15

Mpango wa kikatili wa Nikanori
1 Nikanori aliposikia kwamba Yuda na watu wake walikuwa sehemu za Samaria, alifanya mpango kuwashambulia siku ya Sabato, wakati ambapo walikuwa wamepumzika.
2 Wayahudi waliokuwa wameshurutishwa kumfuata walimwomba asifanye ukatili na unyama kama huo, bali aiheshimu siku hiyo ambayo Mungu aonaye yote alikuwa ameiheshimu na kuifanya takatifu kuliko siku nyingine zote.
3 Ndipo Nikanori, mlaaniwa mkuu, alipouliza kama eti kulikuwa na mfalme mbinguni aliyekuwa amewaamuru wao kuiheshimu Sabato.
4 Wayahudi wakajibu: “Ndiyo, yuko; Bwana aishiye, atawalaye mbinguni, alituamuru tuiheshimu Sabato.”
5 Lakini Nikanori akajibu: “Mimi ndiye mtawala duniani, na ninawaamuru kushika silaha zenu na kufanya anachoamuru mfalme.” Hata hivyo, Nikanori hakufaulu kutekeleza mpango wake wa kikatili.

Yuda aandaa askari wake kwa mapambano
6 Katika majivuno yake, Nikanori alikuwa amejigamba eti angejenga mnara wa ukumbusho wa ushindi wake dhidi ya Yuda.
7 Lakini Yuda alikuwa na imani thabiti kwamba Bwana angemsaidia.
8 Hivi akawahimiza watu wake wasiwaogope maadui. Aliwatia moyo kwa kuwataka wakumbuke jinsi Mungu Mwenye Nguvu alivyokuwa amewasaidia siku za nyuma, na akawathibitishia kwamba Mungu angewasaidia pia safari hii.
9 Aliwatia moyo kwa maneno ya sheria na mafundisho ya manabii na kwa kuwakumbusha mapambano mbalimbali waliyokuwa wameshinda, akawafanya wawe na hamu zaidi ya kupiga vita.
10 Watu wake walipokuwa tayari kwa mapigano, aliwapa maagizo yake, akiwaonesha jinsi watu wa mataifa mengine walivyokuwa hawaaminiki, kwa sababu hawakushika mikataba yao.
11 Aliwahimiza wawe hodari, si kwa kutegemea ngao na mikuki, bali kwa maneno ya ujasiri ya kutia moyo. Pia aliwachangamsha wote kwa kuwasimulia ndoto - aina ya maono aliyokuwa amepata, ambayo ilistahili kusadikiwa.
12 Aliwaeleza kwamba alikuwa amemwona katika ndoto Onia yule aliyekuwa zamani kuhani mkuu, mtu mwema na wa ajabu, mnyenyekevu na mpole, mtu aliyekuwa msemaji maarufu na ambaye alikuwa amefundishwa tangu utoto juu ya mambo mema kabisa, amenyosha mikono kuiombea jumuiya yote ya Wayahudi.
13 Kisha, Yuda aliona mtu mwenye nywele nyeupe na wa kupendeza.
14 Onia akasema: “Huyu, Yeremia, ni nabii wa Mungu, nabii ambaye anawapenda Wayahudi wenzake, na hutoa sala nyingi kwa ajili yetu na Yerusalemu, mji mtakatifu.”
15 Hapo Yeremia alinyosha mkono wake wa kulia na kumpa Yuda upanga wa dhahabu, akisema:
16 “Upanga huu wa dhahabu ni zawadi kutoka kwa Mungu. Pokea, ukawaangamizie maadui zako.”
17 Maneno mazuri aliyosema Yuda yalimtia moyo na ushujaa kila mtu, na wavulana walikuwa wametiwa hamu ya kupiga vita kama watu wazima. Mji wao, dini yao, na hekalu lao vilikuwa hatarini. Hivyo, Wayahudi wakaamua wasipoteze muda zaidi, ila wamshambulie adui na kuchunguza uwezekano wa kufaulu kwa mapigano ya ana kwa ana.
18 Hofu yao haikuwa juu ya wake na watoto wao wenyewe na jamaa, ila hasa juu ya hekalu lao takatifu.
19 Na wale waliopaswa kubaki Yerusalemu walipata wasiwasi juu ya mapigano yaliyokuwa yanaendelea nje kwenye uwanja wa mapambano.

Kushindwa na kuuawa kwa Nikanori
20 Kila mmoja alikuwa anangoja kuona nani angeshinda vita hivyo. Askari wa maadui walikuwa wanasonga mbele, wakiandamana na wapandafarasi kulia na kushoto kwao, na tembo wao wamewaweka katika sehemu muhimu.
21 Basi, Yuda Makabayo akaangalia hilo jeshi kubwa la maadui, silaha zao za ainaaina, na tembo wao wakali. Halafu akainua mikono yake kuelekea mbinguni, akamwomba Bwana ambaye hutenda maajabu, maana alijua kwamba Bwana huwapa ushindi wale wanaostahili, si wale ambao wana jeshi lenye nguvu.
22 Basi, akamwomba Mungu hivi: “Bwana, Hezekia alipokuwa mfalme wa Uyahudi, ulimtuma malaika wako, akawaua watu 185,000 wa jeshi la mfalme Senakeribu.
23 Sasa, kwa mara nyingine, ewe Bwana wa mbingu, umtume malaika wako mwema kuwatikisa na kuwatetemesha kwa hofu maadui zetu.
24 Kwa uwezo wako mkuu, uwaangamize watu hawa ambao wamekukufuru wewe, na ambao wamekuja kulishambulia taifa lako teule.” Kwa maneno hayo, Yuda alimaliza sala yake.
25 Nikanori na watu wake walisonga mbele kwa muziki wa tarumbeta na nyimbo za vita,
26 lakini Yuda na watu wake walijitia vitani huku wanamwomba Mungu awasaidie.
27 Kwa mikono yao walipiga vita; kwa mioyo yao walimwomba Mungu; hivi Wayahudi wakawaua maadui zaidi ya 35,000. Shukrani yao haikuwa na kifani kwa msaada huo waliokuwa wamepata kutoka kwa Mungu.
28 Baada ya vita, walipokuwa wanarudi nyumbani huku wanafurahia ushindi wao, wakamwona Nikanori katika uwanja wa mapambano, amekufa, akiwa amevaa silaha zake zote.
29 Ndipo wakapaaza sauti wakishangilia na kumsifu Bwana kwa lugha yao.
30 Yuda Makabayo, ambaye daima alikuwa amepiga vita kwa nguvu zake zote na kwa moyo wake wote kwa ajili ya Wayahudi wenzake, bila kupoteza kamwe wema wake wa ujanani, akawaamuru watu wake kukata kichwa cha Nikanori na mkono wake wa kulia na kupeleka Yerusalemu.
31 Walipowasili mjini Yerusalemu, Yuda aliwakusanya pamoja watu wote, akawaweka makuhani mbele ya madhabahu, na kuagiza waletwe watu waliokuwa ngomeni.
32 Akawaonesha kichwa cha yule mlaaniwa, Nikanori na mkono ambao yule mwovu alikuwa ameunyosha kwa ufidhuli dhidi ya hekalu takatifu la Mungu Mwenye Nguvu.
33 Kisha akaukata ulimi wa yule mkufuru, akiahidi atawatupia ndege wale, na mabaki ya kichwa kuyaning'iniza mkabala na hekalu, yawe ushindi wa mapato ya upumbavu wa Nikanori.
34 Kila mmoja aliinua macho mbinguni, akamsifu Bwana aliyeonesha uwezo wake na kuzuia hekalu lake lisitiwe najisi.
35 Yuda akakining'iniza kichwa cha Nikanori katika ukuta wa ngome, kiwe ushahidi waziwazi kwa kila mmoja kuhusu msaada wa Bwana.
36 Kwa kauli moja iliamuliwa kwamba siku hiyo isisahauliwe kamwe, bali iadhimishwe kila mwaka siku inayotangulia siku ya Mordekai, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili uitwao Adari kwa Kiaramu.

Hatima
37 Hivyo ndivyo mambo yalivyomwendea Nikanori. Toka siku hiyo mji wa Yerusalemu umebaki mikononi mwa taifa la Wayahudi; nami namalizia masimulizi yangu hapa.
38 Kama yameandikwa kwa ufasaha na mpangilio, ninafurahi; lakini kama yameandikwa ovyoovyo na bila kivutio, hivyo ndivyo nilivyoweza.
39 Tunajua kwamba haileti afya kunywa divai au maji peke yake, ambapo divai iliyochanganywa na maji hufanya kinywaji chenye ladha ya kupendeza. Hivi, pia, masimulizi mazuri yakiandikwa kwa ustadi huwafurahisha na kuwaburudisha wasomaji. Na hapa ndio mwisho.

Generic placeholder image