6

Wayahudi wadhulumiwa kwa sababu ya imani yao
1 Baada ya muda si mrefu, mfalme alimtuma mzee mmoja Mwathene kuwashurutisha Wayahudi kuachilia mbali dini yao na mila na desturi za wazee wao.
2 Pia aliagizwa kulitia najisi hekalu lao na kuliita “Hekalu la Zeu,” mungu wa Olimpia. Hekalu lililokuwa juu ya mlima Gerizimu ilibidi liitwe rasmi “Hekalu la Zeus, Mungu wa Ukarimu”, kama wakazi wa huko walivyoomba liitwe.
3 Uovu uliofuata ulikuwa mbaya na wa kuchukiza mno.
4 Watu wa mataifa mengine walilijaza hekalu kwa tafrija mbalimbali na kila aina ya ufisadi. Hata makahaba walitembea nao hekaluni. Vitu vilivyokatazwa viliingizwa hekaluni,
5 na madhabahu ilifunikwa na tambiko za kuchukiza zilizokatazwa na sheria yetu.
6 Haikuwezekana kuishika Sabato, wala kuadhimisha sikukuu za jadi, wala hata kujitaja waziwazi kuwa ni Myahudi.
7 Kila mwezi ilipoadhimishwa siku ya kuzaliwa kwa mfalme, Wayahudi walilazimishwa kwa nguvu kula matumbo ya wanyama wa tambiko. Halafu, wakati wa sikukuu ya Dionisio, mungu wa divai, walitakiwa wavae mataji ya majani vichwani na kufanya maandamano.
8 Kwa dokezo la Tolemai, miji ya Kigiriki ya jirani pia iliagizwa kuwataka Wayahudi wale tambiko;
9 na wote ambao wangekataa kuishi kadiri ya utamaduni wa Kigiriki, iliamuriwa wauawe. Haikuwa vigumu kuona kwamba wakati mgumu ulikuwa unakuja.
10 Mathalani, wanawake wawili walishikwa kwa sababu waliwatahiri watoto wao. Walitembezwa kuzunguka mji huku watoto wao wananing'inia kwenye maziwa yao; halafu wakatupwa chini kutoka ukuta wa mji.
11 Tukio jingine. Filipo aliambiwa kwamba Wayahudi kadha walikuwa wamekusanyika katika pango la karibu ili kushika Sabato kwa siri. Filipo akawashambulia na kuwachoma moto wote pamoja. Wao lakini hawakujitetea kwa mabavu, kwa vile waliiheshimu sana Sabato.

Bwana huadhibu na kuhurumia
12 Hapa nawahimiza wasomaji wa makala haya wasivunjike moyo kutokana na misiba ya kutisha iliyotukia. Ieleweke kwamba adhabu hizo zilitolewa na Bwana siyo kuwaangamiza bali kuwapa nidhamu.
13 Kwa kweli, kumwadhibu mtu mpotovu ni ishara ya huruma kubwa, kuliko kumwachilia kwa muda mrefu bila adhabu.
14 Bwana hatutendei sisi kama anavyoyatendea mataifa mengine. Hao wengine huwaadhibu baada ya kungoja kwa uvumilivu mpaka wamezama kabisa dhambini;
15 lakini sisi hutuadhibu kabla hatujatenda dhambi mno.
16 Kwa hiyo, Bwana anatuhurumia daima, sisi watu wake. Ingawa hutuadhibu kwa misiba, kamwe hatutupi.
17 Nimeeleza hayo machache kwa kuwakumbusheni tu. Sasa tuendelee na simulizi letu.

Eleazari afia imani yake
18 Palikuwa na mwalimu mmoja wa sheria aitwaye Eleazari, mtu mzee na mwenye kuheshimiwa sana. Huyo alifunguliwa mdomo wake kwa nguvu kula nyama ya nguruwe.
19 Lakini Eleazari aliona heri kufa kwa heshima kuliko kuishi kwa upotovu. Basi, akatema hiyo nyama na kwenda kwa hiari yake mahali pa kuteswa,
20 akionesha jinsi watu wanavyopaswa kuwa wajasiri kukataa kula chakula najisi, hata kama kufanya hivyo kutawagharimu maisha yao.
21 Watu waliohusika na tambiko hiyo walikuwa wanamjia Eleazari sana, hivyo walimchukua kando, wakamsihi alete nyama yake mwenyewe, iliyo halali kuliwa, ajifanye kana kwamba anakula nyama ya tambiko ambayo mfalme aliamuru itolewe.
22 Kwa kufanya hivyo hangeuawa, na angetendewa vizuri kwa sababu ya urafiki wao wa tangu zamani.
23 Lakini Eleazari akakata shauri lililostahili mtu mzee na umri wake mkubwa. Tangu utoto wake alikuwa ameishi kwa kushika kikamilifu amri takatifu za Mungu. Hivyo akajibu: “Niueni, hapahapa, sasa hivi.
24 Mtu wa umri mkubwa kama wangu, ni aibu kudanganya namna hiyo. Vijana wengi wasije wakafikiri kwamba nimeikana imani yangu baada ya kutimiza umri wa miaka tisini.
25 Kama nitafanya kana kwamba nakula nyama hii, ili tu niendelee kuishi kidogo tena, nitakuwa nimejiletea aibu na fedheha, na vijana wengi watakuwa wamepotoshwa.
26 Hata kama ningeweza kwa sasa kuepuka hilo pigo la watu wafao, sitaweza kuuepa mkono wa Mungu Mwenye Nguvu niwe hai au nimekufa.
27 Kwa kukipokea kifo sasa kwa uhodari, nitadhihirisha kwamba nastahili uzee wangu.
28 Hapo vijana watajifunza kutokana na mfano wangu, jinsi ipasavyo kukubali kwa furaha kufa kwa ajili ya sheria za kale na takatifu za Mungu.” Alipokwisha sema hayo, alipaendea mahali pa kuteswa.
29 Na watu walewale waliokuwa wamemfanyia kirafiki dakika chache kabla yake, sasa walimgeukia, maana walidhani alikuwa ameongea kama mwendawazimu.
30 Walipokuwa wamempiga mpaka karibu na kufa, Eleazari akatoa mlio wa maumivu na kusema: “Bwana ajua yote. Anajua kwamba ningeweza kuwa nimeepuka mateso haya makali na kifo. Pia anajua kwamba nimevumilia hayo kwa furaha, kwa sababu namcha yeye.”
31 Hivyo ndivyo Eleazari alivyokufa. Lakini kifo chake cha ujasiri kilikumbukwa na kuhesabiwa kuwa mfano mtukufu si na vijana tu, bali na taifa lake zima.

Generic placeholder image