13

Menelao auawa
1 Mwaka 149, Yuda Makabayo na wafuasi wake walipata habari kwamba Antioko Eupatori alikuwa anakuja na jeshi kubwa kuikabili Yudea,
2 na kwamba Lisia, yule mlinzi wa mfalme na mkuu wa serikali, alikuwa pamoja na huyo Antioko. Kila mmoja wao alikuwa na jeshi la askari Wagiriki wa miguu 110,000, wapandafarasi 10,000, wapandafarasi 5,300, tembo 22, na magari 300 yaliyofungiwa miti yenye ncha kali.
3 Menelao alijiunga nao pia, na kwa unafiki akawahimiza kuendelea na harakati hiyo, si kwa sababu aliitakia mema nchi, ila kwa sababu alitumaini angethibitishwa katika wadhifa wa kuhani mkuu.
4 Lakini Mfalme wa wafalme, akamtia Antioko hasira dhidi ya Menelao. Lisia alimhakikishia Antioko kwamba huyo mwovu ndiye aliyekuwa amesababisha shida na matatizo yake yote; kwa hiyo Antioko akaamuru Menelao apelekwe mjini Berea na kuuawa huko kwa mtindo wa hukohuko.
5 Katika mji huo umo mnara wenye urefu wa mita 22 hivi kwenda juu. Umejazwa majivu, na, kuzunguka mnara huo, kwa ndani, kuna jukwaa ambalo ngazi zake zateremkia kwenye majivu hayo.
6 Watu wanaoshtakiwa kwa kuikosea miungu, au kwa kufanya kosa kubwa lingine lolote lile, hupelekwa huko mnarani na kusukumizwa chini wafe.
7 Basi, Menelao aliuawa kwa njia hiyo, akakosa hata fursa ya kuzikwa;
8 na hilo ndilo alilostahili. Maana mara nyingi alikuwa ameyatumia vibaya majivu matakatifu ya moto wa madhabahuni hekaluni, na sasa alikufa katika majivu.

Mapigano karibu na mji wa Modeini
9 Mfalme Antioko, kwa kiburi chake, alipania kuja kuwatesa Wayahudi kwa mateso makali zaidi kuliko baba yake alivyokuwa amewatesa.
10 Yuda alipopata kujua hilo, akawaamuru watu wake wamwombe Bwana usiku na mchana, kwa sababu walikuwa katika hatari ya kupoteza sheria yao, nchi yao, na hekalu lao takatifu; walihitaji sana msaada wa Bwana na ulinzi wake
11 ili nchi yao waliyokuwa wamerudishiwa isitue tena mikononi mwa watu wa mataifa mengine wenye kumkufuru Mungu.
12 Kwa siku tatu watu walibaki wamelala kifudifudi vumbini, wakifunga na kulia na kumwomba Bwana mwenye huruma awasaidie. Kisha Yuda akawatia moyo na kuwaamuru wakae tayari.
13 Baada ya kushauriana faraghani na wazee wa Wayahudi, Yuda akaamua kutoka na kwenda kumkabili mfalme kwa msaada wa Mungu, kabla ya Antioko kuivamia Yudea na kuuteka mji wa Yerusalemu.
14 Kwa hiyo, akiwa amemwachia uamuzi Mungu Muumba wa ulimwengu, Yuda akawatia moyo watu wake kupiga vita kwa ushujaa, na kuwa tayari kufa kwa ajili ya sheria zao, hekalu, Yerusalemu, nchi yao, na utamaduni wao. Basi akapiga kambi karibu na mji wa Modeini.
15 Yuda akawapa watu wake shime hii ya vita: “Ushindi hutoka kwa Mungu.” Basi, usiku ule, akiwa na kikosi maalumu cha vijana hodari kabisa, Yuda akafanya mashambulizi karibu na hema la mfalme na kuwaua watu wasiopungua 2,000. Pia akamchoma mkuki na kumuua tembo kiongozi na mpandaji wake.
16 Mwishowe, kila mmoja kambini alijawa na kitisho na woga, naye Yuda na watu wake wakaondoka kwa ushindi.
17 Hayo yalitukia jua lilipokaribia kuchomoza, na yote yaliwezekana kwa kuwa Bwana aliwalinda.

Antioko wa Tano afanya mkataba na Wayahudi
(1Mak 6:48-63)
18 Mfalme Antioko alikuwa ameuonja huo ujasiri wa Wayahudi, akajaribu mbinu nyingine za kuyateka maboma yao.
19 Aliishambulia ngome yao imara ya Beth-zuri, lakini tena na tena alipigwa, na hatimaye akashindwa kabisa.
20 Yuda aliwapelekea mahitaji ya lazima wale waliokuwa wanailinda ngome hiyo.
21 Lakini askari mmoja wa Kiyahudi, kwa jina Rodoko, akawafunulia maadui siri fulani. Huyo aligunduliwa, akakamatwa na kutiwa ndani.
22 Mfalme akajaribu kwa mara ya pili kufikia maafikiano na watu wa Beth-zuri, na alipofanikiwa, akaondoa askari wake. Halafu akaenda kumshambulia Yuda na watu wake, lakini tena akapigwa na kushindwa.
23 Wakati huo, mfalme Antioko alipata habari kwamba Filipo ambaye alikuwa ameachwa Antiokia kama mkuu wa serikali, alikuwa ameasi. Mfalme alighadhibika akaanzisha mazungumzo ya amani na Wayahudi, akayakubali masharti yao, na kuahidi kwa kiapo kuwatendea kwa haki Wayahudi, akatoa tambiko, akaonesha heshima kwa hekalu kwa kutoa zawadi kwa ukarimu,
24 na akampokea Yuda Makabayo kwa heshima. Baada ya hapo, mfalme akamteua Hegemonide awe mkuu wa nchi yote kati ya miji ya Tolemai na Gerari,
25 halafu yeye mwenyewe akaenda zake Tolemai. Watu wa Tolemai walikuwa wamekasirika sana juu ya mkataba huo wakataka ufutiliwe mbali.
26 Lakini Lisia akatoa hotuba ya hadhara, akautetea mkataba huo kwa ufasaha wake wote, akafaulu kuwatuliza watu na kupata kibali chao. Kisha akarejea Antiokia. Hivyo ndivyo uvamizi wa mfalme Antioko na kurudi nyuma kwake kulivyokuwa.

Generic placeholder image