3

Ubishi kati ya Onia na Simoni
1 Wakati Onia alipokuwa kuhani mkuu, mji mtakatifu ulikuwa na amani na ustawi, na sheria zilishikwa kiaminifu kabisa, kwa sababu Onia alikuwa mcha Mungu na alichukia maovu.
2 Wafalme waliliheshimu hekalu, wakalitunukia zawadi za thamani.
3 Na mfalme Seleuko, mtawala wa Asia yote, alikuwa analipia gharama za matoleo ya tambiko hekaluni kutoka katika hazina yake mwenyewe.
4 Lakini Simoni, mtu mmoja wa kabila la Benyamini, aliyekuwa ofisa mkuu wa shughuli za hekalu, alikuwa na mzozo na Onia kuhusu utaratibu wa soko la mji.
5 Wakati huo Apolonio wa Tarso alikuwa mkuu wa Siria Kuu. Basi, Simoni akamwendea Apolonio,
6 akamwambia kwamba hazina ya hekalu ilikuwa na fedha nyingi hivi hata haikuwezekana kuihesabu; na kwamba kwa vile fedha hiyo haikuhitajika kwa ajili ya tambiko, ingeweza pia kuwekwa mikononi mwa mfalme.

Heliodoro atumwa Yerusalemu
7 Apolonio alipokutana na mfalme, alimweleza habari ya fedha hiyo, naye mfalme akaamuru Heliodoro, waziri wake mkuu, akaichukue na kumletea fedha hiyo.
8 Heliodoro aliondoka mara kwenda alikotumwa, lakini alifanya kana kwamba alikuwa anafanya ziara ya kukagua miji ya Siria Kuu.
9 Alipowasili Yerusalemu na kukaribishwa vizuri sana na kuhani mkuu, alieleza madhumuni halisi ya safari yake, na akauliza kama yale aliyokuwa ameambiwa yalikuwa kweli.
10 Kuhani mkuu alimweleza kwamba palikuwa na fedha fulani iliyowekwa katika hazina ya hekalu, lakini kiasi fulani ilikuwa kwa ajili ya wajane na yatima,
11 na kiasi kingine kilikuwa mali ya Hirkano mwana wa Tobia, mtu maarufu sana. Pia alibainisha kwamba kiasi cha fedha hiyo kilikuwa kilo 13,000 tu, na dhahabu ilikuwa kilo 6,500.
12 Aliongeza kusema kwamba ilikuwa haiwezekani kabisa kuwadhulumu watu walioweka tumaini lao kwa utakatifu na usalama wa hekalu lililosifika duniani kote.

Heliodoro apanga kuingia hekaluni
13 Lakini Heliodoro alisisitiza kwamba fedha hiyo lazima ichukuliwe kwa ajili ya hazina ya mfalme, kama mfalme alivyokuwa ameamuru.
14 Hivi akapanga siku ya kwenda hekaluni kusimamia hesabu ya fedha hiyo. Kitendo hicho kilisababisha ghasia kubwa mji mzima.
15 Makuhani, wakiwa wamevalia mavazi yao ya kikuhani, walianguka kifudifudi mbele ya madhabahu, wakamwomba Mungu ailinde fedha hiyo, kwa vile alikuwa ametoa sheria kulinda fedha waliyoweka watu hekaluni.
16 Kila aliyemtazama kuhani mkuu alichomwa moyoni. Uso wake ulibadilika rangi, uchungu wa roho yake ukadhihirika nje.
17 Kiwiliwili chake kilikuwa kinatetemeka kwa hofu, huzuni yake ya moyoni haikufichika.
18 Watu walitoka mbio majumbani mwao, wakaenda kujiunga na makuhani katika sala kusudi hekalu lisitiwe unajisi.
19 Wanawake nao, hali wamejifunga gunia kifuani, walifurika mitaani. Wanawali, ambao wazazi wao hawakuwa wamewaruhusu kutoka ndani, walikimbilia kwenye milango au kuta za mji, na wengine wakabaki wanachungulia madirishani.
20 Hao wote, kila walipokuwa, waliinua mikono yao kwa Mungu, wakisali.
21 Ama hakika ilisikitisha kumwona kuhani mkuu katika kuvunjika moyo na maumivu makali kama hayo, na kuwaona watu wote mjini wamechanganyikiwa na kulala kifudifudi vumbini.

Bwana alilinda hekalu lake
22 Wakati walipokuwa wanamwomba Bwana Mwenye Nguvu ailinde salama fedha hiyo iliyokuwa imewekwa chini ya ulinzi wake,
23 Heliodoro aliamua kuendelea na mpango wake.
24 Lakini mara tu yeye na walinzi wake walipofika penye hazina, Bwana wa roho zote na mamlaka yote akaleta tukio la ajabu hivi kwamba kila mmoja aliyekuwa amethubutu kuingia na Heliodoro alipigwa na fadhaa na kuishiwa nguvu mwilini kwa hofu.
25 Katika tukio hilo waliona farasi na mpandaji wake. Farasi alikuwa na matandiko ya fahari, na mpandafarasi alikuwa anatisha. Ghafla, huyo farasi alimkabili Heliodoro na kumshambulia kwa miguu yake ya mbele.
26 Pia vijana wawili, wenye nguvu ajabu na uzuri mno wamevalia nguo za fahari, walitokea mbele ya Heliodoro na kusimama mmoja kulia na mmoja kushoto kwake; wakampiga Heliodoro mapigo mengi.
27 Heliodoro akaanguka chini mara na kupoteza fahamu. Watu wake wakamwokota na kumweka katika machela,
28 wakamtoa nje. Dakika chache tu kabla yake mtu huyu aliyekuwa ameingia kwenye hazina na kundi kubwa la watu, wakiwamo walinzi wake wote, lakini sasa alikuwa anaondolewa kwa machela, yu hoi. Basi, watu wote walikiri uwezo mkuu wa Mungu.

Onia amwombea Heliodoro kupona
29 Kutokana na kipigo hicho kutoka kwa Mungu, Heliodoro alibaki amelala taabuni, hawezi kusema wala hana tumaini la kupona.
30 Lakini Wayahudi wakamsifu Bwana aliyetenda kwa namna ya ajabu kwa ajili ya maskani yake. Nalo hekalu ambalo hapo awali lilikuwa na watu wamejaa woga na wasiwasi sasa likawa shangwe na furaha tupu.
31 Baadhi ya marafiki wa Heliodoro, walimwomba Onia, kuhani mkuu, amsihi Mungu Mkuu ili amwepushe na kifo huyo aliyekuwa katika hatari ya kufa.
32 Basi, kuhani mkuu akatoa tambiko kwa matumaini kwamba Mungu angemponya Heliodoro, maana hakutaka mfalme ahisi kwamba Wayahudi ndio waliokuwa wamemtenda hivyo mtu aliyetumwa naye.
33 Onia alipokuwa anatoa tambiko hiyo, wale vijana wawili, wakiwa wamevaa nguo zilezile kama kwanza, wakamtokea tena Heliodoro na kusema: “Umshukuru sana kuhani mkuu; maana kwa ajili yake, Bwana ameyaokoa maisha yako.
34 Kumbuka kwamba Bwana wa mbingu ndiye aliyekuadhibu. Sasa nenda zako, na ukamweleze kila mtu habari juu ya nguvu ya ajabu ya Mungu.” Walipokwisha sema hayo, vijana wakatoweka.

Heliodoro amsifu Mungu
35 Hapo Heliodoro akamtolea Bwana tambiko na kuweka ahadi nyingi, kwa sababu Bwana alikuwa ameokoa maisha yake. Halafu alimwaga Onia, akarudi kwa mfalme pamoja na jeshi lake.
36 Huko akamsimulia kila mtu mambo ambayo Bwana, Mwenye Nguvu alikuwa amefanya.
37 Mfalme alipomwuliza Heliodoro kama nani angefaa zaidi kutumwa Yerusalemu safari nyingine, Heliodoro alijibu:
38 “Kama unaye adui, au kama unamjua mtu anayefanya njama dhidi ya serikali yako, mpeleke huyo. Atarudi amepigwa vibaya sana - kama atajaliwa kurudi - maana kule Yerusalemu uwezo wa ajabu wa Mungu unatenda kazi.
39 Mungu aliye na makao yake mbinguni hulilinda hilo hekalu yeye mwenyewe na kumwangamiza yeyote anayetaka kulidhuru.”
40 Hayo ndiyo matokeo ya kisa cha Heliodoro na hazina iliyolindwa ya hekalu.

Generic placeholder image