11

Kuanguka kwa Aleksanda Epifane
1 Mfalme Tolemai wa Sita wa Misri alikusanya jeshi la askari wengi zaidi kuliko mchanga wa pwani, akaandaa na meli nyingi. Lengo lake lilikuwa kumnasa Aleksanda, kutwaa ufalme wake na kuuongeza kwenye milki yake mwenyewe.
2 Hivi akaenda Siria, akiwaahidia watu amani. Raia wa huko wakamfungulia milango na kumkaribisha. Mfalme Aleksanda alikuwa amewaamuru wafanye hivyo kwa sababu Tolemai alikuwa mkwewe.
3 Lakini Tolemai alipoelekea kaskazini, alipita na kuacha kikosi cha askari katika kila mji.
4 Alipowasili Ashdodi, watu wakamwonesha magofu ya hekalu la Dagoni lililounguzwa moto, na uharibifu wote uliofanyika katika mji wa Ashdodi na viunga vyake. Maiti zilikuwa zimetapakaa kila mahali. Maiti za wale waliochomwa moto na Yonathani zilikuwa zimerundikwa kandokando ya barabara aliyopita Tolemai.
5 Watu walimweleza maovu aliyokuwa ametenda Yonathani, wakitumaini kwamba atatiwa hatiani; lakini Tolemai hakusema lolote.
6 Yonathani, kwa fahari, akaenda Yopa kuonana na Tolemai. Waliamkiana na kulala huko.
7 Yonathani alimsindikiza Tolemai hadi mto Eleuthero, halafu akarejea Yerusalemu.
8 Kwa njia hiyo mfalme Tolemai, katika hila zake dhidi ya Aleksanda, alijitwalia miji yote ya pwani hadi bandari ya Seleukia.
9 Kutoka huko, Tolemai alimpelekea mfalme Demetrio ujumbe huu: “Hebu tufanye mapatano. Sasa hivi binti yangu ni mke wa Aleksanda. Lakini mimi nitamchukua tena huyo binti na kumwoza kwako na kukufanya utawale ufalme wa baba yako.
10 Najilaumu kwa nini nilimpa Aleksanda binti yangu, kwa sababu ametafuta mbinu za kuniua.”
11 Tolemai alimlaumu hivyo Aleksanda kwa kuwa alitaka kumpokonya ufalme wake.
12 Basi, akamnyang'anya binti yake na kumwoza Demetrio; akavunja uhusiano wote na Aleksanda, na uadui wao ukaonekana wazi.
13 Tolemai akaingia Antiokia na kujichukulia utawala wa Asia; hivi alikuwa mtawala wa Misri na Asia.
14 Wakati huo mfalme Aleksanda alikuwa Kilikia, kwa vile watu wa mkoa huo walikuwa wakifanya ghasia.
15 Lakini aliposikia juu ya uvamizi wa Tolemai, aliondoka mara na kumshambulia Tolemai. Tolemai, akiwa na jeshi kubwa, alirudisha mashambulio na kumshinda kabisa Aleksanda.
16 Aleksanda akakimbilia Arabia apate kujificha,
17 lakini Mwarabu mmoja, Zabdieli, akamkata kichwa chake na kukipeleka kwa Tolemai.
18 Siku mbili baadaye Tolemai naye akafa, na askari wake aliokuwa amewaacha katika ngome mbalimbali wakauawa na wenyeji wa miji hiyo.
19 Hivi, mwaka 167, Demetrio wa Pili akawa mfalme.

Yonathani akubalika kwa Demetrio wa Pili
20 Siku hizohizo, Yonathani aliwakusanya watu wa Yudea ili kuishambulia ngome ya Yerusalemu. Waliunda mitambo mingi ya vita kwa ajili hiyo.
21 Lakini Wayahudi fulani wasaliti, waliolichukia taifa lao wenyewe, wakaenda kwa mfalme Demetrio wa Pili na kumwambia kwamba Yonathani alikuwa anaizingira ngome ya Yerusalemu.
22 Demetrio aliposikia hayo alikasirika, akahamishia makao yake Tolemai. Halafu akamwandikia Yonathani na kumwamuru aache kuizingira ngome, na aende, bila kukawia, kuonana naye Tolemai.
23 Yonathani alipopata ujumbe huo, akawaamuru watu wake waendelee kuizingira ngome. Halafu akawachagua baadhi ya viongozi na makuhani wa Kiyahudi wamsindikize. Bila kujali maisha yake
24 alikwenda Tolemai kwa mfalme, akiwa amemchukulia mavazi, fedha na dhahabu, na zawadi nyingine nyingi. Mfalme alipendezwa sana naye.
25 Ingawa wahaini fulani wa taifa lake walikuwa wamemlaumu na kumshtaki Yonathani,
26 mfalme alimtendea Yonathani kama vile wafalme waliomtangulia walivyokuwa wamemtendea. Akampa heshima mbele ya washauri wake wote,
27 na akamthibitisha katika wadhifa wake wa kuhani mkuu. Alimrudishia madaraka yake yote ya awali, akampandisha juu kabisa katika orodha ya “Rafiki ya Mfalme”.
28 Ndipo Yonathani akamwomba mfalme afute kodi kwa nchi ya Yudea na ile mikoa mitatu ya Samaria, akiahidi kumlipa kwa mkumbo mmoja fedha kiasi cha kilo 10,000, kama angefuta hiyo kodi.
29 Mfalme akakubali, na akaandika barua ifuatayo kwa Yonathani kuthibitisha hayo yote:
30 “Mfalme Demetrio, kwa nduguye Yonathani ndugu yake na taifa la Wayahudi: Salamu!
31 “Hapa naambatisha, kwa taarifa yako, nakala ya barua niliyomwandikia ndugu Lasthene juu yako.
32 “‘Mfalme Demetrio kwa Mheshimiwa Ndugu Lasthene: Salamu!
33 Nimeamua kulipatia taifa la Wayahudi maslahi fulani kwa sababu ni rafiki zetu waaminifu na wanashika masharti ya mkataba wao.
34 Ninathibitisha kwamba taifa la Wayahudi lina haki juu ya nchi ya Yudea na ile mikoa mitatu ya Afairema, Luda na Rathamini, ambayo sasa inahamishiwa Yudea kutoka Samaria, pamoja na ardhi yote inayoihusu mikoa hiyo. Wote watakaotoa tambiko Yerusalemu hawatawajibika kulipa kodi kwa mfalme, ambayo hapo awali mfalme aliwadai kila mwaka, kutoka mavuno ya nafaka na matunda; kodi hiyo sasa itakuwa kwa manufaa ya hekalu.
35 Pia ninawaondolea malipo yote ninayowadai kutokana na zaka, ushuru, kodi ya machimbo ya chumvi, na kodi nyingine maalumu.
36 Vipengee vyote vya barua hii vitabaki hivyo bila kubatilishwa hata milele.
37 “‘Basi, angalia kwamba barua hii inanakiliwa kwa uaminifu, na nakala hiyo anapewa Yonathani, ili iwekwe mahali pa kufaa katika mlima wa hekalu, itakapoonekana wazi na watu wote.’”

Yonathani amsaidia Demetrio wa Pili
38 Mfalme Demetrio alipoona kwamba nchi imetulia chini ya utawala wake, na hakuna tena upinzani, akalivunja jeshi lake na kuwarudisha nyumbani askari wote - isipokuwa wale aliokuwa amewakodi kutoka visiwa vya Ugiriki. Kitendo hicho kiliwaudhi askari wote waliokuwa wameajiriwa na wafalme waliomtangulia Demetrio, kwa vile sasa walikuwa hawana mshahara; wakamchukia mfalme.
39 Trifo, ambaye kwanza alikuwa upande wa Aleksanda, alipoona askari wote wananung'unika juu ya Demetrio, akamwendea Imalkue, Mwarabu aliyekuwa anamlea na kumtunza Antioko, mwana wa Aleksanda.
40 Trifo akakaa huko kwa muda mrefu, akimbembeleza Imalkue amwachie yeye huyo mtoto mdogo wa Aleksanda, ili amfanye mfalme badala ya baba yake. Pia alimsimulia Imalkue kuhusu matendo ya Demetrio, na jinsi askari walivyomchukia.
41 Wakati huo huo, Yonathani akampelekea ujumbe mfalme Demetrio, akimwomba aondoe askari wake katika ngome ya Yerusalemu na maboma mengine ya Yudea, kwa vile walikuwa wanawanyanyasa Wayahudi.
42 Demetrio akajibu: “Nitatekeleza ombi lako, na wasaa utakaporuhusu, nitakutunukia wewe na taifa lako heshima za hali ya juu kabisa.
43 Lakini sasa uniletee msaada wa askari watakaonipigania, maana askari wangu wote wameniasi.”
44 Basi, Yonathani akawapeleka Antiokia askari hodari 3,000. Mfalme alifurahi sana walipowasili,
45 kwa sababu genge la watu 120,000 lilikuwa limekusanyika mjini, limepania kumwua mfalme.
46 Lakini mfalme akatorokea ikulu, wakati watu wanaishika mitaa ya mji na kuanza ghasia.
47 Hapo mfalme akaita askari wa Kiyahudi wamsaidie, nao wote wakaitika mara, wakaenda huko na huko mjini na kuwaua watu wapatao laki moja.
48 Waliokoa maisha ya mfalme, lakini mji waliupora na kuuchoma moto.
49 Watu walipoona kwamba Wayahudi wameukamata mji wao kabisa, walivunjika moyo, wakamsihi mfalme, wakiomba:
50 “Tupe amani, na ukomeshe hayo mashambulio ya Wayahudi dhidi yetu na mji wetu.”
51 Hao waasi wakaweka silaha chini na kupandisha mikono juu. Mfalme na raia wake wote wakawa na heshima kubwa kwa Wayahudi. Nao Wayahudi wakarejea Yerusalemu na shehena ya mateka.
52 Lakini mfalme Demetrio alipoimarika tena katika utawala wake, na nchi yote kuwa na amani,
53 akakiuka ahadi zake zote na kuvunja uhusiano na Yonathani; badala ya kumlipa mema kama ilivyotazamiwa, yeye alimkandamiza vibaya sana.

Yonathani amwunga mkono Antioko wa Sita
54 Kitambo baadaye, Trifo alirejea pamoja na yule mvulana Antioko, akamtia taji na kumtawaza kuwa mfalme.
55 Wale askari wote walioachishwa kazi na Demetrio wakamwunga mkono mfalme mpya. Wakampiga na kumshinda Demetrio, naye akakimbia.
56 Trifo akawateka tembo wa vita na kuushika mji wa Antiokia.
57 Mfalme chipukizi, Antioko, akamwandikia Yonathani na kumthibitisha katika cheo chake cha kuhani mkuu, na cha mkuu wa mikoa ile minne, akamteua awe “Rafiki wa Mfalme”.
58 Akampelekea vyombo vya dhahabu na vya kutumia mezani, akampa idhini ya kunywea vikombe vya dhahabu, kuvaa mavazi ya kifalme, na kuvaa bizimu ya dhahabu.
59 Pia alimteua ndugu ya Yonathani, Simoni, kuwa mkuu wa eneo lote kutoka mlima Ngazi ya Tirza hadi mipaka ya Misri.
60 Kisha, Yonathani akapita na jeshi lake katika miji ya Siria Kuu; majeshi yote ya Siria yakajumuika naye katika ushirika. Alipofika Askaloni, wenyeji wa mji huo walimlaki na kumpatia heshima.
61 Halafu akaenda Gaza, lakini wakazi wake wakafunga milango ya mji na kumzuia. Basi, Yonathani akauzingira mji huo, akauchoma moto na kuviteka viunga vyake.
62 Ndipo watu wa Gaza wakamtaka amani, naye akafanya mpango wa amani. Akawachukua wana wa viongozi na kuwapeleka Yerusalemu wawe mateka. Baada ya hayo, akaenda zake Damasko.
63 Yonathani akasikia kwamba maofisa wa Demetrio walikuwa wamefika Kadeshi, Galilaya, na jeshi kubwa, wakinuia kumwondoa Yonathani madarakani.
64 Basi, akamwacha nduguye Simoni, nchini Yudea, akaondoka kwenda kupambana na jeshi la Demetrio.
65 Simoni akauzingira mji wa Beth-zuri na kuupiga vita kwa muda mrefu.
66 Kisha wenyeji wake wakaomba masharti ya amani, naye Simoni akakubali. Basi, akauteka mji huo, akawafukuzia nje wakazi wake, akaweka humo kikosi cha askari.
67 Yonathani na jeshi lake wakapiga kambi kando ya Ziwa Genesareti. Mapema asubuhi iliyofuata aliwaongoza wanajeshi wake kwenye tambarare ya Hazori,
68 ambako sehemu kubwa ya jeshi la kigeni ilikuwa inasonga mbele kumkabili. Kumbe maadui walikuwa wameacha kikosi cha askari kikivizia milimani, lakini wakakutana naye ana kwa ana.
69 Hao askari waliojificha wakatokeza na kuanza kushambulia.
70 Jeshi lote la Yonathani likageuka na kukimbia. Hapana aliyebaki, isipokuwa maofisa wawili: Matathia mwana wa Absalomu, na Yuda mwana wa Kalfi, makamanda wa jeshi.
71 Yonathani alirarua mavazi yake kwa uchungu, akajitia mavumbi kichwani, akasali.
72 Kisha akarudi kwenye mapambano, akawapiga maadui, na kuwafanya wakimbie.
73 Askari wake waliokuwa wanakimbia walipoona hayo, walirudi na kujiunga naye katika kuwafuatia maadui. Waliwafukuza adui moja kwa moja hadi kambini kwao Kadeshi, halafu wakaiteka hiyo kambi.
74 Askari wa adui wasiopungua 3,000 waliuawa siku hiyo. Yonathani akarejea Yerusalemu.

Generic placeholder image