8

Maasi ya Yuda Makabayo
(1Mak 3:1-26)
1 Yuda ambaye aliitwa pia Makabayo na rafiki zake walikwenda kwa siri vijijini ambako walikusanya jeshi la wanaume wa Kiyahudi wapatao 6,000, ambao walikuwa wanashikilia bado dini ya Kiyahudi.
2 Walimwomba Bwana awasaidie watu wake waliokuwa wameonewa na mataifa yote; alionee huruma hekalu lililokuwa limetiwa unajisi na watu wasio na dini,
3 na auhurumie mji wa Yerusalemu unaoharibiwa na karibu ubomolewe. Walimwomba asikilize damu iliyomwagwa inayomlilia
4 akumbuke maangamizi mabaya ya watoto wasio na hatia na kufuru zinazofanywa dhidi ya jina lake, aoneshe chuki yake juu ya uovu.
5 Mara Yuda Makabayo alipokamilisha kuunda jeshi lake, watu wa mataifa mengine hawakuweza kushindana naye kwa sababu hasira ya Bwana dhidi ya Israeli sasa iligeuka kuwa huruma.
6 Bila kutazamiwa, Yuda alishambulia miji na vijiji, akavichoma moto. Alikamata sehemu muhimu, na maadui wengi akawakimbiza.
7 Saa za usiku zilimfaa zaidi kwa mashambulio hayo. Na kila mahali watu walikuwa wanazungumzia ushujaa wake.

Tolemai amtuma Nikanori kumshambulia Yuda
(1Mak 3:38-41)
8 Filipo, alipotambua kwamba Yuda alikuwa anaendelea kupata ushindi na kwamba alikuwa anasonga mbele na kufanikiwa mara nyingi, alimwandikia barua Tolemai, mkuu wa Siria Kuu na Foinike aje kumsaidia mfalme.
9 Bila kukawia, Tolemai akamteua Nikanori mwana wa Patroklo, mmoja wa marafiki wa mfalme, akamtuma pamoja na askari zaidi ya 20,000 wa mataifa mbalimbali kwenda kufutilia mbali taifa la Wayahudi. Tolemai pia alimteua Gorgia, jenerali mwenye uzoefu mwingi wa mambo ya vita, aende pamoja naye.
10 Basi, Nikanori akaamua kuchukua fursa hiyo kwa niaba ya mfalme kulipa deni la fedha talanta 2,000 za kodi kwa Waroma, kwa kuwauza utumwani Wayahudi waliotekwa.
11 Kwa hiyo, mara moja akapeleka taarifa kwa miji ya pwani kwamba atakuwa anauza Wayahudi kwa bei nafuu: Watumwa tisini kwa fedha talanta moja, bila kujua kwamba hukumu ya Mungu Mwenye Nguvu ilikuwa inamngoja.

Yuda agundua mipango ya Nikanori
(1Mak 3:42-54)
12 Yuda alipata habari juu ya uvamizi wa Nikanori. Basi, alipowaambia wenzake kwamba jeshi la Nikanori lilikuwa linafika Yudea,
13 baadhi waliokuwa waoga na wanaoitilia shaka haki ya Mungu, wakatoroka mbio.
14 Lakini wengine wakauza vitu vyao vyote vilivyobaki na kumwomba Bwana awaokoe wale ambao Nikanori amekwisha wauza utumwani hata kabla ya mapigano kuanza.
15 Walisali Mungu awaokoe; na kama hakuwa tayari kufanya hivyo kwa ajili yao wenyewe tu, basi, awaokoe kwa sababu ya maagano aliyokuwa amefanya na wazee wao, na kwa sababu yeye, alikuwa amewaita kuwa watu wake na kwa ajili ya jina lake takatifu na tukufu.
16 Basi, Makabayo akawakusanya pamoja askari watu wake, wakafika 6,000, akawatia moyo wasitishike wala kukimbia kwa hofu pindi waonapo idadi kubwa ya askari wa mataifa mengine waliokuwa wanawajia kuwakabili bila ya kisa bali wapige vita kwa ushujaa,
17 wakikumbuka maovu waliyotenda watu wa mataifa mengine dhidi ya hekalu, na mateso waliyosababisha kwa Yerusalemu na walivyofutilia mbali mila za Kiyahudi.
18 Basi, akasema, “Wao wanategemea silaha zao na uhodari wao, lakini sisi tunamtumainia Mungu Mwenye Nguvu, ambaye aweza kuwaangamiza si tu hao wanaotushambulia bali hata ulimwengu mzima, kwa kuinamisha kichwa tu.”
19 Halafu Yuda aliendelea kuwakumbusha jinsi Mungu alivyokuwa amewasaidia wazee wao: Wakati wa Senakeribu maadui 185,000 waliangamizwa;
20 na walipokuwa Babuloni, Wayahudi 8,000 waliwasaidia Wamakedonia 4,000, wakawashinda Wagalatia 120,000 na kuteka nyara nyingi sana - hayo yote kwa msaada uliotoka kwa Mungu.

Yuda amshinda Nikanori
(1Mak 3:55-4L27)
21 Maneno ya Yuda yaliwatia moyo watu wake na kuwafanya wawe tayari kufa kwa ajili ya dini yao na nchi yao. Kisha akaligawa jeshi lake katika vikosi vinne
22 vya watu wapatao 1,500 kila kimoja. Yuda mwenyewe na nduguze, Simoni, Yosefu na Yonathani, walikuwa viongozi wa vikosi, kila mmoja na kikosi chake.
23 Licha ya hayo, Yuda alimteua Eleazari asome kwa sauti sehemu ya Maandiko Matakatifu, kisha akawapa watu wake msemo huu wa shime vitani: “Mungu atatusaidia.” Halafu, akiongoza kikosi cha kwanza yeye mwenyewe, akaanzisha vita dhidi ya Nikanori.
24 Mungu Mwenye Nguvu alipiga vita pamoja nao, wakawaua maadui zaidi ya 9,000, na kuwajeruhi wengi, na kulifanya jeshi lote la adui likimbie.
25 Wakawanyang'anya fedha watu waliokuwa wamekuja kuwanunua Wayahudi na kuwafanya watumwa. Kisha wakawafukuza maadui kwa masafa marefu, mpaka ilipowabidi kurudi,
26 kwa vile muda wa Sabato kuanza ulikuwa umekaribia sana.
27 Baada ya kukusanya silaha za maadui na kuwapora mali za maiti, waliadhimisha Sabato, wakimsifu na kumshukuru Mungu, kwa sababu alikuwa amewafikisha salama mpaka siku ile, na alikuwa amewapa ishara ya kwanza ya huruma yake.
28 Sabato ilipoisha, walitwaa sehemu ya mateka wakawapa watu waliojeruhiwa, wajane na yatima; na sehemu iliyobaki wakagawana miongoni mwa familia zao wenyewe.
29 Baadaye walijumuika kusali na kumwomba Bwana mwenye huruma, apatane kabisa na watumishi wake Wayahudi.

Yuda awashinda Timotheo na Bakide
30 Katika mapambano na majeshi ya Timotheo na Bakide, Wayahudi waliwaua watu zaidi ya 20,000. Waliteka ngome kadha ndefu sana na kupata nyara nyingi, ambazo waligawa sawa kwa sawa kwao wenyewe na kwa wajane, yatima, wazee, na majeruhi wa vita.
31 Kwa uangalifu walikusanya silaha zote za maadui na kuzihifadhi katika sehemu muhimu, lakini mateka wengine walipelekwa Yerusalemu.
32 Walimuua kamanda wa jeshi la Timotheo ambaye alikuwa mtu mbaya sana na aliyekuwa amewasumbua Wayahudi.
33 Wakiwa wanasherehekea ushindi wao katika mji wa wazee wao, wakawachoma moto mpaka kufa wale watu waliokuwa wameichoma moto milango ya hekalu. Miongoni mwa waliouawa alikuwa Kalisthene na wengine, waliokuwa wamejificha katika kibanda kimoja; hao wakapokea adhabu waliyostahili kwa maovu yao.
34 Nikanori, yule mlaanifu kupindukia, aliyewaleta wafanyabiashara 1,000 wa kuwanunua Wayahudi,
35 alidhiliwa na maadui zake kwa msaada wa Bwana, maadui walewale aliowadharau sana. Alitupilia mbali sare yake maridadi na kukimbia peke yake kama mtumwa anayetoroka, mpaka alipofika Antiokia. Alichokuwa amefanikiwa ni kuliangamiza tu jeshi lake zima.
36 Basi, mtu huyu, aliyekuwa amejaribu kuwalipa Waroma deni kwa kuwauza watu wa Yerusalemu, alioneshwa wazi kwamba Wayahudi wanaye anayewalinda na kwa hiyo wao hawawezi kamwe kushindwa kwa sababu walizitii sheria alizokuwa amewapa Mungu.

Generic placeholder image