5

Maono na mapigano angani
1 Yapata wakati huo huo, Antioko wa Nne aliishambulia Misri kwa mara ya pili.
2 Kwa siku karibu arubaini, kila mahali Yerusalemu watu walipata maono, wakaona wapandafarasi wenye mavazi ya dhahabu wakienda kwa nguvu angani. Wapandafarasi hao walikuwa wameshika mikuki na kuinua mapanga juu.
3 Walijipanga kivita, kila mmoja na adui, wakishambuliana. Ngao ziligonganishwa kwa mshindo, mikuki ilirushwa kama mvua ya upepo, na mishale ilichakaza anga. Mavazi ya aina mbalimbali na deraya za dhahabu vilimetameta kwa mwanga wa jua.
4 Kila mmoja mjini alisali na kuomba maono hayo yabashiri mema.

Yasoni ashambulia Yerusalemu
5 Habari za uongo zilienea kwamba Antioko alikuwa amekufa. Basi, Yasoni akakusanya watu zaidi ya 1,000, akaishambulia Yerusalemu kwa ghafla. Wakawarudisha nyuma watu waliokuwa wamepangwa kwenye kuta za mji, wakaiteka Yerusalemu hatimaye. Menelao akakimbilia ngomeni, karibu na mlima wa hekalu,
6 wakati Yasoni na watu wake wanaendelea kuwaua Wayahudi wenzao bila huruma. Yasoni hakutambua kwamba kuwashinda watu wa taifa lake kulikuwa ni balaa lisilo na kifani. Alifanya kana kwamba anawashinda adui, na wala si wananchi wenzake.
7 Hata hivyo, Yasoni hakufaulu kuichukua serikali. Badala yake alilazimika kukimbilia tena kwenye nchi ya Waamoni, na hatimaye uasi wake ulimletea aibu na fedheha,
8 akafa katika hali mbaya sana. Areta, mtawala wa Waarabu, alikuwa amemtia ndani Yasoni; alikuwa amehesabiwa kama mhalifu, akadharauliwa kwa sababu alikuwa amelisaliti taifa lake mwenyewe; kila mmoja alikuwa anamwinda Yasoni, hivi alikuwa amelazimika kukimbia kutoka mji hadi mji. Alikimbilia kujisalimisha huko Misri,
9 na hatimaye alikimbilia Lakedemonia akitumaini kupokewa kama mkimbizi kwa sababu ya uhusiano na Wayahudi. Mwishowe, mtu huyu, aliyekuwa amewalazimisha wengine wengi kukimbia kutoka nchini mwao, alikufa akiwa mkimbizi katika nchi ya kigeni.
10 Yasoni alikuwa ameua watu wengi na kuwaacha bila kuwazika, sasa yeye mwenyewe alikufa, asiwe na mtu wa kumwombolezea; hakuzikwa wala kuwa na nafasi katika kaburi la wazee wake.

Antioko ashambulia Yerusalemu
(1Mak 1:20-63)
11 Habari za mambo yaliyokuwa yametukia Yerusalemu zilipomfikia, mfalme Antioko alidhani kuwa nchi nzima ya Yudea ilikuwa imeasi. Basi, kwa hasira kali aliondoka Misri, akashambulia Yerusalemu
12 na kuwaamuru watu wake wamuulie mbali bila huruma kila mtu ambaye wangekutana naye au kumfuma amejificha nyumbani.
13 Wakawaua watu wote, wanaume kwa wanawake, wavulana kwa wasichana; hata watoto wachanga wakawaulia mbali.
14 Kwa muda wa siku tatu Yerusalemu ilikuwa imepoteza watu 80,000: 40,000 waliouawa katika mapigano ya ana kwa ana na maelfu kama hao waliouawa walichukuliwa na kuuzwa utumwani.
15 Bila kutosheka na hayo, Antioko alithubutu hata kuingia katika hekalu lililo takatifu kushinda yote ulimwenguni, akiongozwa na Menelao, yule aliyekuwa msaliti kwa dini yake na kwa taifa lake.
16 Kwa mikono yake michafu na najisi, Antioko akavikumba vyombo vitakatifu na vitu ambavyo wafalme wengine walikuwa wametoa zawadi ili kuongeza utukufu na heshima ya hekalu.
17 Antioko alijawa na msisimko na furaha juu ya ushindi wake hata hakutambua ya kwamba kwa kitambo tu Bwana alikuwa ameachilia hekalu lake takatifu litiwe unajisi kwa sababu dhambi ya watu wa Yerusalemu.
18 Kama watu wa Yerusalemu wasingekuwa wamehusika na dhambi hizo nyingi, Antioko angekuwa ameadhibiwa mara na kuzuiwa kufanya kitendo cha kipumbavu namna hiyo. Yangekuwa yamempata kama yale yaliyompata Heliodoro, aliyekuwa ametumwa na mfalme Seleuko kukagua hazina.
19 Lakini Bwana hakuwachagua watu wake kwa ajili ya hekalu lake, bali alilichagua hekalu lake kwa ajili ya watu wake.
20 Kwa hiyo hekalu lilishiriki katika misiba ya taifa, hali kadhalika, baadaye lilishiriki katika ufanisi wake. Kwa hasira ya Mungu Mwenye Nguvu liliachwa, lakini Bwana alipopatanishwa lilirekebishwa tena.

Yerusalemu yashambuliwa tena
21 Antioko alichukua kutoka hekaluni fedha kilo 62,000, akaenda zake kwa haraka Antiokia. Alikuwa na kiburi hata akadhani angeweza kuzifanya meli zisafiri nchi kavu, na askari watembee kuvuka bahari.
22 Aliwateua magavana wa kuwanyanyasa watu. Huko Yerusalemu alimweka Filipo, mtu wa Frugia ambaye alikuwa mwovu zaidi kuliko Antioko mwenyewe.
23 Kwenye mlima Gerizimu alimweka Androniko. Zaidi ya hao, alikuwako Menelao, ambaye aliwatendea Wayahudi wenzake vibaya zaidi kuliko walivyofanya hao magavana. Antioko aliwachukia Wayahudi
24 hata akapeleka Yerusalemu jeshi la askari wa kukodiwa 22,000 kutoka Misia, chini ya uongozi wa mtu aliyeitwa Apolonio. Alikuwa amewaamuru waende wakawaue watu wote mjini na kuwauza utumwani wanawake na watoto.
25 Apolonio aliwasili Yerusalemu, akijidai eti anatafuta amani. Na halafu siku ya Sabato, Wayahudi wote walipokuwa wanapumzika, aliwaamuru askari wake washike silaha na kujipanga nje ya mji.
26 Ghafla akawapa amri ya kumuua kila mmoja aliyekuwa ametoka nje kuwatazama askari hao. Halafu wakaingia kwa haraka mjini na kuwaua watu wengi sana.
27 Lakini Yuda Makabayo na wengine wapatao tisa walitorokea milimani, ambako waliishi kama wanyama wa porini. Ili wasijitie unajisi, walikula mimea ya porini tu.

Generic placeholder image