14

Alkimo amsengenya Yuda
(1Mak 7:1-21)
1 Miaka mitatu baadaye, Yuda na watu wake walipata habari kwamba Demetrio, mwana wa Seleuko alikuwa ameingia bandarini Tripoli akiwa na jeshi lenye nguvu na msururu wa meli,
2 na kwamba alikuwa amemuua mfalme Antioko na Lisia mlinzi wa mfalme, na kuitwaa nchi.
3 Kulikuwa na mtu mmoja aliyeitwa Alkimo. Kabla yake alikuwa kuhani mkuu, ambaye kwa furaha alikuwa amekubali kuishi kama Wagiriki wakati ule wa maasi. Akitambua kwamba asingeweza tena kamwe kuwa kuhani mkuu, na kwamba alikuwa katika hatari,
4 Alkimo alimwendea mfalme Demetrio, mwaka 151. Kwa nafasi hiyo alimpatia mfalme zawadi hizi: Taji ya dhahabu, tawi la mtende, na matawi ya mizeituni ambayo kijadi yalitolewa kwa hekalu. Lakini hakusema lolote juu ya mipango yake.
5 Hata hivyo, baadaye alipata fursa ya kutekeleza mipango yake ya kipumbavu. Basi, Demetrio alikuwa na mkutano na washauri wake. Akamwita Alkimo mkutanoni na kumwuliza Wayahudi walikuwa wananuia kufanya nini. Ndipo Alkimo akasema:
6 “Wale Wayahudi wanaoitwa Wahasidi, ambao kiongozi wao ni Yuda Makabayo, ndio wanaochochea vita na maasi, hata taifa haliwezi kuwa na amani.
7 Ni kosa lao kwamba mimi sina tena ule wadhifa wa kuhani mkuu, ambao ninastahili kwa kuzaliwa. Na hivi nimekuja hapa,
8 kwanza kabisa kwa sababu ninakujali sana wewe mfalme, na pili kwa sababu nawaonea huruma wananchi wenzangu, maana kutokana na fujo za kijinga za akina Yuda, taifa zima limo taabuni.
9 Basi, nakusihi, ewe mfalme, kuyachunguza kwa makini mambo hayo yote, kisha ufanye chochote kadiri ya hisani yako ya siku zote ili kuondoa huo ukandamizaji na unyanyasaji wa taifa letu na watu wake.
10 Kama Yuda ataendelea kuishi, basi, taifa letu halitakuwa na amani kamwe.”

Demetrio amtuma Nikanori kumshambulia Yuda
11 Alkimo alipomaliza kusema hayo, washauri wengine wa mfalme ambao walimchukia Yuda, wakadakia na kuchochea hasira ya Demetrio.
12 Basi, mfalme Demetrio mara moja akamteua Nikanori aliyekuwa kamanda wa vikosi vya tembo wake, awe mkuu wa Yudea, akamtuma aende huko
13 akamwulie mbali Yuda na kuwatawanya wafuasi wake, na kumfanya Alkimo kuwa kuhani mkuu wa hekalu kuu.
14 Nao watu wote wa mataifa huko Yudea ambao walikuwa wamemkimbia Yuda, walimiminika kujiunga na askari wa Nikanori, wakifikiri kwamba maafa na balaa walizopata Wayahudi, kwao ingekuwa faida.
15 Wayahudi walisikia kwamba Nikanori alikuwa anakuja pamoja na wale watu wa mataifa waliojiunga naye, wakajitia mavumbi kichwani, wakasali kwa Mungu wao aliyekuwa amelichagua taifa lao liwe mali yake milele, na ambaye huwapa ushindi hao watu wake kwa kujionesha kwao.
16 Basi, kwa amri ya kiongozi wao, wakatoka mara moja kwenda kumpiga adui karibu na kijiji cha Adasa.
17 Simoni nduguye Yuda, alikuwa anapigana na Nikanori, lakini alikuwa anazidi kulemewa kwa sababu ya miondoko isiyotazamiwa ya adui.
18 Hata hivyo, Nikanori aliposikia jinsi Yuda na watu wake walivyokuwa wanaipigania nchi yao kwa ushujaa na moyo, akaamua kuacha mapigano na kumaliza hayo matatizo kwa njia nyingine.
19 Hivyo akawatuma Posidonio, Theodoto na Matathia kwenda kufanya mkataba na Wayahudi.
20 Masharti ya mkataba yalishughulikiwa katika vipengee vyake vyote. Na Nikanori alipowafahamisha askari wake, walikubaliana kwa kauli moja.
21 Halafu ilipangwa siku ya viongozi kukutana faraghani. Viti vya heshima vililetwa kutoka kila kambi, vikapangwa.
22 Yuda alikuwa amefanya tahadhari. Aliwaweka askari wenye silaha sehemu muhimu, maadui wasije wakamfanyia jeuri. Lakini hao viongozi wawili walikutana na kuongea vizuri.
23 Nikanori akaendelea kukaa Yerusalemu kwa kitambo baada ya mkutano, na watu waliokuwa wamejiunga naye aliwarudisha kwao.
24 Hao viongozi wawili wakawa marafiki wakubwa, na Nikanori akawa daima ameshikamana na Yuda.
25 Nikanori akamhimiza Yuda aoe na kujipatia watoto. Basi, Yuda akaoa na akaishi maisha matulivu ya kawaida.

Nikanori amgeukia Yuda
26 Alkimo alipoona Nikanori na Yuda wanapatana vizuri, akatwaa nakala ya mkataba ule, akamwendea mfalme Demetrio. Alimwambia mfalme kwamba Nikanori hakuwa mwaminifu kwa serikali, kwa sababu alikuwa amemteua msaliti Yuda ashike utawala baada yake.
27 Mashtaka hayo ya uongo yalimkasirisha sana mfalme. Katika ghadhabu yake, mfalme akamwandikia Nikanori, akimwarifu ya kwamba hakuwa ameridhishwa na ule mkataba, na hivi alimwamuru ampeleke Yuda Makabayo kama mfungwa Antiokia bila kuchelewa.
28 Taarifa hiyo ilipomfikia, Nikanori aliumia sana moyoni, asijue la kufanya, kwa sababu hakutaka kuvunja mkataba na mtu aliyekuwa ameshika masharti yote kwa upande wake.
29 Lakini kwa vile haikuwezekana kupinga amri ya mfalme, akaanza kutafuta jinsi ya kumnasa Yuda.
30 Yuda Makabayo, alipotambua kwamba Nikanori alianza kuwa na tahadhari katika uhusiano wao na kwamba alikutana naye kwa ukali kuliko alivyokuwa hapo mbele, akajua kuwa kuna kasoro fulani. Basi, akakusanya idadi kubwa ya wafuasi wake, akaenda kujificha.
31 Nikanori alipogundua kwamba Yuda alikuwa amemshinda kwa werevu, akaenda kwenye hekalu kuu na takatifu wakati makuhani wanatolea tambiko, akawaamuru wamlete Yuda kwake.
32 Lakini makuhani wakasema kwa kiapo ya kwamba hawakujua Yuda alikuwa amejificha wapi.
33 Ndipo Nikanori akanyosha mkono wake wa kulia kuelekea hekalu, akaapa: “Msipomtoa Yuda na kumkabidhi kwangu kama mfungwa, nitalibomoa na kulipondaponda hili hekalu la Mungu; nitaivunjilia mbali hii madhabahu, na kujenga mahali hapahapa hekalu tukufu la Dionisio.”
34 Kisha, akaondoka, na mara wale makuhani wakainua mikono kuelekea mbinguni, wakasali kwa Mungu, Mlinzi mwaminifu wa taifa letu:
35 “Bwana wa watu wote, ingawa wewe huhitaji chochote, ilikupendeza kuliweka hekalu lako hapa, na kukaa miongoni mwetu.
36 Kwa hiyo ewe Mtakatifu, Bwana wa utakatifu wote, ulilinde milele hili hekalu ambalo limetakaswa tu hivi punde, lisitiwe najisi tena.”

Razi afa kwa ajili ya nchi yake
37 Mmoja wa viongozi wa Yerusalemu, mtu aliyeitwa Razi, alishtakiwa kwa Nikanori. Ilisemwa kwamba Razi alikuwa amewasaidia watu wake kwa namna nyingi, na kwamba watu walimheshimu hivi hata wakawa wanamwita “Baba wa Wayahudi.”
38 Siku za mwanzo za mapinduzi alikuwa amejitoa mhanga maisha yake kwa ajili ya dini ya Kiyahudi, na alikuwa ameshtakiwa kwa sababu hiyo.
39 Ili kuonesha wazi jinsi alivyowachukia Wayahudi, Nikanori alituma askari zaidi ya 500 kwenda kumkamata Razi,
40 maana alifikiri kukamatwa kwake kungekuwa pigo kubwa kwa Wayahudi.
41 Askari walivunja mlango wa nje, wakawa tayari kuuteka mnara. Wakaagiza moto uletwe, na milango kuchomwa. Razi alijikuta amezungukwa na maadui, akajaribu kujiua kwa upanga wake;
42 aliona afadhali kufa na heshima, kuliko kukamatwa na wenye dhambi na kupata dharau isiyostahili hadhi yake ya kuzaliwa.
43 Katika kuzidiwa na mambo, Razi alikuwa hajajichoma sawasawa upanga wake, na hivi hakuwa amekufa. Basi, askari walipokuwa wanafurika kuingia ndani, Razi akafyatuka mbio na kuruka ukuta, akajitupa kwa ushujaa, juu ya kundi la watu.
44 Haraka watu wakarudi nyuma, na Razi akaangukia pakavu.
45 Akiwa bado hai, na anawaka kwa hasira, Razi aliinuka, na huku damu zinabubujika kutoka majeraha yake, akakimbia katikati ya msongamano wa watu, akapanda juu ya mwamba mrefu na kusimama.
46 Hapo, akiwa hana tone la damu mwilini, alirarua matumbo yake kwa mikono miwili, akawatupia hao watu, huku anasali kumwomba Bwana wa uhai amrudishie matumbo hayo. Hivyo ndivyo alivyokufa.

Generic placeholder image