7

Mama na wanawe waifia imani yao
1 Wakati mmoja mama wa Kiyahudi na wanawe saba walishikwa. Mfalme alitoa amri wapigwe fimbo na mijeledi mpaka wale nyama ya nguruwe.
2 Ndipo mmoja wa vijana hao akasema: “Hivi mnatazamia kupata nini kwa haya mnayofanya? Sisi tupo tayari kufa kuliko kuachana na mila na desturi za wazee wetu.”
3 Maneno hayo yalimwudhi sana mfalme hata akaamuru yapashwe moto masufuria na makaango;
4 nayo yalipokuwa yamekolea moto, mfalme akaamuru yule kijana aliyekuwa msemaji wao akatwe ulimi na kuchunwa ngozi ya kichwani na wamkate mikono na miguu yake wakati mama yake na nduguze sita wanaangalia.
5 Kijana alikatwakatwa, akabaki fungu la nyama inayopumua. Hapo mfalme akatoa amri kijana huyo achukuliwe na kutumbukizwa katika kikaango kimojawapo. Wakati wingu la moshi linatoka katika kile kikaango, ndugu wale sita na mama yao walitiana moyo wafe kijasiri, wakisema:
6 “Bwana Mungu anaangalia hayo, na anaelewa mateso yetu. Mose aliliweka hilo wazi alipoandika wimbo kuwalaumu na kuwalaani wale waliokuwa wamemtupa Bwana. Alisema, ‘Bwana atawahurumia wale wanaomtumikia yeye.’”
7 Baada ya kuuawa yule ndugu wa kwanza namna ile, askari walianza kujifurahisha kwa kumnyofoa nywele na kumchuna ngozi ya kichwani ndugu wa pili. Kisha wakamwuliza: “Je, utakula sasa nyama hii ya nguruwe, au unataka tukukate mikono na miguu?”
8 Kijana akajibu kwa lugha yake: “Sitaila kamwe!” Basi, askari wakamtesa kama walivyomtesa yule wa kwanza,
9 lakini huyu alipokuwa anatoa pumzi ya mwisho alimzomea mfalme, akisema: “Muuaji wewe! Unaweza kutuua, lakini Mfalme wa ulimwengu atatufufua kutoka kwa wafu na kutupatia uhai wa milele, kwa sababu tumezitii sheria zake.”
10 Baada ya huyo, askari wakaanza kujifurahisha na ndugu wa tatu. Aliamuriwa atoe ulimi nje, akautoa mara. Halafu akainyosha mikono yake kwa ujasiri,
11 akisema kwa ushupavu: “Mungu alinipa mikono hii. Lakini sheria za Mungu zina maana zaidi kwangu kuliko mikono yangu, na ninajua Mungu atanirudishia mikono hii.”
12 Mfalme na wale waliokuwa pamoja naye walishangazwa na ushupavu huo wa kijana na jinsi alivyokuwa tayari kuteseka.
13 Baada ya kuuawa, askari wakamtesa kijana wa nne kwa ukatili wa aina hiyohiyo,
14 lakini maneno yake ya mwisho yalikuwa: “Ninayo furaha kuuawa mikononi mwako, kwa sababu tuna hakika kwamba Mungu atatufufua kutoka kwa wafu. Lakini wewe, Antioko, hutafufuliwa!”
15 Askari walimshika kijana wa tano, wakaanza kumtesa.
16 Kijana alimkazia macho mfalme usoni na kumwambia: “Unao uwezo wa kutufanya chochote utakacho, ingawa hata wewe utakufa. Lakini usifikiri kwamba Mungu amewatupa watu wetu.
17 Ngoja tu. Mungu atatumia uwezo wake mkuu kukutesa wewe na wazawa wako.”
18 Halafu askari walimtwaa kijana wa sita. Kabla tu hajafa, akasema: “Usidanganyike. Sisi tunateswa hivi kwa sababu tumetenda dhambi dhidi ya Mungu wetu. Ndiyo maana maovu haya yote yanatupata.
19 Lakini usifikiri kwamba hutaadhibiwa kwa kumpiga vita Mungu.”
20 Mama yao alishangaza zaidi kuliko wanawe wote, na anastahili kukumbukwa kwa namna ya pekee. Ingawa alishuhudia watoto wake saba wakiuawa kwa siku moja, alivumilia kwa ushujaa mkuu kwa sababu alimtumainia Bwana.
21 Kwa uthabiti aliimarisha tabia yake ya kike kwa ushupavu wa kiume, akawatia moyo wanawe kwa lugha ya kwao, kila mmoja kwa zamu yake,
22 kama hivi: “Sijui jinsi wewe ulivyoanza kuwa hai tumboni mwangu. Si mimi niliyekupa wewe uhai na pumzi na kuunganisha viungo vya mwili wako.
23 Mungu ndiye aliyefanya hayo; Mungu aliyeumba ulimwengu, binadamu, na vyote vilivyoko. Ni mwenye huruma, na hivi atakurudishia uhai na pumzi yako, kwa sababu unazipenda sheria zake zaidi kuliko unavyojipenda mwenyewe.”
24 Antioko alijua kwa hakika kwamba yule mama alikuwa anamdhihaki yeye; hivi akajaribu sana kumshawishi mwanawe wa mwisho, ambaye alikuwa bado hai, aachilie mbali jadi za wazee wake. Alimwahidia kijana kwa kiapo kumpa mali nyingi na hali njema, na kumpa wadhifa wenye mamlaka, na kumfanya rafiki yake.
25 Lakini kijana hakutia maanani maneno hayo. Ndipo Antioko akajaribu kumshawishi mama yake kijana aongee na mwanawe ili kuokoa maisha yake.
26 Baada ya kubembelezwa sana, mama alikubali.
27 Akiwa amemwinamia mwanawe, mama akampuuza yule mfalme katili akisema kwa lugha yake: “Mwanangu, unionee huruma. Kumbuka kwamba nilikuchukua mimba miezi tisa, na nikakulea kwa miaka mitatu. Nimekutunza na kukupatia mahitaji yako yote mpaka siku ya leo.
28 Hivi nakusihi, mtoto wangu, uzitazamae mbingu na dunia. Chunguza kwa makini kila ukionacho huko, na utambue kwamba Mungu alivifanya hivyo vyote bila kutumia kitu kingine chochote, kama vile alivyowaumba binadamu.
29 Usimwogope mwuaji huyu. Kubali kufa kwa hiari yako na kuonesha kuwa u mstahifu kama ndugu zako, ili kwa huruma ya Mungu nikupokee tena pamoja nao siku ya ufufuo.”
30 Kabla mama hajamaliza kuongea hayo, kijana akasema: “Mfalme Antioko, unangoja nini? Nakataa kuzitii amri zako. Ninachotii mimi ni amri zile tu zilizo katika Sheria ambayo Mose aliwapa wazee wetu.
31 Umebuni kila namna ya ukatili wa kuwafanyia watu wetu, lakini hutaepa kamwe adhabu ambayo Mungu amekuwekea.
32 Ni kweli, tunateseka kwa sababu ya dhambi zetu.
33 Mungu wetu aliye hai ametukasirikia, na anatusahihisha ili tuwe na nidhamu. Lakini hayo yatadumu kwa muda mfupi tu, kwa vile sisi bado ni watumishi wake; hivi atatusamehe.
34 Ila wewe ni mtu katili na mwovu kuliko viumbe vyote. Hivi usijidanganye kwa kudhani eti utakuwa mkuu, na huku unawaadhibu watu wa Mungu.
35 Huna jinsi ya kuepa adhabu atakayotoa Mungu Mwenye Nguvu aonaye yote.
36 Kaka zangu waliteseka kwa muda mfupi kwa sababu ya uaminifu wetu kwa agano la Mungu, lakini sasa wamepata uhai wa milele. Ila wewe utahukumiwa na Mungu na kuadhibiwa kama unavyostahili kwa kiburi chako.
37 Sasa ninatoa mwili wangu na uhai wangu kwa ajili ya sheria za wazee wetu, kama ndugu zangu walivyofanya. Lakini pia namwomba Mungu awahurumie mara watu wake, na akutese wewe vikali mpaka ulazimike kukiri kwamba yeye peke yake ni Mungu.
38 Mimi na ndugu zangu naomba tuwe wa mwisho kupatwa na pigo la hasira ya Mwenyezi-Mungu, ambalo kwa haki kabisa limeliadhibu taifa letu zima.”
39 Maneno hayo ya dhihaka yalimwudhi Antioko hivi hata akaamuru kijana ateswe kwa ukatili zaidi kuliko ndugu zake.
40 Na hivi kijana akafa, akiwa amemtumaini Mungu kabisa, bila kupoteza uaminifu hata kwa nukta moja.
41 Hatimaye mama yao naye akauawa.
42 Naona nimesimulia vya kutosha kuhusu Wayahudi walivyoteswa na kulazimishwa kula matumbo ya wanyama wa tambiko.

Generic placeholder image