4

1 Gorgia akawachukua askari wa miguu 5,000 na wapandafarasi wenye uzoefu 1,000, akatoka nao usiku
2 kwenda kulishambulia ghafla jeshi la Wayahudi; walioongoza njia walikuwa walinzi wa ngome ya Yerusalemu.
3 Lakini Yuda aliugundua mpango huo, akaondoka na watu wake ili kulishambulia jeshi la mfalme kule Emau
4 wakati Gorgia na vikosi vyake bado hawajarejea kambini.
5 Basi, Gorgia na jeshi lake wakafika kwenye kambi la Yuda usiku huo. Hawakumkuta yeyote yule huko. Wakaanza kuwatafuta milimani, wakidhani kwamba walikuwa wametoroka.
6 Kulipopambazuka, Yuda alitokea kwenye tambarare akiwa na watu 3,000, lakini hawakuwa na silaha za kuwaridhisha.
7 Wakaliona jeshi kubwa la watu wa mataifa mengine, wenye uzoefu wa vita, wamejisheheneza silaha, na ngome yao imezungukwa na askari wapandafarasi.
8 Lakini Yuda akawaambia watu wake, “Msihangaike juu ya ukubwa wa jeshi lao, wala msiogope watakaposhambulia.
9 Kumbukeni jinsi wazee wetu walivyookolewa katika Bahari ya Shamu mfalme wa Misri alipokuwa anawafuatia na jeshi lake!
10 Sasa na tumwombe Mungu atuonee huruma. Tusali ili alishike agano lake na wazee wetu, na hivi aliponde jeshi mbele yetu leo.
11 Ndipo watu wote wa mataifa mengine watatambua kwamba kunaye mwenye kuwakomboa na kuwaokoa watu wa Israeli.”
12 Hao watu wa mataifa mengine walipochungulia na kuona Yuda na watu wake wanawajia,
13 wakatoka kambini mwao ili kupiga vita. Yuda na watu wake wakapiga tarumbeta
14 na kuanza kushambulia. Maadui wakatawanyika na kukimbilia kwenye tambarare,
15 na askari wao wote waliokuwa mstari wa nyuma wameuawa kwa upanga. Waisraeli wakawafukuza maadui hadi Gazara na tambarare za Idumea, mpaka Ashdodi na Yamnia. Adui 3,000 wakaangamia.
16 Halafu Yuda na kikosi chake wakaacha kuwafukuza maadui, wakarudi nyuma.
17 Yuda akawaambia watu wake, “Msiwe na pupa ya mateka. Tunakabiliwa bado na mapambano.
18 Gorgia na jeshi lake wapo hapo milimani, karibu nasi. Lazima tusimame imara na kumpiga adui. Baada ya ushindi, kila mmoja ataweza kuchukua mateka anayotaka.”
19 Kabla Yuda hajamaliza kusema hayo, kikosi cha adui kikatokeza, kikivizia kutoka milimani.
20 Mara kiligundua kwamba jeshi lake lilikuwa limefukuziwa mbali, na kwamba, kutokana na moshi waliouona, Wayahudi walikuwa wanalichoma moto kambi lake.
21 Ndipo wakashikwa na hofu kubwa. Na walipoliona jeshi la Yuda limejipanga kwenye tambarare, tayari kwa vita,
22 wote wakakimbilia nchi ya Wafilisti.
23 Basi, Yuda akarudi na kuliteka kambi la adui; wakapata dhahabu na fedha nyingi, nguo za buluu na urujuani, na mali nyingi.
24 Walipokuwa wanarudi kambini kwao, Wayahudi wakaimba utenzi wa sifa kwa Mungu: “Kwa kuwa yeye ni mwema, na huruma yake yadumu milele.”
25 Hivi, Israeli ilifaidi wokovu mkubwa siku hiyo.

Ushindi dhidi ya Lisia
(2Mak 11:1-12)
26 Wale wanajeshi wa mataifa mengine walionusurika walimwendea Lisia na kumwarifu yote yaliyokuwa yametukia.
27 Aliposikia hayo, Lisia alifadhaika na kuvunjika moyo, kwa vile Waisraeli hawakuwa wamepigwa kama alivyokuwa amekusudia wala hawakupatwa na yale aliyoamuru.
28 Mwaka uliofuata, Lisia akakusanya jeshi la askari wa miguu 60,000 na wapandafarasi 5,000 ili kuwashinda Wayahudi.
29 Wakaingia Idumea na kupiga kambi Beth-zuri. Yuda, pamoja na askari 10,000, akaja hapo kupambana nao.
30 Yuda alipoona kuwa jeshi la adui lilikuwa lenye nguvu, akasali, akisema: “Usifiwe wewe, Mwokozi wa Israeli, uliyekomesha mashambulio ya lile jitu kwa mkono wa mtumishi wako Daudi, ukalitia jeshi la Wafilisti mikononi mwa Yonathani mwana wa Shauli na yule kijana mchukuasilaha zake.
31 Sasa uyadhoofishe pia majeshi haya kwa mkono wa watu wako Israeli, uwafanye watu wake waone aibu juu ya askari wao wa miguu na wapandafarasi wao.
32 Uwajaze woga, uyeyushe uhodari wa nguvu yao, watetemeke katika maangamizi.
33 Uwaangushe chini kwa upanga wa wale wakupendao, na kuwawezesha wote walijualo jina lako wakusifu kwa nyimbo.”
34 Ndipo vita vikaanza; katika mapambano, waliuawa watu 5,000 wa Lisia.
35 Lisia alipoona jeshi lake linalemewa, na alipoona ujasiri na ushupavu wa Yuda na watu wake - ambao walionesha kwamba walikuwa tayari kuishi au kufa kuilinda hadhi yao - akarudi Antiokia. Huko akaandikisha askari wa kukodi, ili aende tena Yudea siku za mbele na jeshi kubwa zaidi.

Kulitakasa hekalu
(2Mak 10:1-8)
36 Yuda na ndugu zake wakasema: “Sasa maadui zetu wameshindwa. Twende zetu Yerusalemu tukalitakase hekalu na kulitabaruku upya.”
37 Basi, jeshi lote likakusanyika, likaenda kwenye mlima Siyoni.
38 Huko watu wakakuta hekalu limeachwa ukiwa, madhabahu yake imetiwa unajisi, milango yake imechomwa moto, nyasi na vichaka vimeota katika nyua zake kama porini au milimani, na vyumba vya makuhani vimebomolewa.
39 Hapo wakararua mavazi yao, wakalia na kuomboleza kwa huzuni kubwa, wakijitia majivu kichwani
40 na kuanguka kifudifudi. Tarumbeta ilipopigwa kutoa alama, kila mmoja alimlilia Bwana.
41 Halafu Yuda, akawaamuru baadhi ya askari wake wawashambulie watu waliokuwa ngomeni, wakati yeye analitakasa hekalu.
42 Aliwachagua makuhani kadha waliostahili na walioshika sheria kiaminifu.
43 Hao wakalitakasa hekalu, wakayachukua mawe yaliyokuwa yametiwa unajisi na kuyapeleka nje mahali pachafu.
44 Wakajadiliana wafanye nini na madhabahu ya sadaka za kuteketezwa, ambayo ilikuwa imetiwa unajisi.
45 Wakaamua afadhali kuibomoa, ili isibaki imesimama hekaluni na kuwaletea lawama kwa vile watu wa mataifa walikuwa wameitia unajisi. Basi, wakaibomoa madhabahu
46 na kuyahifadhi mawe yake mahali pazuri juu ya mlima wa hekalu, mpaka nabii atokee wa kuamua nini cha kuyafanyia mawe hayo.
47 Halafu wakachukua mawe yasiyochongwa, kwa mujibu wa sheria, wakajenga madhabahu mpya, sawa na madhabahu ya zamani.
48 Hali kadhalika walilifanyia matengenezo hekalu, ndani na nje, wakazitakasa na nyua zake.
49 Walitengeneza vyombo vipya kwa ajili ya ibada, na wakaingiza hekaluni kinara, madhabahu ya ubani, na meza ya mikate.
50 Wakafukiza ubani juu ya madhabahu, na kuwasha taa za kinarani zipate kuangaza hekaluni.
51 Wakaweka mikate mezani, wakatundika mapazia, na kumaliza kazi yote waliyokuwa wamenuia kufanya.
52 Mapema asubuhi, siku ya ishirini na tano ya mwezi wa tisa, yaani, mwezi wa Kislevu, mwaka 148,
53 wakaamka na kutambika, kadiri ya sheria, juu ya madhabahu mpya waliyokuwa wamejenga.
54 Hivi, waliiweka wakfu madhabahu mpya kwa nyimbo na muziki wa vinubi na vinanda na matari, wakati ule ule na siku ileile ilipotiwa unajisi na watu wa mataifa mengine, mwaka mmoja kabla yake.
55 Watu wote wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu na kumsifu Bwana aliyewafanikisha.
56 Kwa siku nane waliadhimisha sikukuu ya kuitabaruku madhabahu, wakatolea kwa furaha sadaka za kuteketezwa, na kutoa tambiko ya wokovu na shukrani.
57 Waliupamba ukuta wa mbele wa hekalu kwa taji za dhahabu na ngao ndogondogo; wakatengeneza milango ya hekalu; wakajenga upya vyumba vya makuhani na kuweka milango.
58 Watu walikuwa na furaha kubwa sana, nayo aibu iliyoletwa na watu wa mataifa mengine ikawa imeondolewa.
59 Kisha, Yuda na nduguze na jumuiya yote ya Israeli wakaamua kwamba kila mwaka wakati kama ule ifanyike, kwa furaha na shangwe, kumbukumbu ya kutabaruku madhabahu kwa muda wa siku nane, kuanzia siku ya ishirini na tano ya mwezi Kislevu.
60 Halafu wakajenga kuta ndefu na minara imara kuuzunguka mlima Siyoni, kuwazuia watu wa mataifa mengine wasiingie tena na kuikanyaga kama walivyofanya.
61 Yuda akaweka kikosi cha askari hapo ili kulinda hekalu. Pia aliuimarisha mji wa Beth-zuri, ili watu wa Israeli wawe na ngome moja inayokabiliana na Idumea.

Generic placeholder image