halafu tunaweza kuja tena pamoja na ndugu zetu; hapo tutawapiga maadui. Lakini kwa sasa sisi ni wachache mno.”
10 Yuda akajibu: “Ni aibu kwetu kufanya hivyo na kukimbia vita! Kama ajali yetu imefika, basi, na tufe kishujaa kwa ajili ya ndugu zetu Wayahudi. Tusichafue jina letu!”
11 Hapo jeshi la Bakide likatoka kambini na kujipanga, tayari kuwashambulia Wayahudi. Askari wapandafarasi waligawanywa katika vikosi viwili. Askari hodari waliwekwa mstari wa mbele, lakini wapiga mishale na askari wenye makombeo walitangulizwa mbele kabisa.
12 Bakide mwenyewe alijipanga upande wa kulia. Askari wa miguu wakaanza kusonga mbele, wakiwa wamekingwa pande zote mbili na wapandafarasi. Tarumbeta za vita zilikuwa zinapigwa. Na askari wa Yuda nao wakapiga tarumbeta zao.
13 Ardhi ilitetemeka majeshi hayo mawili yalipokutana; yalipigana toka asubuhi mpaka jioni.
14 Yuda aligundua kwamba Bakide na askari wenye hatari wa jeshi lake walikuwa upande wa kulia. Basi, mashujaa wake wote wakajiunga naye,
15 wakawapondaponda askari wa kulia wa Bakide, na kuwafuatia mpaka mlima Azoto.
16 Lakini wanajeshi wa Siria waliokuwa upande wa kushoto walipoona wenzao wa upande wa kulia wamepigwa vibaya, waligeuka na kumfuata Yuda na watu wake kwa nyuma.
17 Mapambano yalikuwa makali sana. Askari wengi wa pande zote mbili, walipoteza maisha yao.
18 Hatimaye Yuda mwenyewe aliuawa. Ndipo watu wake wote wakakimbia.
19 Yonathani na Simoni wakachukua maiti ya ndugu yao na kumzika katika kaburi la babu zao kule Modeini.
20 Wakaketi hapo kaburini na kumlilia Yuda. Waisraeli wote waliomboleza na kumlilia kwa siku nyingi, wakisema:
21 “Jinsi gani mwenye nguvu ameanguka, yeye aliye mwokozi wa Israeli!”
22 Na matendo mengine ya Yuda, mapambano aliyoendesha, ujasiri wake, na mafanikio yake makubwa hayakuandikwa, maana yalikuwa mengi mno.

Yonathani kiongozi baada ya Yuda
23 Baada ya kifo cha Yuda, wale waasi wasioshika sheria walianza kuonekana tena kila mahali katika Yudea, na waovu wote wakatokea tena.
24 Wakati huo huo njaa kali iliingia, na nchi nzima ikawa upande wa waovu hao.
25 Hivi, Bakide kwa makusudi kabisa akawateua baadhi ya Wayahudi hao waasi wawe watawala wa nchi.
26 Basi, wakawasaka rafiki za Yuda na kuwafikisha wote mbele ya Bakide. Bakide akawatesa na kuwanyenyekesha.
27 Ulikuwa wakati wa matatizo na huzuni kubwa zaidi kuliko wakati manabii walipoanza kutoweka miongoni mwa Waisraeli.
28 Ndipo marafiki wote wa Yuda wakakusanyika pamoja na kumwambia Yonathani:
29 “Tangu ndugu yako Yuda alipofariki dunia, hajatokea mwingine kama yeye wa kutuongoza dhidi ya maadui zetu, dhidi ya Bakide na Wayahudi wenzetu wanaotupinga.
30 Kwa hiyo leo tunakuchagua wewe kuwa mtawala na kamanda wetu badala yake, tuendeleze mapambano yetu.”
31 Yonathani akapokea uongozi siku hiyo, akatwaa nafasi ya nduguye, Yuda.

Kampeni za Yonathani
32 Bakide alipogundua jambo hilo, aliamua kumwua Yonathani.
33 Lakini Yonathani alipopata habari ya njama hizo, akakimbilia kwenye nyika ya Tekoa, yeye na nduguye, Simoni, na watu wao. Huko wakapiga kambi karibu na bwawa la Asfari.
34 (Bakide alipata habari kuhusu jambo hilo siku ya Sabato, akavuka mto Yordani pamoja na jeshi lake lote.)
35 Yonathani akamtuma nduguye, Yohane, aliyezishughulikia familia za askari, akawaombe Wanabatea, rafiki zake Yonathani, ruhusa ya kuhifadhi katika ghala yao vitu vyao vingi walivyokuwa navyo.
36 Lakini watu wa jamaa ya Yambri kutoka Medeba wakamshambulia Yohane, wakamteka nyara na kupora vitu vyote alivyokuwa navyo.
37 Baada ya kitambo, Yonathani na nduguye Simoni, walipata habari kwamba jamaa ya Yambri ilikuwa karibu kusherehekea harusi kubwa, kwamba pangekuwa na maandamano makubwa ya kumsindikiza bibiarusi kutoka mji wa Nadabathi. Bibiarusi alikuwa binti ya mmoja wa wakuu wa Kanaani.
38 Yonathani na Simoni wakaamua kulipa kisasi kwa damu ya ndugu yao, Yohane, iliyomwagwa. Wao na watu wao wakapanda mlima mmoja na kujificha.
39 Waliangalia, wakaona kundi la watu waliobeba mizigo, wanapita wakipiga kelele. Bwanaharusi, rafiki zake, na jamaa zake walikuwa wanakwenda kukutana nao. Walikuwa wamebeba silaha, huku wanapiga ngoma na ala nyingine za muziki.
40 Hapo Wayahudi wakatoka kwenye maoteo yao, wakawashambulia na kuwaua wengi wao; walioponea chupuchupu wakakimbilia milimani. Wayahudi wakachukua mali yao yote.
41 Hivi, harusi hiyo iligeuka kuwa matanga, na nyimbo za shangwe zikawa maombolezo ya huzuni.
42 Yonathani na Simoni walipokwisha lipiza kisasi kifo cha ndugu yao walirejea kwenye mabwawa ya Yordani.
43 Bakide akapata habari juu ya hayo. Siku ya Sabato akawasili na jeshi kubwa kwenye kingo za mto Yordani.
44 Yonathani akawaambia watu wake: “Sasa ni lazima tupigane kufa na kupona. Tumezingirwa vibaya sana, kuliko wakati mwingine wowote ule.
45 Adui yuko mbele yetu. Nyuma yetu kuna mto. Kulia na kushoto kwetu kuna mabwawa na vichaka. Tutatorokea wapi?
46 Basi, ombeni Bwana atuokoe na makucha ya adui.”
47 Mapambano yalianza. Yonathani alinyosha mkono wake ili kumwulia mbali Bakide. Lakini Bakide aliepa, akatorokea mstari wa nyuma wa jeshi lake.
48 Basi, Yonathani na watu wake wakajitosa mtoni Yordani, wakaogelea mpaka ng'ambo ya pili wapate kutoroka. Lakini watu wa Bakide hawakuvuka mto na kuwafuatia.
49 Siku hiyo Bakide alipoteza watu wake 1,000 hivi.
50 Baada ya kurejea Yerusalemu, Bakide akajenga maboma yenye kuta ndefu na milango imara katika miji ya Yudea: Emau, Beth-horoni, Betheli, Timnathi, Farathoni, Tefoni; na ngome ya Yeriko.
51 Katika miji hiyo yote Bakide aliweka vikosi vya askari kwa ajili ya kuwanyanyasa Wayahudi.
52 Pia akaimarisha maboma ya miji ya Beth-zuri na Gazara, na ngome ya Yerusalemu. Aliweka humo vikosi vya jeshi na akiba ya chakula.
53 Kisha akawakamata wana wa watu maarufu nchini na kuwafanya mateka, akawafungia katika ngome ya Yerusalemu.
54 Mwezi wa pili wa mwaka 153, kuhani mkuu, Alkimo, aliamuru ukuta wa ua wa ndani wa hekalu ubomolewe. Kufanya hivyo ingekuwa sawa na kuharibu kile walichokuwa wamekamilisha manabii; lakini walipoanza tu kubomoa ukuta,
55 Alkimo alipata pigo, na kazi ikakoma. Alikuwa amepooza, hawezi kufungua mdomo wala kusema wala kutoa wosia kwa familia yake.
56 Kwa mateso makali alikata roho.
57 Bakide alipopata taarifa ya kifo hicho, alirejea kwa mfalme Demetrio, na nchi ya Yudea ikawa na amani kwa miaka miwili.
58 Kisha waasi wote wakakusanyika na kusema: “Tazameni, Yonathani na watu wake wanakaa kwa amani na usalama. Tukimleta Bakide hapa sasa, anaweza kuwakamata hao wote kwa usiku mmoja.”
59 Basi, wakaenda kujadili suala hilo na Bakide.
60 Bakide akaondoka na jeshi kubwa akapeleka barua za siri kwa rafiki zake wote waliokuwa Yudea, akiwaomba wamkamate Yonathani na watu wake. Lakini hawakufanikiwa kutekeleza hilo kwa sababu mpango wao uligunduliwa kabla.
61 Yonathani na watu wake wakawakamata viongozi 50 wa wahaini hao, wakawaua.
62 Halafu Yonathani, Simoni na wanajeshi wao wakaondoka na kwenda Beth-basi nyikani. Huko wakafufua magofu ya maboma na kuimarisha ulinzi wa mji wa Beth-basi.
63 Bakide alipopata habari ya hayo yote, alikusanya jeshi lake lote na kuwaweka tayari wote waliomwunga mkono nchini Yudea.
64 Halafu akaenda na kuushambulia mji wa Beth-basi kutoka pande zote, akajenga na mitambo ya vita. Mapambano yalipokuwa yameendelea kwa siku nyingi,
65 Yonathani akamwacha nduguye, Simoni humo mjini, akaenda sehemu za mashambani nchini na kikosi kidogo cha watu.
66 Huko, Yonathani akamshinda Odomera na watu wake, halafu akawashambulia jamaa ya Fasironi katika mahema yao. Hao walioshindwa wakajiunga naye wakaanza mashambulizi.
67 Wakati huo huo, Simoni na watu wake walikimbia kutoka mji wa Beth-basi, wakaichoma moto ile mitambo ya vita.
68 Katika mapambano hayo Bakide alikabwa vibaya hivi hata mipango yake yote ikaenda kombo; akashindwa vitani.
69 Hivi akawakasirikia sana wale Wayahudi waasi waliomshauri na kumhimiza aende Yudea; akawaua wengi wao. Kisha, Bakide akaamua kurejea nchini kwake.
70 Lakini Yonathani alipopata habari hiyo, akatuma wajumbe kwa Bakide kufanya mipango ya masharti ya amani na kurejeshwa kwa wafungwa wa Kiyahudi.
71 Bakide akakubali kufanya kama Yonathani alivyoomba, akaahidi kwa kiapo kwamba hatamdhuru maisha yake yote.
72 Bakide akamrudishia Yonathani wafungwa aliokuwa amewakamata kabla yake nchini Yudea. Halafu akaondoka kurejea nchini kwake, asije tena katika nchi ya Wayahudi.
73 Hivyo, vita vikakoma katika Israeli. Yonathani akafanya makao yake Mikmashi, akaanza kuwatawala Waisraeli, na kuwafutilia mbali nchini wahaini wote.

Generic placeholder image