11

Yuda Makabayo amshinda Lisia
(1Mak 4:26-35)
1 Mara baada ya hayo, si muda mrefu baada ya Timotheo kushindwa, Lisia, mlinzi na ndugu ya mfalme na mkuu wa serikali, alipata habari hizo. Alikasirika sana,
2 akaongoza askari wa miguu 80,000 na wapandafarasi wake wote dhidi ya Wayahudi. Alikuwa na shabaha ya kuufanya mji wa Yerusalemu makao ya Wagiriki,
3 na kulitoza kodi hekalu, kama mahali pengine pote pa ibada ya watu wa mataifa mengine. Na ukuhani mkuu ungenadiwa kila mwaka.
4 Lisia hakujali chochote juu ya uwezo wa Mungu, bali alijivunia makumi elfu ya askari wake wa miguu, maelfu ya wapandafarasi wake, na tembo wake themanini.
5 Hivi akaivamia Yudea na kuishambulia ngome ya Beth-zuri, yapata kilomita thelathini kusini ya Yerusalemu.
6 Yuda Makabayo na watu wake waliposikia kwamba Lisia alikuwa anazizingira ngome zao, wakalia na kuomboleza pamoja na watu wote, wakimsihi Bwana amtume malaika mwema awaokoe.
7 Yuda Makabayo alikuwa wa kwanza kuchukua silaha, akawahimiza wengine wajiunge naye katika kutoa mhanga maisha yao ili kuwasaidia Wayahudi wenzao. Hivi, wakatoka pamoja naye kwa ari na motomoto kabisa.
8 Lakini, kabla hawajaenda mbali na Yerusalemu, kwa ghafla wakagundua kwamba walikuwa wanaongozwa na mpandafarasi mwenye mavazi meupe, amechukua silaha za dhahabu.
9 Mara, wote kwa pamoja, wakamshukuru Mungu kwa huruma yake; alikuwa amewatia ujasiri wa kutosha kwa kushambulia si binadamu tu, bali pia wanyama wakali na hata kuta za chuma.
10 Basi, wakaenda mbele wamejipanga kivita, wakiwa pamoja na yule msaidizi kutoka mbinguni, maana Bwana alikuwa amewaonea huruma.
11 Kama simba, waliwarukia maadui zao na kuwaangusha askari wa miguu 11,000, na wapandafarasi 1,600, na kuwafanya wengine wakimbie.
12 Wengi wa hao waliokimbia walikuwa wamejeruhiwa na kupoteza silaha zao. Hata Lisia mwenyewe alikimbia kwa aibu.

Lisia apatana na Wayahudi
(1Mak 6:56-61)
13 Lisia, kwa vile hakuwa mjinga, alitafakari juu ya kushindwa kwake vitani, akatambua kwamba Wayahudi walikuwa hawashindiki kwa sababu Mungu Mwenye Nguvu alikuwa amewapigania. Kwa hiyo akapeleka ujumbe,
14 akawashawishi wakubali kupatana kwa masharti ya haki, na akaahidi kumshawishi mfalme awe rafiki wao.
15 Kwa manufaa ya watu wake, Yuda Makabayo akayakubali mapendekezo yote ya Lisia, kwa vile mfalme alikuwa ameyapokea na kuyakubalia maombi yote ambayo Yuda alikuwa amempa Lisia kwa maandishi.

Barua ya Lisia kwa Wayahudi
16 Ifuatayo ni barua ambayo Lisia aliwaandikia Wayahudi: “Mimi Lisia kwa taifa la Wayahudi, salamu.
17 Wajumbe wenu, Yohane na Absalomu, wamenikabidhi hati maalumu ambayo mliwatuma waniletee, na wameniomba nikubaliane na yaliyoandikwa katika hati hiyo.
18 Nimemwarifu mfalme kuhusu masuala yote ambayo mlitaka kuweka mbele yake, naye amekubali kufanya lolote linalowezekana.
19 Kama mtaendelea kuwa waaminifu kwa serikali, nitafanya kila niwezalo siku za mbele, kwa manufaa ya taifa lenu.
20 Nimewaagiza wajumbe wenu na wawakilishi wangu kukutana nanyi na kujadiliana mambo hayo katika vipengele vyake vyote.
21 Nawatakieni kila la fanaka. Imeandikwa siku ya ishirini na nne ya mwezi Dioskorinthio, mwaka 148.”

Barua ya mfalme kwa Lisia
22 Na barua ya mfalme ilikuwa kama ifuatavyo: “Mimi mfalme Antioko kwa ndugu yangu Lisia, salamu.
23 Kwa kuwa baba yangu amekwenda kujiunga na miungu, nataka raia wa ufalme wangu kuendesha mambo yao wenyewe bila kuingiliwa.
24 Naelewa kwamba Wayahudi hawataki kuishi kadiri ya utamaduni wa Kigiriki - kama baba yangu alivyokuwa amenuia - ila wanapendelea kuishi kadiri ya utamaduni wao, na wameomba waruhusiwe kuishi hivyo.
25 Kwa vile natamani waishi bila wasiwasi kama mataifa mengine katika milki yangu, sasa natoa amri kwamba warudishiwe hekalu lao, na kuruhusiwa kuishi kadiri ya mila za wazee wao.
26 Basi, itakuwa vema kuwajulisha juu ya uamuzi huu, na kuwahakikishia kwamba nitakuwa rafiki kwao, ili waweze kuendesha mambo yao wenyewe kwa amani, bila wasiwasi wowote.”
27 Ifuatayo ni barua ya mfalme kwa taifa la Wayahudi: “Mimi mfalme Antioko kwa Baraza Kuu la Wayahudi na Wayahudi wengine wote, salamu.
28 Natumaini mambo yenu yote yanawaendea vizuri kama ninavyotamani. Mimi ni mzima wa afya.
29 Menelao ameniarifu kwamba mnataka kurudi nyumbani na kushughulika na mambo yenu wenyewe.
30 Kwa hiyo, basi, baadhi yenu watakaorudi nyumbani ifikapo tarehe kumi na tatu ya mwezi Ksanthiko, ninawaapia, wasiogope chochote.
31 Mnaweza kuendelea kushika sheria zenu kuhusu vyakula, na nyinginezo, kama mlivyokuwa mmezoea. Na hapana Myahudi atakayenyanyaswa kwa mambo yaliyofanyika bila kujua.
32 Ninamtuma Menelao kuwatieni moyo.
33 Tunawatakieni fanaka. Imeandikwa siku ya kumi na tano ya mwezi Ksanthiko, mwaka 148.”

Barua ya Waroma kwa Wayahudi
34 Waroma nao waliwaandikia Wayahudi barua ifuatayo: “Kwinto Memio na Tito Manio, wawakilishi wa Waroma, kwa Wayahudi, salamu.
35 Sisi tunakubaliana kabisa masharti yote mliyopewa na Lisia, nduguye mfalme.
36 Sasa tumo njiani kwenda Antiokia; kwa hiyo, yachunguzeni kwa makini masuala yale ambayo Lisia alimwuliza mfalme. Halafu tuleteeni majibu haraka kusudi tuweze kuwawakilisheni kwa mfalme, kwa manufaa yenu. Fanyeni hilo mapema iwezekanavyo,
37 bila kukawia, ili tuweze kujua mmeamua nini. 38Tunawatakieni fanaka. Imeandikwa siku ya kumi na tano ya mwezi Ksanthiko, mwaka 148.”

Generic placeholder image