15

Antioko wa Saba aomba msaada kwa Simoni
1 Kutoka visiwani baharini, Antioko mwana wa mfalme Demetrio, aliandika barua ifuatayo kwa Simoni, kuhani mkuu na kiongozi wa Wayahudi, na kwa taifa zima:
2 “Mfalme Antioko kwa Simoni, kuhani mkuu na mtawala, na kwa taifa la Wayahudi: Salamu!
3 Kama mnavyojua, ufalme wa wazee wangu umevamiwa na kushikwa na wahaini. Nimeamua kuurudisha na kuupatia hadhi yake ya awali. Nimekusanya jeshi kubwa la askari wa kukodiwa, na nimeandaa meli za vita.
4 Lengo langu ni kuivamia nchi na kuwashambulia wale walioiharibu nchi yetu na kuiteka miji mingi.
5 “Basi, sasa ninawathibitishieni misamaha yote ya kodi na malipo mliyopewa na wafalme waliotangulia.
6 Ninawapeni idhini ya kutengeneza fedha yenu wenyewe itakayotumika kihalali nchini mwenu.
7 Hapana kodi itakayodaiwa kwa mji wa Yerusalemu na hekalu. Silaha zote mlizotengeneza, na ngome mlizojenga na mnazozimiliki sasa, vitabaki mali yenu.
8 Zaidi ya hayo, madeni yote mnayodaiwa na hazina ya mfalme, au yale ambayo mngedaiwa siku za mbele, yanafutwa moja kwa moja.
9 Mara nitakapokuwa nimeushika tena ufalme wangu, nitakupa wewe, taifa lako, na hekalu heshima kubwa hivi hata utukufu wa nchi yenu ujulikane duniani kote.”
10 Mwaka 174, Antioko aliivamia nchi ya wazee wake. Karibu askari wote walijumuika na kujiunga naye; wachache sana wakabaki upande wa Trifo. 11Trifo, akiandamwa na Antioko, akakimbilia Dori, mji ulioko pwani.
12 Alijua kwamba mambo yalikuwa yamemchachia, kwa vile askari wake wote walikuwa wamemwacha.
13 Antioko akauzingira mji wa Dori na askari waliochaguliwa 120,000, na wapandafarasi 8,000.
14 Baharini alikuwa na meli zilizoshambulia pia. Hivi, mji ulikuwa umezingirwa pande zote na kusongwa hivi hata haikuwezekana mtu yeyote kuingia au kutoka mjini.

Roma yawasaidia Wayahudi
15 Wakati huo huo, Numenio na wenzake waliwasili Yerusalemu kutoka Roma, wamechukua barua ifuatayo, iliyoandikwa kwa wafalme na nchi mbalimbali:
16 “Kutoka kwa Lukio, balozi wa Waroma, kwa mfalme Tolemai: Salamu!
17 Wajumbe kutoka kwa rafiki zetu na washirika, Wayahudi, wamekuja kwetu kufanya upya mkataba wa awali wa urafiki na ushirikiano. Hao walitumwa na kuhani mkuu Simoni na taifa la Wayahudi,
18 na wameleta zawadi ya ngao ya dhahabu yenye uzito wa kilo 500.
19 Hivi tumeamua kuandika kwa wafalme na nchi mbalimbali kuwasihi wasifanye madhara ya aina yoyote kwa Wayahudi, miji yao au nchi yao; wasiwapige vita Wayahudi au kuwasaidia maadui wanaowashambulia Wayahudi.
20 Tumeamua kuipokea ngao waliyoleta na kuwalinda.
21 Kwa hiyo, kama waasi wowote watatokea Yudea na kukimbilia nchini mwako, warudishe kwa Simoni, kuhani mkuu, naye atawaadhibu kulingana na sheria ya Kiyahudi.”
22 Lukio aliandika barua kama hiyo kwa mfalme Demetrio, kwa Atalo, Ariarathe na Arsake,
23 na kwa nchi zifuatazo: Sampsame, Sparta, Delo, Mindo, Sikyoni, Karia, Samo, Pamfulia, Likia, Halikarnaso, Rode, Faseli, Kosi, Side, Arado, Gortina, Nido, Kupro na Kurene.
24 Nakala ya barua hiyo pia ilipelekwa kwa Simoni, kuhani Mmkuu.

Antioko wa Saba afarakana na Simoni
25 Mfalme Antioko, kwa mara ya pili, aliuzingira mji wa Dori, akawa anaushambulia tena na tena. Alitengeneza mitambo ya vita; akamzuia Trifo na watu wake kuingia au kutoka mjini.
26 Simoni akapeleka askari waliochaguliwa 2,000 kumsaidia Antioko, hali kadhalika fedha na dhahabu na zana nyingi.
27 Lakini Antioko akakataa kupokea misaada hiyo, akafutilia mbali makubaliano yote ya nyuma aliyokuwa amefanya na Simoni, akawa adui yake.
28 Halafu Antioko akamtuma Athenobio, ofisa wake wa kuaminika, kwenda kuafikiana na Simoni. Athenobio akamwambia Simoni: “Nyinyi mnaishika Yopa, Gazara, na ngome ya Yerusalemu, miji ambayo ni ya ufalme wangu.
29 Mmezikumba sehemu hizo na kusababisha matatizo mengi nchini. Mmeshika mahali pengi katika ufalme wangu.
30 Sasa mtarudisha ile miji mliyoiteka, na mtanipa fedha yote ya kodi mliyokusanya kutoka sehemu mlizozikalia nje ya nchi ya Yudea.
31 Kama hamtaki kufanya hivyo, basi, mtanilipa fedha kilo 17,000, na nyingine tena kilo 17,000 kufidia hasara nilizopata na kodi nilizopoteza. Kama hamtaki kutekeleza hata hilo, basi mtakuwa mmejitangazia vita.”
32 Athenobio alipowasili Yerusalemu na kuona fahari na utukufu wa Simoni, vyombo vya dhahabu na fedha katika ukumbi wa karamu na mengine ya fahari na utajiri, alibaki mdomo wazi kwa mshangao. Halafu akampatia Simoni ujumbe wa mfalme.
33 Simoni akajibu: “Kamwe hatujajinyakulia ardhi kutoka taifa lingine lolote lile, na wala hatujanyang'anya kitu chochote cha taifa lolote lile. Bali, kinyume chake, tumejirudishia tu mali ambayo tulirithi kutoka kwa wazee wetu, nchi ambayo maadui zetu walikuwa wametunyang'anya bila haki siku za nyuma.
34 Sasa hivi sisi tunatumia nafasi hiyo kuupata tena urithi wa wazee wetu.
35 Na kuhusu Yopa na Gazara, miji mnayodai ni yenu, tutawapeni fedha kilo 3,400, ingawa wakazi wa miji hiyo wameleta madhara makubwa kwa taifa letu.” Athenobio hakujibu neno,
36 bali akarudi kwa mfalme amejaa hasira. Alipomweleza mfalme kauli ya Simoni, na kumsimulia juu ya fahari na utukufu wa Simoni na yote aliyokuwa ameona, mfalme akaghadhibika sana.

Ushindi wa Yohane dhidi ya Kendebeo
37 Wakati huo huo, Trifo alikuwa amepanda meli na kutorokea mjini Orthosia.
38 Mfalme Antioko akamteua Kendebeo awe kamanda wa sehemu za mwambao, akampatia askari wa miguu na wapandafarasi,
39 na kumpa amri apige kambi dhidi ya Yudea. Pia alimwamuru aujenge upya mji wa Kedroni na kuimarisha milango yake, ili aweze kupambana na taifa la Wayahudi. Mfalme mwenyewe akaendelea kumfuatilia Trifo.
40 Kendebeo akafika Yamnia na kuanza kuwanyanyasa Wayahudi kwa kuivamia Yudea, kuwateka watu na kuwaulia mbali.
41 Aliujenga upya mji wa Kedroni na kuviweka hapo vikosi kadha vya askari wa miguu na wapandafarasi, ili waweze kufanya mashambulio na kuzilinda barabara za Yudea, kama mfalme alivyokuwa ameagiza.

Generic placeholder image