16

1 Yohane, mwana wa Simoni, akaondoka Gazara, akaenda kumwarifu baba yake mambo aliyokuwa amefanya Kendebeo.
2 Simoni akawaambia Yohane na Yuda, wanawe wakubwa, “Mimi na ndugu zangu, na familia yote ya baba yangu, tumepiga vita vya Israeli maisha yetu yote, na mara nyingi tumefanikiwa kuiokoa Israeli.
3 Mimi sasa ni mzee, lakini nyinyi, shukrani kwa Mungu, mmejaa utomvu wa utu uzima. Lazima mchukue nafasi yangu na ile ya ndugu yangu katika kulipigania taifa letu. Bwana awe nanyi kuwasaidia.”
4 Hapo Yohane akaunda jeshi la Kiisraeli la askari hodari na wapandafarasi 20,000, akaondoka kumkabili Kendebeo. Baada ya kulala Modeini,
5 mapema asubuhi iliyofuata wakaelekea kwenye tambarare. Huko wakaona jeshi kubwa la askari wa miguu na wapandafarasi linakuja kupambana nao, lakini kati yao na maadui palikuwa na mto.
6 Yohane na jeshi lake wakajipanga kivita dhidi ya maadui, na askari walipoonesha wanaogopa kuvuka mto, Yohane akatangulia kuvuka, na watu wake wakamfuata.
7 Yohane akaligawa jeshi lake na kuwaweka wapandafarasi katikati ya askari wa miguu, kwa sababu idadi ya maadui wapandafarasi ilikuwa kubwa sana.
8 Tarumbeta zilipigwa, mapambano yakaanza. Kendebeo na jeshi lake walipigwa vibaya sana, wakashindwa na kupoteza askari wengi. Walionusurika kifo wakakimbilia Kedroni, kwenye ngome yao.
9 Yuda alikuwa amejeruhiwa vitani, lakini nduguye, Yohane, akaendelea kuwafuatia maadui hadi Kedroni, mji ambao Kendebeo alikuwa ameujenga upya.
10 Askari hao waliokuwa wanatoroka walikimbilia kwenye minara iliyokuwa katika mashamba ya Ashdodi na Yohane akauchoma moto mji huo. Siku hiyo askari 2,000 wa maadui waliuawa; Yohane akarejea salama Yudea.

Kuuawa kwa Simoni na wanawe wawili
11 Simoni, kuhani mkuu, alikuwa amemteua Tolemai, mwana wa Abubo, awe kamanda kwa ajili ya tambarare za Yeriko. Tolemai alikuwa tajiri sana,
12 kwa sababu alikuwa mkwe wa Simoni.
13 Lakini alikuwa na tamaa mno, akataka kuchukua utawala wa nchi. Hivi akafanya hila ya kumwua Simoni na wanawe.
14 Simoni, pamoja na wanawe, Matathia na Yuda, alikuwa anatembelea miji mbalimbali, ili kuona mahitaji yao. Mwezi wa Shebati yaani wa kumi na moja, mwaka 177, wakawasili Yeriko.
15 Tolemai, akiwa bado anakula njama ya kumwua Simoni na wanawe, akawapokea katika ngome ndogo iliyoitwa Doki ambayo alikuwa ameijenga mwenyewe. Akawafanyia karamu kubwa, lakini alikuwa amewaficha watu humo ngomeni.
16 Simoni na wanawe walipokuwa wamelewa, Tolemai na watu wake wakajitokeza na mapanga mikononi, wakaingia mbio katika ukumbi wa karamu, wakawaua Simoni na wanawe wawili, na baadhi ya wahudumu.
17 Kwa tendo hilo ovu na la uhaini, Tolemai alikuwa amelipa jema kwa baya.
18 Kisha Tolemai akaandika taarifa ya hayo aliyokuwa ametenda, akaipeleka kwa mfalme. Katika taarifa hiyo aliomba apelekewe askari wa kumsaidia, na kwamba apewe utawala wa miji na wa nchi yenyewe.
19 Aliandika barua kwa maofisa wa jeshi akiwaalika wajiunge naye na kuwaahidia fedha, dhahabu, na zawadi maridhawa. Halafu akawatuma baadhi ya watu wake kwenda Gazara kumwua Yohane,
20 na wengine kwenda kushika mji wa Yerusalemu na mlima wa hekalu.
21 Lakini mtu mmoja akapiga mbio, akafika Gazara kabla watu hao wa Tolemai hawajafika, akamwarifu Yohane kwamba baba yake na ndugu zake walikuwa wameuawa, na kwamba Tolemai alikuwa amewatuma askari kumwua yeye Yohane.
22 Yohane alifadhaika sana aliposikia hayo, lakini, kwa vile alikuwa ametahadharishwa kabla, alifaulu kuwakamata na kuwaulia mbali watu waliokuwa wametumwa kumuua yeye.
23 Habari nyingine za Yohane: Kuhusu vita vyake, matendo yake ya ujasiri, ujenzi wake wa kuta, na mafanikio yake mengine,
24 zote zimeandikwa katika kumbukumbu za utawala wake kama kuhani mkuu, tangu alipoupata baada ya baba yake.

Generic placeholder image