5

Vita na mataifa jirani
(2Mak 10:14-33; 12:10-45)
1 Mataifa jirani yaliposikia kwamba Wayahudi walikuwa wamejenga upya madhabahu na hekalu limewekwa wakfu kama kwanza yaliwaka hasira,
2 yakaamua kuwaangamiza wazawa wa Yakobo waliokuwa wanaishi miongoni mwao. Hivi wakaanza kufanya mauaji na uharibifu miongoni mwa watu.
3 Kule Akrabatene, Idumea, wana wa Esau walikuwa wanawavizia Waisraeli. Yuda akawapiga vita na kuwaangamiza kabisa, akawanyenyekesha na kupora mali zao.
4 Pia hakusahau wana wa Baeani ambao walikuwa tishio na mtego kwa watu wa Israeli, kwa vile walikuwa wakijificha njiani na kuwashambulia Waisraeli.
5 Yuda akawafungia Wabaeani katika ngome zao, akaweka nadhiri ya kuwaangamiza, akazichoma moto ngome hizo na kuwaunguza wote waliokuwa ngomeni.
6 Halafu akavuka kuwaendea Waamoni. Akakuta jeshi kubwa na lenye nguvu, likiongozwa na Timotheo.
7 Yuda akapambana na jeshi hilo katika mapigano mengi; hatimaye akalishinda nguvu.
8 Akauteka Yazeri na vijiji vyake, kisha akarejea nchini Yudea.
9 Watu wa mataifa huko Gileadi walikusanyika ili kuwashambulia na kuwaangamiza Waisraeli waliokuwa wanakaa nchini mwao. Lakini Waisraeli wakakimbilia kwenye ngome ya Dathema,
10 na kumwandikia Yuda na nduguze barua iliyosema: “Jirani zetu, watu wa mataifa mengine, wamekusanyika ili kutuangamiza.
11 Wanajiandaa kuja kuiteka ngome ambamo tumekimbilia, naye Timotheo anaongoza majeshi yao.
12 Basi, fanya haraka, uje utuokoe, maana wengi wetu wamekwisha uawa.
13 Na ndugu zetu wote waliokuwa katika nchi ya Tobu wameuawa; maadui wamechukua mateka wake zao, watoto wao, na mali yao, na kuwaangamiza watu wapatao 1,000.”
14 Barua hiyo ilipokuwa bado inasomwa, wajumbe wengine, waliokuwa wamerarua mavazi yao kwa uchungu, waliwasili na taarifa kama hiyo kutoka Galilaya.
15 Wakasema: “Jeshi kutoka Tolemai, Tirza, Sidoni, na mkoa mzima wa Galilaya, limekusanyika kutuangamiza.”
16 Yuda na watu wake waliposikia hayo yote, wakaita mkutano mkubwa kuamua jinsi ya kuwasaidia wananchi wenzao waliokuwa wanasumbuka na kushambuliwa na maadui.
17 Yuda akamwambia nduguye Simoni: “Chagua baadhi ya watu wako, nenda ukawaokoe Wayahudi wenzetu huko Galilaya; mimi na ndugu yetu Yonathani tutakwenda Gileadi.”
18 Yuda akaviacha vikosi vingine vya jeshi lake viilinde Yudea, chini ya uangalizi wa Yosefu mwana wa Zekaria, na Azaria, kiongozi wa watu.
19 Akawaambia hao wawili: “Waangalieni watu hawa, lakini msijitie katika mapambano na watu wa mataifa mengine mpaka sisi tutakaporudi.”
20 Ndipo Simoni akatwaa watu 3,000 na kwenda nao Galilaya, na Yuda akaenda zake Gileadi na watu 8,000.
21 Simoni akaenda Galilaya, akapigana vita vingi na watu wa mataifa mengine. Akawashinda
22 na kuwafuatia mpaka mji wa Tolemai. Aliwaua watu wapatao 3,000, akapora na mali zao.
23 Halafu akawachukua Wayahudi waliokuwa Galilaya na Arbata, pamoja na wake zao, watoto wao na mali zao zote, akarudi nao Yudea kwa shangwe kubwa.
24 Wakati huo, Yuda Makabayo na nduguye Yonathani walikuwa wamevuka mto Yordani na kusafiri jangwani siku tatu.
25 Walikutana na baadhi ya Wanabatea ambao waliwakaribisha kwa amani na kuwaeleza yote yaliyokuwa yamewapata Wayahudi wenzao kule Gileadi.
26 Wanabatea hao walieleza kwamba Wayahudi wengi walikuwa wamefungwa katika miji yenye ngome, miji ya Bozra, Bosori, Alema, Chasfo, Makedi na Karnaimu; miji mikubwa na midogo;
27 wengine wamefungwa katika miji midogomidogo ya Gileadi. Pia walitoa taarifa kwamba maadui walikuwa wamejitayarisha kuzishambulia ngome wapate kuteka na kuwaangamiza Wayahudi wote kwa siku moja.
28 Basi, Yuda na jeshi lake wakageuka mara na kupita njia ya jangwani. Wakaushambulia na kuuteka mji wa Bozra, na kuwaua watu wote mjini humo, wakateka nyara na kuuchoma moto mji huo.
29 Kisha wakaondoka, wakasafiri usiku kucha hadi kwenye ngome ya mji wa Dathema.
30 Alfajiri, Yuda na watu wake wakaona jeshi kubwa la watu wasiohesabika, wamebeba ngazi na zana za vita, kuiteka hiyo ngome na kuwashambulia Wayahudi.
31 Yuda aliposikia vishindo na makelele na sauti za tarumbeta kutoka mjini, akatambua kwamba vita vilikuwa vimeanza.
32 Basi, akawaambia watu wake: “Pigeni vita leo kwa ajili ya Wayahudi wenzetu!”
33 Yuda akapanga watu katika vikosi vitatu, wasonge mbele kuelekea upande wa nyuma wa maadui; walipiga tarumbeta na kusali kwa sauti kubwa.
34 Jeshi lililokuwa chini ya Timotheo lilipoona kuwa linakabiliwa na Yuda Makabayo, likageuka na kuanza kukimbia. Yuda akalipiga barabara na kuwaua watu wapatao 8,000 siku hiyo.
35 Halafu Yuda akaugeukia mji wa Alema, akaushambulia na kuwaua wakazi wake wote, akateka nyara, na kuuchoma moto mji huo.
36 Kutoka hapo aliendelea mbele, akaiteka miji ya Chasfo, Makedi, Bosori, na mingineyo ya Gileadi.
37 Baada ya hayo, Timotheo akakusanya jeshi lingine, akapiga kambi mkabala na Rafoni, upande wa pili wa mto.
38 Yuda akatuma watu fulani kwenda kupeleleza kambi ya adui. Wapelelezi walirudisha taarifa kwake kwamba watu wote wa mataifa mengine katika eneo hilo walikuwa wamejiunga na Timotheo na kufanya jeshi kubwa.
39 Timotheo alikuwa pia amekodi askari wa Kiarabu wamsaidie; hao nao walikuwa kambini, upande wa pili wa mto, tayari kumshambulia Yuda. Basi, Yuda akaenda kupambana nao.
40 Yuda na jeshi lake walipokaribia kufika mtoni, Timotheo akawaambia maofisa wake: “Kama akivuka mto kwanza, hatutaweza kurudisha mashambulio yake, naye atatushinda.
41 Lakini kama ataogopa na kusimama upande mwingine wa mto, sisi tutavuka na kumshambulia na kumshinda.”
42 Yuda alipoufikia ukingo wa mto, aliwaamuru maofisa wake: “Msimruhusu yeyote yule kusimama; wote waingie vitani!”
43 Halafu yeye mwenyewe akawa wa kwanza kuvuka mto, na watu wake wote wakamfuata. Maadui wakapigwa vibaya, wakatupa silaha zao na kukimbilia kwenye hekalu lililokuwa mjini Karnaimu.
44 Lakini Yuda na watu wake wakauteka mji huo, wakalichoma moto hekalu hilo na kuwaunguza wote waliokuwa humo ndani. Basi, Karnaimu ulichukuliwa, na watu hao hawakuweza tena kumzuia Yuda.
45 Kisha, Yuda akawakusanya Wayahudi wote waliokuwa Gileadi, tangu watoto hata wazee, wanawake na watoto wao pamoja na mali yao; likawa kundi kubwa sana la watu wanarudi nchini Yudea.
46 Basi, wakaenda hadi Efroni. Huo ulikuwa mji mkubwa na imara sana, umejengwa njiani. Hawakuweza kuuzunguka, wala kulia wala kushoto; ikawabidi kupita katikati ya mji.
47 Lakini wakazi wa Efroni wakawafungia nje Wayahudi na kuziba milango ya mji kwa mawe.
48 Yuda akawapelekea ujumbe huu wa kirafiki: “Tuacheni tupite katika nchi yenu ili turudi kwetu. Hapana atakayewadhuru nyinyi. Sisi tutapita tu na kwenda zetu.” Lakini wao wakakataa kufungua milango.
49 Basi, Yuda akawaambia wote waliofuatana na jeshi lake wasimame walipo.
50 Halafu akawaamuru askari wake kujiandaa kwa mapambano dhidi ya mji wa Efroni. Pakawa na mapigano mchana kutwa na usiku kucha, mpaka mji ulipotekwa na Wayahudi.
51 Yuda akawaua kwa upanga wanaume wote wa Efroni, akaubomoa mji na kuteka nyara. Halafu yeye na jeshi lake wakapita katikati ya magofu ya mji huo, wakitembea juu ya maiti.
52 Walivuka mto Yordani na kuifikia tambarare pana mbele ya Beth-sheani.
53 Njiani kote Yuda alikuwa akiwakusanya waliolegalega nyuma na kuwatia moyo watu wake mpaka walipowasili Yudea.
54 Kwa shukrani na shangwe, walipanda mlimani Siyoni, wakatolea sadaka za kuteketezwa, kwa sababu walikuwa wamerudi salama bila ya kumpoteza hata mmoja wao.
55 Yuda na Yonathani walipokuwa Gileadi, na ndugu yao Simoni alipokuwa anaushambulia mji wa Tolemai katika Galilaya,
56 Yosefu na Azaria, makamanda wa jeshi lililobaki Yudea, walisikia habari za ujasiri na ushindi wao.
57 Wakaambiana: “Na tuanze vita na watu wa mataifa yanayotuzunguka, tujipatie sifa fulani na sisi.”
58 Hivi, wakatoa amri kwa watu wao, wakaushambulia mji wa Yamnia.
59 Gorgia na watu wake wakatoka nje ya mji ili kupambana na Wayahudi hao.
60 Watu wa Gorgia wakawashinda Yosefu na Azaria, na kuwafuatia hadi mipakani mwa Yudea. Siku hiyo waliuawa Waisraeli wasiopungua 2,000.
61 Hasara hiyo kubwa iliwapata kwa sababu Yosefu na Azaria walitafuta sifa, wakawakaidi Yuda na nduguze.
62 Zaidi ya hayo, hao hawakuwa wa ukoo wa Makabayo ambao Mungu alikuwa amewachagua kuleta uhuru kwa watu wa Israeli.
63 Yuda Makabayo na nduguze waliheshimiwa sana miongoni mwa Waisraeli na watu wote wa mataifa mengine. Watu waliposikia sifa zao,
64 walikusanyika makundi kwa makundi kuwapa hongera.
65 Kisha, Yuda, pamoja na ndugu zake, akaenda kusini kuwapiga vita wana wa Esau. Aliishambulia Hebroni na miji iliyoizunguka, akaziharibu ngome zake na kuunguza minara yake yote.
66 Halafu akaingia katika nchi ya Wafilisti, akipitia Marisa.
67 Siku hiyo makuhani kadha waliuawa katika mapigano kwa sababu, kwa tamaa ya kupata sifa ya ushujaa, walianzisha mapambano.
68 Yuda akageuka na kwenda Ashdodi katika Filistia. Huko akabomoa madhabahu zao, akazichoma moto sanamu za miungu yao, akaiteka nyara miji yao, kisha akarejea nchini Yudea.

Generic placeholder image