9

Bwana amwadhibu mfalme Antioko
(1Mak 6:1-7; 2Mak 1:11-17)
1 Yapata wakati huo huo, Antioko alikuwa anarudi nyuma na ghasia kutoka Persia,
2 ambako alikuwa ameingia katika mji wa Persepoli na kujaribu kuyaibia mahekalu na kuutwaa mji. Wenyeji wa huko walishika silaha na kumshambulia Antioko. Jeshi lake likalazimika kurudi nyuma kwa aibu.
3 Antioko alipofika Ekbatana, alijulishwa yaliyokuwa yamempata Nikanori na askari wa Timotheo.
4 Aliwaka hasira na kuamua kuwalipa Wayahudi kisasi kwa kupigwa na kushindwa kwake. Hivi akamwamuru dereva wa gari lake akaze mwendo bila kusimama mpaka amalize safari yake. Na kwa kiburi chake akasema: “Nitakapofika huko nitaugeuza mji wa Yerusalemu kuwa kaburi la Wayahudi.” Lakini hakujua kwamba hukumu ya Mungu ilikuwa inaandamana naye.
5 Basi, Mungu wa Israeli, aonaye yote akampiga pigo lisiloponyeka na lisiloonekana. Naam! Mara tu alipokwisha kusema akapatwa na maumivu makali ya tumbo yasiyotulizika -
6 ndiyo adhabu ya kufaa kwa mtu aliyekuwa amewaumiza wengine kwa mateso mengi ya kutisha!
7 Hata hivyo, hakuacha majivuno yake. Kiburi chake kikaongezeka. Huku anawaka kwa hasira na kutoa vitisho dhidi ya Wayahudi, alimwamuru dereva wake kwenda kasi zaidi. Katika mbio hizo Antioko alitupwa kutoka garini, akaanguka kwa kishindo na kuumia vibaya sana katika kila kiungo cha mwili wake.
8 Kiburi chake kilimfanya afikiri kwamba alikuwa na nguvu na uwezo wa kuyafanya mawimbi ya bahari yamtii, na wa kuipima uzito milima mirefu juu ya mizani. Kumbe kwa ghafla akaanguka chini na kuchukuliwa machela; na hivyo kufanya uwezo wa Mungu udhihirike kwa wote.
9 Mwili wa mtu huyu asiyemjali Mungu ukajaa wadudu, na alipokuwa bado hai na katika maumivu makali na uchungu mwingi, nyama yake ikaanza kuoza. Harufu aliyotoa ilikuwa mbaya hata askari wote wa jeshi lake wakaona kinyaa.
10 Hapana hata mmoja aliyeweza kumsogelea na kumchukua kumpeleka popote. Kumbe muda mfupi tu kabla yake, huyu alidhani anaweza kuzikamata nyota za mbinguni!

Antioko aweka ahadi kwa Mungu
(1Mak 6:8-17)
11 Hapo kiburi chake kikaanza kupungua, akapondeka moyo. Mapigo ya Mungu yalimfanya apate akili na maumivu yake yakampata wakati wote.
12 Kisha, aliposhindwa kabisa kuvumilia mnuko wake mwenyewe, akasema: “Ni haki binadamu ajiweke chini ya Mungu; mtu kiumbe asijidai kuwa sawa naye.”
13 Kisha huyo mtu wa kuchukiza akamwahidi hivi Bwana ambaye hakuwa na huruma kwake tena:
14 “Ule mji mtakatifu niliotaka kuubomoa na kuufanya kaburi lililojaa Wayahudi, sasa natangaza kwamba ni mji huru. 15Wayahudi ambao sikuwaona wastahili maiti zao kuzikwa ila nilipanga maiti zao na za watoto wao watupiwe wanyama wa pori na ndege sasa nakusudia kuwafanya wote wenye haki sawasawa kabisa na raia wa Athene.
16 Na lile hekalu nililolipora hapo awali nitalipamba kwa zawadi nzuri, na vyombo vyake vitakatifu nitavirudisha na kuongeza vingi zaidi; tena nitalipa gharama za tambiko kutoka mfukoni mwangu.
17 Zaidi ya hayo yote, mimi mwenyewe nitakuwa Myahudi, na nitakwenda kila waliko watu na kuwatangazia uwezo wa Mungu.”

Barua ya Antioko kwa Wayahudi
18 Lakini maumivu ya Antioko yalipoendelea bila kupungua kwa namna yoyote kwa vile hukumu ya Mungu ilikuwa imemkumba kwa haki, alikata tamaa kabisa. Basi, akaandika barua ifuatayo kwa Wayahudi, nayo ilikuwa ya mtindo wa maombi:
19 “Mimi mfalme Antioko kwa Wayahudi, raia wangu wastahifu. Salamu za upendo, matashi mema, afya njema na ufanisi kwenu.
20 “Ni furaha yangu kama nyinyi na watoto wenu mu wazima na mambo yenu yanaendelea vizuri. Tumaini langu ni kwa Mungu,
21 na ninakumbuka kwa furaha kubwa heshima na wema mlionifanyia. “Nilipokuwa narejea nyumbani kutoka Persia nilipatwa na ugonjwa mkali sana, na hivi niliona inafaa kuanza kufanya mipango ya ustawi kwa jumuiya yote.
22 Bado sijakata matumaini ya kupona; kwa kweli nina imani kabisa ya kwamba nitapona.
23 Lakini nakumbuka baba yangu alikuwa na kawaida ya kumteua mwandamizi wake kila alipokwenda vitani katika nchi za nyanda za juu.
24 Alifanya hivyo ili, kama mambo yakitokea isivyotazamiwa, au ripoti mbaya ikiletwa, raia wake wasiingiwe na hofu, maana walijua nani ameachiwa madaraka.
25 Aidha, ninajua jinsi watawala wa nchi zinazopakana na ufalme wangu wanavyosubiri wakati wa kufaa na kungojea yatakayotukia. Kwa sababu hiyo nimemteua mwanangu Antioko kuwa mfalme baada yangu. Mara nyingi nimemwacha mikononi mwenu na kuwatakeni mwelewane naye nilipokuwa nakwenda kufanya ziara katika mikoa ya nyanda za juu. Yeye anapata nakala ya barua hii.
26 “Sasa ninawasihi sana kila mmoja wenu azikumbuke fadhili za hadhara na faragha nilizowatendeeni, mpate kuendelea na nia yenu njema kwangu na kwa mwanangu.
27 Nina imani kwamba atawatendeeni kwa haki na wema, kama mimi nilivyokuwa nimewatendeeni kila mara.”
28 Na hivyo, huyu mwuaji aliyekuwa amemkufuru Mungu, alipata maumivu makali sana, kama yale aliyokuwa amesababisha kwa wengine, akafa kifo cha kutisha mno huko milimani, katika nchi ya kigeni.
29 Filipo mmoja wa rafiki zake wakubwa, alipeleka maiti ya Antioko nyumbani; lakini kwa kuwa alimwogopa mwana wa Antioko, akaenda zake Misri kwa mfalme Tolemai Filometori.

Generic placeholder image