8

Mkataba na Waroma
1 Yuda alikuwa amesikia sifa ya Waroma, kwamba walikuwa na nguvu sana kijeshi. Alijua kwamba waliwakaribisha wale wote waliojiunga nao kama washirika, na kwamba wale waliojumuika nao walikuwa na hakika ya kupokewa kirafiki na Roma.
2 Watu walikuwa wamemweleza Yuda juu ya vita vilivyopigwa na Waroma, na matendo ya kishujaa waliyowatenda Wagalatia, jinsi walivyowashinda na halafu kuwalazimisha kulipa kodi.
3 Alikuwa ameambiwa jinsi Waroma walivyofanya kule Hispania walipokamata machimbo ya fedha na dhahabu.
4 Kwa mipango yao na subira, walikuwa wameiteka nchi nzima ya Hispania, ingawa ilikuwa mbali na Roma. Pia walikuwa wamewashinda wafalme waliowajia kwa vita kutoka nchi za mbali, wakawaponda na kuwapiga vibaya hivi hata wale walionusurika kuuawa ikawapasa kulipa kodi kwa Waroma kila mwaka.
5 Walikuwa wamepiga vita na kuwashinda Filipo, na Perseo, mfalme wa Makedonia, na wote waliojiunga nao dhidi ya Roma.
6 Walikuwa wamemshinda hata Antioko Mkuu, mfalme wa Asia ambaye alikuwa amewashambulia Waroma kwa tembo 120, farasi, magari, na jeshi kubwa sana.
7 Walimkamata Antioko angali hai, wakamlazimisha yeye na wafalme waliomfuta kulipa kodi kubwa, kupeleka mateka kwao, na kutoa na kuwapa Waroma baadhi ya mikoa yao mizuri,
8 yaani, nchi ya India, Media na Lidia. Wakazichukua sehemu hizo na kumpa mfalme Eumene.
9 Wagiriki walipofanya mipango ya kuwashambulia na kuwaangamiza,
10 Waroma waliigundua mipango hiyo, wakampeleka jemadari mmoja kupambana nao. Waroma wakawaua Wagiriki wengi, wakawachukua utumwani wake zao na watoto wao, wakateka nyara, wakaitwaa nchi yao, wakabomoa na ngome zao, na wao wakawafanya watumwa - kama walivyo leo.
11 Pia waliwaangamiza au kuwafanya watumwa watu wa falme nyingine wa visiwani, na yeyote aliyekuwa amethubutu kupigana nao.
12 Lakini walidumisha urafiki wao na washirika wao na wale waliowategemea wao kiulinzi. Waliwapiga na kuwashinda wafalme wa karibu na wa mbali, na kila mtu aliyesikia sifa ya Waroma aliwaogopa.
13 Waliwasaidia watu wengine kuwa wafalme, lakini kwa upande mwingine, waliwaondolea mbali wafalme wengine. Ama hakika, Waroma walikuwa na nguvu kushinda mataifa yote duniani.
14 Hata hivyo, hapakuwa na Mroma yeyote aliyejaribu kuinua wadhifa wake binafsi kwa kujitia taji au kuvalia mavazi ya kifalme ya urujuani.
15 Ila waliunda baraza la wazee, na kila siku wazee wa baraza 320 walikutana ili kujadili mambo ya watu na ustawi wao.
16 Kila mwaka walimkabidhi mtu mmoja wajibu wa kuongoza nchi nzima. Kila raia alimtii kiongozi huyo, na hapakuwa na wivu au husuda miongoni mwao.
17 Basi, Yuda akawachagua Eupolemo mwana wa Yohane na mjukuu wa Akosi, na Yasoni mwana wa Eleazari, akawatuma Roma kufanya mkataba wa urafiki na ushirika na Waroma.
18 Alifanya hivyo ili kuondokana na ukoloni wa Wagiriki, kwa vile Wayahudi waliona wazi kwamba walikuwa wanafanywa watumwa.
19 Baada ya safari ndefu na ya taabu, Eupolemo na Yasoni waliwasili Roma, wakaingia kwenye baraza la wazee, na kusema hivi:
20 “Yuda Makabayo, ndugu zake, na taifa la Wayahudi wametutuma kwenu kufanya nanyi mkataba wa amani na ulinzi, ili tuweze kuandikwa rasmi kuwa marafiki na washirika wenu.”
21 Waroma walikubali ombi hilo,
22 na ifuatayo ni nakala ya barua iliyoandikwa juu ya vipande vya shaba, ikapelekwa Yerusalemu kuwekwa huko iwe kumbukumbu ya mkataba huo wa amani na ushirika:
23 “Ufanisi wa kudumu kwa Waroma na taifa la Wayahudi, barani na baharini! Upanga usiwaguse; adui asiwasogelee.
24 Ikiwa vita vitatangazwa kwanza dhidi ya Roma au dhidi ya mshirika wake yeyote yule na popote pale,
25 taifa la Wayahudi litatoa msaada wa hali na mali, kadiri itakavyohitajika.
26 Na hao maadui wafanyao vita, Wayahudi wasiwape wala kuwapatia chakula, silaha, au meli, kama ilivyokubaliwa Roma. Wayahudi watatimiza masharti hayo bila ya malipo.
27 “Vivyo hivyo, ikiwa vita vitatangazwa kwanza dhidi ya taifa la Wayahudi, Waroma watatoa msaada wa hali na mali, kadiri itakavyohitajika.
28 Na hao maadui wa Wayahudi hawatapewa wala kupatiwa chakula, silaha, fedha, au meli, kama ilivyokubaliwa Roma. Waroma watatimiza masharti hayo bila ya hila.
29 “Haya ndiyo masharti ya mkataba ambao Waroma wamefanya na taifa la Wayahudi.
30 Lakini kama, hapo baadaye, pande zote mbili zitakubaliana kuongeza au kuondoa kipengee chochote, zitaruhusiwa kufanya hivyo, na chochote zitakachoongeza au kuondoa kitakuwa halali.
31 “Zaidi ya hayo, kuhusu maovu ambayo mfalme Demetrio anawatenda Wayahudi, tumemwandikia Demetrio ifuatavyo: ‘Kwa nini umewakandamiza na kuwanyanyasa vibaya hivyo rafiki zetu na washirika wetu, Wayahudi?
32 Kama watakuja kwetu na kulalamika tena dhidi yenu, sisi tutawaunga mkono Wayahudi, tutapambana nanyi majini na katika nchi kavu.’”

Generic placeholder image