1

BARUA KWA WAYAHUDI WA MISRI
1 “Kutoka kwa Wayahudi wa Yerusalemu na Yudea, kwa ndugu zao walio Misri. Salamu na amani!
2 “Mungu awafanikishe, na kulitekeleza agano lake alilofanya na watumishi wake waaminifu: Abrahamu, Isaka, na Yakobo.
3 Mungu amjaze kila mmoja wenu ari ya kumwabudu, kuyatekeleza matakwa yake kwa moyo wote na kwa hiari kamili.
4 Mungu awajalie muweze kuzielewa sheria na amri zake. Tunaomba awajalieni amani,
5 asikilize sala zenu, awasamehe dhambi zenu na asiwatupe kamwe wakati wa shida.
6 Ndivyo tunavyowaombea nyinyi tukiwa hapa Yudea.
7 “Mwaka wa 166, Demetrio wa Pili alipokuwa mfalme sisi Wayahudi huku tuliwaandikieni kuhusu taabu na wakati mgumu tuliokuwa nao miaka ile baada ya Yasoni na kikundi chake kufanya maasi katika nchi takatifu.
8 Yasoni na watu wake waliuchoma moto mlango wa hekalu na kuwaua watu wasio na hatia. Tulimwomba Bwana, naye akasikiliza sala zetu. Tulitoa tambiko ya wanyama na ya nafaka safi tukawasha taa hekaluni na kuweka mikate mitakatifu.
9 Kwa sababu hiyo tunawasihi mwadhimishe kila mwezi wa Kislevu sikukuu kama ile ya vibanda. Mwaka wa 188.

BARUA KWA ARISTOBULO
10 “Sisi watu wa Yerusalemu na Yudea, na Baraza Kuu la wazee na Yuda tunakuandikia wewe Aristobulo, mzawa wa makuhani na mwalimu wa mfalme Tolemai, na Wayahudi walio Misri. Twakusalimu na kukutakia afya njema.
11 “Tunamshukuru Mungu kwa sababu alituokoa katika hatari kubwa, akitusaidia dhidi ya mfalme.
12 Mungu ndiye aliyewafukuza maadui kutoka mji wetu mtakatifu.
13 Mfalme Antioko alipofika Persia na jeshi lililoonekana halishindiki, askari hao walikatwa vipandevipande katika hekalu la Nanea kwa sababu ya hila walizofanya makuhani wa huyo mungu wa kike, Nanea.
14 Antioko alikuwa amekwenda hekaluni pamoja na baadhi ya washauri wake ati kumwoa huyo mungu wa kike, lakini shabaha yake ya kweli ilikuwa kujipatia hazina zilizowekwa humo hekaluni kama mahari.
15 Makuhani walipokuwa wamefungua hazina, na Antioko na watu wake wachache wakaingia ndani hekaluni kuchukua mali, walifunga milango mara,
16 wakawatupia mawe kutoka darini ambamo walikuwa wamefungua mlango fulani wa siri, wakakatakata miili yao na kutupa vichwa vyao nje kwa watu.
17 Atukuzwe Mungu wetu kwa kila namna, kwa maana amewahukumu adhabu hao waovu!

Moto wateketeza tambiko ya Nehemia
18 “Siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Kislevu tutaadhimisha sikukuu ya kutakaswa kwa hekalu, kama vile tunavyoadhimisha sikukuu ya vibanda. Tuliona ni lazima kuwakumbusheni hilo, ili nanyi pia muweze kuadhimisha sikukuu hiyo. Mtakumbuka jinsi moto ulivyozuka wakati Nehemia alipotoa tambiko baada ya kumaliza kujenga upya hekalu na madhabahumeza ya sadaka yake.
19 Wakati wazee wetu walipokuwa wanapelekwa uhamishoni huko Persia, makuhani wacha Mungu wachache walichukua moto kidogo kutoka madhabahuni, wakauficha kwa siri mvunguni ndani ya kisima kikavu. Huo moto waliuficha vizuri hata haukugunduliwa na yeyote yule.
20 Miaka mingi baadaye, Mungu alipowahurumia watu, mfalme wa Persia alimrudisha Nehemia Yerusalemu. Nehemia akawaambia wazawa wa wale makuhani kuutafuta ule moto. Walirudisha ripoti kwetu kwamba walikuwa hawajaona moto, ila tu maji mazito. Nehemia akawaambia wakateke maji hayo na kumletea.
21 Wakati vitu vyote vinavyohitajiwa kwa ajili ya tambiko vilipokuwa vimewekwa juu ya madhabahu, Nehemia akawaambia makuhani kumwaga hayo maji juu ya kuni na juu ya tambiko.
22 Wakafanya hivyo. Wakati huo wote jua lilikuwa limefichwa na mawingu. Kitambo baadaye, jua likaangaza, na ghafla kila kitu madhabahuni kikalipuka moto. Watu wote waliangalia kwa mshangao.
23 Hapo, moto ulipokuwa unateketeza tambiko, Yonathani, kuhani mkuu, akaanzisha sala, na watu wengine wote wakamwitikia, wakiongozwa na Nehemia.”

Sala ya Nehemia
24 Sala ya Nehemia ilisema hivi: “Bwana Mungu, Muumba wa vitu vyote! Wewe ni wa kutisha na mwenye nguvu, papo hapo mwingi wa huruma na haki. Wewe peke yako ni mfalme. Hapana aliye mwema ila wewe;
25 hapana aliye na fadhili na mwenye kutenda sawa ila wewe. Wewe ni mwenye nguvu na wa milele. Wewe wawaokoa Waisraeli katika uovu wowote; uliwachagua wazee wetu na kuwaweka wakfu kwako.
26 Ipokee tambiko hii tunayokutolea kwa niaba ya watu wako Waisraeli wote; uwalinde hao wateule wako na kuwafanya watakatifu.
27 Uwakusanye pamoja watu wetu waliotawanyika. Uwaachilie huru wale walio watumwa katika nchi za kigeni. Uwaangalie kwa huruma watu wetu ambao wananyanyaswa na kudharauliwa, uyafanye mataifa mengine yote yajue kwamba wewe ni Mungu wetu.
28 Uwaadhibu wakatili na wafidhuli waliotukandamiza.
29 Uwasimike watu wako katika nchi yako takatifu, kama Mose alivyosema.”

Mfalme wa Persia asikia kuhusu moto
30 “Kisha, makuhani wakaimba tenzi.
31 Na tambiko ilipokwisha teketezwa, Nehemia aliamuru maji yaliyobaki yamwagwe juu ya mawe makubwamakubwa.
32 Mara moto ukalipuka, lakini ukazimishwa na mwanga wa moto ule wa madhabahuni.
33 “Habari za matukio hayo zilienea kila mahali. Mfalme wa Persia alisikia kwamba maji fulani yamegunduliwa mahali ambapo makuhani walikuwa wameficha moto wa madhabahuni kabla hawajapelekwa uhamishoni. Pia alisikia kwamba Nehemia na rafiki zake walikuwa wametumia maji hayo kuteketezea tambiko madhabahuni.
34 Mfalme alipochunguza hayo na kubainisha kwamba ilikuwa kweli, akaamuru mahali hapo pazungushiwe ua, akapafanya mahali patakatifu pa kuhiji.
35 Kwa namna hiyo mfalme alipata fedha nyingi kutokana na mahali hapo, naye akaitumia kwa kutoa zawadi kwa yeyote aliyempenda.
36 Nehemia na rafiki zake wakayaita maji hayo ‘nafthari,’ yaani utakaso; lakini karibu watu wote huyaita maji hayo ‘naftha.’

Generic placeholder image