10

Kutakaswa hekalu
(1Mak 4:36-61)
1 Yuda Makabayo na wafuasi wake, chini ya uongozi wa Bwana, walitwaa tena hekalu na mji wa Yerusalemu.
2 Wakazibomolea mbali madhabahu zilizokuwa zimejengwa na wageni sokoni, wakapaharibu na mahali pengine palipojengwa kufanyia ibada.
3 Walilitakasa hekalu na kujenga madhabahu mpya. Halafu, wakawasha moto kwa kugonganisha mawe, wakatoa tambiko kwa mara ya kwanza katika miaka miwili, wakafukiza ubani, wakawasha taa na kuweka mbele mikate mitakatifu.
4 Baada ya kufanya hayo walilala sakafuni kifudifudi na kusali ili Bwana asiruhusu tena misiba kama ile kuwafikia. Walimwomba awe na huruma wakati wa kuwaadhibu kwa dhambi ambazo wangetenda baadaye, asiwatie tena mikononi mwa watu waovu, wenye kumtukana Mungu na wasio na adabu.
5 Walilitakasa hekalu siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Kislevu, siku na mwezi ule ule hekalu lilipotiwa unajisi na watu wa mataifa mengine.
6 Kwa siku nane watu walisherehekea kwa shangwe, kama kwa sikukuu ya vibanda, na wakakumbuka jinsi, kitambo kidogo tu kabla yake, walivyokuwa wameipitisha sikukuu ya vibanda wakitangatanga milimani na katika mapango kama wanyama wa porini.
7 Basi, wakiwa wamechukua mikononi matawi mabichi ya mitende na fimbo zilizopambwa majani, waliandamana kuzunguka, wakiimba nyimbo za sifa na shukrani kwake yeye aliyekuwa amewezesha hekalu lake mwenyewe litakaswe.
8 Waliamua kwa tangazo rasmi waliloafikiana kwa kura kwamba taifa lote la Wayahudi liadhimishe siku hizo kila mwaka.
9 Ndivyo ilivyokuwa mwisho wa Antioko aliyeitwa Epifane. Tolemai Makroni ajiua
10 Sasa tutasimulia mambo yaliyotukia chini ya Antioko Eupatori, mwana wa huyo mtu ambaye hakumjali Mungu, na tutatoa muhtasari wa maafa makuu yaliyosababishwa na vita vyake.
11 Alipotawazwa mfalme, Antioko Eupatori alimteua mtu mmoja aliyeitwa Lisia awe waziri wa mambo ya nchi na gavana mkuu wa Siria Kuu na Foinike
12 badala ya Tolemai Makroni, ambaye alikuwa gavana wa kwanza aliyewatendea Wayahudi kwa haki. Makroni alikuwa amejenga uhusiano wa amani na Wayahudi, katika jitihada zake za kufukia maovu waliyokuwa wametendewa.
13 Kwa sababu hiyo rafiki za mfalme walimwendea Eupatori, wakamshtaki Makroni kuwa msaliti, kwa vile alikuwa amekiacha kisiwa cha Kupro alichokabidhiwa na mfalme Filometori wa Misri, na alikuwa amemfuata Antioko Epifane. Kila mmoja alimwita Makroni msaliti, na hakuweza tena kuwa na heshima ile iliyodaiwa na wadhifa wake; kwa hiyo hivi akajiua kwa sumu.

Yuda Makabayo awashinda Waidumea
(1Mak 5:1-8)
14 Gorgia alipotawazwa kuwa gavana wa mkoa wa Idumea, alijipatia jeshi la askari wa kukodiwa, akawa anawashambulia Wayahudi kila alipobahatika kufanya hivyo.
15 Zaidi ya hayo, Waidumea wenyewe walishika ngome muhimu kadha, wakawa wanawanyanyasa Wayahudi mara kwa mara. Waliwakaribisha wale waliokimbia kutoka Yerusalemu, na kujaribu kuidumisha nchi katika hali ya vita.
16 Basi, Yuda Makabayo na watu wake, baada ya kumwomba Mungu, wakatoka mbio na kuzishambulia kwa nguvu ngome hizo za Waidumea.
17 Waliwarudisha nyuma askari waliokuwa wanalinda kuta, wakaziteka hizo ngome na kuwaua watu wapatao 20,000.
18 Hata hivyo, askari wa maadui 9,000 hivi walifaulu kukimbia na kujificha katika minara imara miwili, ambayo ilikuwa na kila kitu walichohitaji kustahimili kuzingirwa.
19 Yuda alipaswa kwenda mahali pengine nchini, ambako alihitajika haraka zaidi. Lakini hapo aliwaacha Simoni na Yosefu, pamoja na Zakayo na watu wake. Jeshi hilo lingetosha kuendelea kuzingira,
20 lakini baadhi ya watu wa Simoni walikuwa na uchu wa fedha; walipopewa rushwa ya fedha drakma 70,000 waliwaachilia baadhi yao watoroke kutoka minarani.
21 Yuda alipopata habari za tukio hilo, aliwakusanya pamoja viongozi wa vikosi vyake, akawashtaki hao wala rushwa kwamba walikuwa wamewauza ndugu zao kwa kuwaachilia huru maadui zao warudi kupigana nao.
22 Hapo akawaulia mbali hao wasaliti, akaishambulia na kuiteka ile minara miwili.
23 Katika vita Yuda alifanikiwa daima, na katika shambulio hilo kwenye minara miwili aliwaua watu zaidi ya 20,000.

Yuda amshinda Timotheo
24 Timotheo, ambaye alikuwa amewahi kupigwa na Wayahudi kabla yake, alikuwa amekusanya idadi kubwa ya askari wapandafarasi kutoka Asia, na jeshi la kutisha la askari wa kukodiwa, akawa sasa anasonga mbele kuishambulia na kuitwaa Yudea.
25 Lakini hao maadui walipokuwa wanakaribia, Yuda na watu wake wakamwomba Mungu. Walivaa nguo za gunia, wakajimwagia mavumbi kichwani,
26 na kulala kifudifudi juu ya ngazi za kupandia madhabahuni, wakimwomba Mungu awasaidie kupigana na maadui zao, kama alivyokuwa ameahidi katika sheria yake.
27 Walipomaliza kusali, walichukua silaha zao, wakaenda mbali kidogo na Yerusalemu, na kusimama, karibu na adui.
28 Kulipopambazuka tu, mapambano yakaanza kati ya majeshi hayo mawili. Jeshi la Wayahudi lilitegemea kushinda kutokana na ujasiri wa askari na tumaini lao kwa Bwana, ambapo maadui walitegemea tu uwezo wao wa kupigana kikakamavu.
29 Vita vilipokuwa vimepamba moto kabisa, maadui waliwaona wanaume watano wenye sura za kupendeza wamepanda farasi wenye matandiko ya dhahabu, wakiongoza jeshi la Wayahudi.
30 Hao watu watano walimzunguka Yuda, wakimlinda kwa ngao zao wenyewe na kuwatupia maadui mishale na radi. Askari adui wakapumbazika na kuchanganyikiwa hata wakavunja mistari, nao Wayahudi wakawakata vipandevipande na
31 kuwaua askari wa miguu 20,500, na askari wapandafarasi 600.
32 Timotheo mwenyewe alitorokea kwenye ngome imara sana iitwayo Gazara, ambayo ilikuwa chini ya Kaerea, nduguye Timotheo.
33 Yuda Makabayo na watu wake wakaizingira ngome hiyo kwa muda wa siku nne,
34 lakini watu waliokuwa ngomeni walijisikia wapo salama kabisa, wakawa wanaendelea kumtukana Mungu vibaya na kutoa matusi.
35 Lakini siku ya tano, mapema asubuhi, watu ishirini wa Yuda, wakiwa wanawaka kwa hasira kutokana na kufuru hizo, walipanda ukuta wa ngome kwa ujasiri, wakamuulia mbali kila waliyemkuta.
36 Wakati huo huo, wengine walipanda kuta za ngome kwa upande mwingine, wakaitia moto minara yake. Maadui wengi waliuawa kwa moto huo. Kikosi kingine kikavunja milango na kuwaingiza askari wakauteka mji huo.
37 Timotheo alikuwa amejificha katika tangi. Hata hivyo, walimwulia mbali yeye, pamoja na ndugu zake, Kaerea na Apolofane.
38 Baada ya hayo Wayahudi walisherehekea kwa kuimba tenzi na nyimbo za shukrani kwa Bwana, ambaye alikuwa amewafadhili kwa wingi na kuwapatia ushindi.

Generic placeholder image