6

Kifo cha Antioko wa Nne
(2Mak 1:11-17; 9:1-29; 10:9-11)
1 Mfalme Antioko wa Nne alipokuwa anapita Mesopotamia mikoa ya nyanda za juu alisikia habari za mji Elimaisi katika nchi ya Persia, ambao ulisifika sana kwa utajiri wake wa fedha na dhahabu.
2 Hekalu lake lilikuwa na utajiri mwingi, limejaa ngao za dhahabu, deraya, na zana za vita zilizoachwa humo na Aleksanda, mwana wa mfalme Filipo wa Makedonia, aliyekuwa mtawala wa kwanza wa Wagiriki.
3 Antioko akafika Elimaisi, akajaribu kuutwaa na kuuteka nyara mji huo, lakini hakufanikiwa, kwa vile wakazi wake walikuwa wameigundua mipango yake,
4 wakakusanya majeshi yao kumpinga. Basi, Antioko akarudi Babuloni na moyo mzito.
5 Huko Persia Antioko akafikiwa na mjumbe aliyemwarifu kwamba majeshi aliyoyapeleka Yudea yalikuwa yameshindwa;
6 kwamba Lisia na jeshi lake lenye nguvu alikuwa amelazimika kuwakimbia Wayahudi; kwamba Wayahudi walikuwa wameimarika zaidi kutokana na silaha na zana za vita na nyara walizokuwa wameteka kutoka kwa majeshi ya maadui;
7 kwamba walikuwa wamebomolea mbali ile madhabahu ya mungu wa uongo aliyokuwa ameijenga Antioko juu ya madhabahu Yerusalemu; kwamba walikuwa wamelizungushia hekalu kuta ndefu kama ilivyokuwa kabla yake, na kwamba walikuwa wameuchukua na kuuhami mji wa Beth-zuri, mmoja wa miji ya mfalme Antioko.
8 Mfalme aliposikia habari hiyo, akashikwa na mshangao na fadhaa, akajitupa kitandani na kuugua, kwa sababu mambo yalikuwa yamekwenda kinyume cha matazamio yake.
9 Kwa muda mrefu alilala kwa ugonjwa huo, akizamishwa kitandani kwa mawimbi mazito ya huzuni, hata akatambua kwamba alikuwa anakufa.
10 Basi, akawaita rafiki zake wote, akawaambia: “Usingizi sipati, na moyo wangu umepondeka kwa huzuni na wasiwasi.
11 Kwanza nilijiuliza mwenyewe kwa nini yamenipata matatizo haya, ambapo katika utawala wangu nimekuwa mwema na ninayependwa na wote!
12 Halafu nikakumbuka maovu niliyofanya kule Yerusalemu nilipochukua kutoka hekaluni vyombo vyote vya fedha na dhahabu, nikajaribu, bila sababu ya maana, kuwaangamiza wakazi wa Yudea.
13 Najua hicho ndicho kisa cha mikasa hii iliyonipata, nami karibu ninakufa kwa kukata tamaa katika nchi hii ya kigeni.”
14 Kisha akamwita Filipo, mmoja wa washauri wake wakuu, akamkabidhi milki yake yote.
15 Akampa taji yake, vazi lake, na pete yake ya mhuri, akamwamuru amlee na kumwelimisha mwanawe, Antioko wa Tano, hata awe mfalme.
16 Mfalme Antioko akafariki dunia hapo, mwaka 149.
17 Lisia aliposikia kwamba mfalme amekufa, akamfanya kijana Antioko awe mfalme badala ya baba yake, na akampa jina Eupatori. Lisia alikuwa amemlea Antioko wa Tano tangu utoto.

Kampeni ya Antioko wa Tano na Lisia
(2Mak 13:1-22)
18 Wakati huo, maadui waliokuwa katika ngome ya Yerusalemu walikuwa wanawavizia watu wa Israeli katika eneo la kuzunguka hekalu. Walikuwa wanajaribu kwa namna nyingi kuwaumiza Wayahudi na hivyo kuwaimarisha watu wa mataifa.
19 Basi, Yuda akaamua kuwaangamiza, akawakusanya watu wake wote ili kuwazingira maadui.
20 Watu wakakusanyika wakaizingira ngome hiyo mnamo mwaka 150, na wakajenga minara na mitambo mingine ya kurushia silaha.
21 Lakini baadhi ya maadui waliozingirwa wakatoroka, na Wayahudi waovu kadha, wakajiunga nao.
22 Basi, wakaenda kwa mfalme, wakasema, “Hivi unangoja nini kulipa kisasi kwa maovu waliyofanyiwa wananchi wenzetu?
23 Sisi tulikubali kumtumikia baba yako, kushika amri zake, na kutii sheria zake.
24 Lakini tulipata faida gani? Sasa wananchi wenzetu wamekuwa maadui zetu. Kwa kweli, wamemuua kila mmoja wetu waliyemwona, na wametupora mali zetu.
25 Lakini hawajatudhuru sisi tu; wamewashambulia jirani zao wote.
26 Na sasa wameizingira ngome ya Yerusalemu, wanataka kuiteka. Tena wameliimarisha hekalu na kuuhami mji wa Beth-zuri.
27 Usipowazuia upesi, watafanya mengi zaidi, nawe hutaweza kuwazuia.”
28 Mfalme aliposikia hayo alikasirika sana. Akawakusanya makamanda wote wa jeshi, maofisa wote wa askari wapandafarasi, na washauri wake wakuu.
29 Hali kadhalika akakodi askari wa kulipwa kutoka nchi nyingine na visiwa vya Ugiriki.
30 Jeshi lake likawa na askari wa miguu laki moja, wapandafarasi 20,000, na tembo wa vita 32.
31 Basi, wakapita Idumea na kwenda kuuzingira mji wa Beth-zuri, ambako mapigano yalichukua muda mrefu. Jeshi la mfalme likajenga hapo mitambo ya kurushia silaha, lakini waliokuwa mjini walijitetea kwa ushujaa, wakatoka nje na kuichoma moto hiyo mitambo ya maadui.
32 Kisha Yuda akaondoa vikosi vyake kutoka katika ngome ya Yerusalemu, akapiga kambi Beth-zekaria, kukabiliana na kambi ya mfalme.
33 Mapema asubuhi iliyofuata, mfalme akapeleka jeshi lake kwa haraka katika barabara ya kwenda Beth-zekaria. Huko vikosi vyake vikajipanga, tayari kwa vita; wakapiga tarumbeta.
34 Wakawanywesha tembo wao maji ya rangi ya zabibu na forosadi ili kuwachochea kwa ajili ya vita.
35 Hao tembo wakawagawa kwa vikosi vya askari wa miguu: Kwa kila tembo mmoja askari wa miguu 1,000 deraya za chuma na kofia za shaba. Pia kwa kila tembo waliteuliwa askari wapandafarasi 500, ambao daima walifuatana na tembo wao.
36 Hao walimtangulia huyo tembo kokote alikokwenda, wala hawakumwacha.
37 Mgongoni pa kila tembo kilifungwa kwa ukanda maalumu kibanda imara cha miti. Mbali ya mwendeshaji, (Mhindi), kila tembo alipandwa na askari wanne wenye silaha.
38 Lisia akawapanga wapandafarasi waliobaki mbavuni mwa jeshi, upande huu na ule, ambapo waliweza kukingwa na askari wa miguu wakati wao wenyewe wanawashambulia maadui.
39 Jua liliziangaza ngao zao za dhahabu na shaba, milima ikarudisha mwanga wake ikimetameta kama mienge ya moto.
40 Sehemu ya jeshi la mfalme ilitawanywa kwenye vilima virefu, na nyingine kwenye tambarare, askari wakasonga mbele kwa taratibu na nidhamu.
41 Wote walitetemeka waliposikia mshindo wa miguu yao na mgongano wa silaha zao. Ama hakika, jeshi lao lilikuwa kubwa sana na lenye nguvu.
42 Lakini Yuda na jeshi lake wakajitia vitani, wakawaua wanajeshi 600 wa mfalme.
43 Eleazari Avarani aligundua kwamba tembo mmoja alikuwa mkubwa zaidi kuliko wengine, na kwamba alikuwa amevikwa deraya ya kifalme. Akadhani mfalme mwenyewe amempanda tembo huyo.
44 Hivi akajitoa mhanga kuwaokoa watu wake na kujipatia mwenyewe sifa ya kudumu milele.
45 Kwa ujasiri akamkimbilia huyo tembo, katikati ya kikosi cha askari wa miguu. Akasonga mbele kwa kasi, huku anapita akiua watu kulia na kushoto kwake, hata askari wa mfalme wakamwepa kila upande.
46 Akapenyeza chini ya tembo na kumchoma mkuki tumboni. Tembo akafa, akamwangukia Eleazari na kumwua.
47 Lakini Wayahudi walipoona nguvu ya jeshi la mfalme na ukali wa mashambulio yake, wakarudi nyuma.
48 Mfalme na jeshi lake wakasonga mbele ili kuwashambulia Wayahudi mjini Yerusalemu, wakapiga kambi Yudea na kwenye mlima Siyoni.
49 Mfalme akafanya amani na Wayahudi wa Beth-zuri, nao wakaondoka mjini hapo, kwa sababu hawakuwa na chakula cha kutosha mwaka huo wa Sabato, ambapo watu hawalimi wala hawapandi.
50 Mfalme akauteka mji wa Beth-zuri na kuweka kikosi cha kuulinda.
51 Halafu akalizunguka hekalu na kulizingira kwa muda mrefu. Akaandaa na kutega zana za kubomolea kuta, mitambo ya kurushia silaha, na vyombo vya kutupia moto, mawe na mishale, na makombeo.
52 Wayahudi nao wakatengeneza mitambo ya vita dhidi ya ile ya maadui, mapambano yakaendelea kwa siku nyingi.
53 Lakini hapakuwa na chakula kilichobaki kwa sababu ulikuwa mwaka wa Sabato, na watu waliokuwa wamewakimbia watu wa mataifa mengine na kujificha Yudea walikuwa wamekula chakula chote kilichowekwa akiba Yudea.
54 Uhaba wa chakula ulikuwa mkubwa hivi hata watu wengi wakawa wamerudi nyumbani kwao; wachache tu walibaki hekaluni.
55 Wakati huo, Filipo, yule aliyekuwa ameteuliwa na mfalme Antioko wa Nne amlee na kumwelimisha mtoto Antioko hata awe mfalme,
56 akarejea kutoka Persia na Media. Alikuwa amerudi na jeshi la mfalme, na alipanga kushika utawala wa serikali. Lisia aliposikia habari hizo,
57 akatoa amri ya kuondoka haraka. Akawaambia mfalme kijana, maofisa wake na watu wake: “Kila siku nguvu zetu zinapungua. Hatuna chakula cha kutosha, na mahali hapa tunapopazingira ni pagumu. Isitoshe, kuna mambo ya dharura ya kiserikali ambayo yanadai tuyashughulikie.
58 Basi, na tufanye mapatano ya amani na Wayahudi na taifa lao lote sasa.
59 Tutawaruhusu kushika na kufuata sheria zao na mila zao kama walivyofanya kabla yake. Matatizo haya yote yalianza tulipowachokoza Wayahudi kwa kuondoa na kutupilia mbali sheria, mila na desturi zao.”
60 Pendekezo hilo lilipokewa vizuri na mfalme na maofisa wake. Basi Lisia akawapa Wayahudi masharti ya amani, nao wakayapokea.
61 Mfalme na maofisa wake walipokubali kwa kiapo kuyashika masharti hayo, Wayahudi wakatoka ngomeni mwao.
62 Lakini mfalme alipoingia eneo la mlima Siyoni na kuona jinsi ngome hiyo ilivyokuwa imara, akavunja kiapo chake alichokuwa ameapa, akatoa amri ukuta ulioizunguka ngome ubomolewe.
63 Kisha akaondoka kwa haraka, akarejea Antiokia. Huko akamkuta Filipo ameushika mji, lakini akapigana naye, akauchukua mji wa Antiokia kwa nguvu.

Generic placeholder image