14

Sifa za Simoni
1 Mwaka 172, mfalme Demetrio wa Pili alikusanya jeshi lake na kwenda Media kutafuta msaada zaidi kwa ajili ya vita dhidi ya Trifo.
2 Arsake wa Sita, mfalme wa Persia na Media, aliposikia kwamba Demetrio alikuwa ameivamia nchi yake akatuma mmoja wa makamanda wake na askari kadha kwenda kumkamata Demetrio na kumleta kwake mzima.
3 Askari hao wakalishambulia na kulishinda jeshi la Demetrio, wakamteka Demetrio na kumpeleka kwa mfalme Arsake. Mfalme akamtia Demetrio kifungoni.
4 Muda wote Simoni alipokuwa hai, nchi ilikuwa shwari. Alitafuta fanaka ya taifa lake; utawala wake ukawapendeza watu, na heshima aliyopata maishani mwake.
5 Kilele cha kufana kwake ni kuiteka bandari ya Yopa, akafungua njia ya kufikia visiwa vya Mediteranea.
6 Aliiongeza mipaka ya nchi yake, akawa na mamlaka kamili juu yake.
7 Aliwaleta nchini wafungwa wengi wa kivita; alitawala miji ya Gazara na Beth-zuri, na ngome ya Yerusalemu. Aliitakasa ngome hiyo, na hapakuwa na aliyempinga.
8 Wayahudi walilima mashamba yao kwa amani, nchi ilitoa mavuno yake, na miti matunda tele.
9 Wazee walibarizi barabarani, wote walizungumzia mambo mema; nao vijana walivalia sare maridadi za vita.
10 Simoni aliipatia miji chakula, na kuijazia silaha za kujihami. Sifa zake zilienea mpaka miisho ya dunia.
11 Alileta amani nchini, na furaha ya Israeli haikuwa na kifani.
12 Wote walikaa kwa amani kwenye mizabibu na mitini yao, wala hapakuwa na mtu wa kuwatisha.
13 Hakuna aliyebaki nchini kupigana nao, wafalme maadui walikuwa wamezimishwa siku zile.
14 Simoni aliwasaidia maskini wote wa taifa lake, aliizingatia sheria na kuondolea mbali waovu na waasi wote.
15 Alilipamba hekalu likatukuka, akaongeza idadi kubwa ya vyombo vya ibada.
16 Basi habari zikafika Roma, zikaenea hata mpaka Sparta kwamba Yonathani amekufa, watu wakasikitika mno.
17 Lakini Wasparta waliposikia kwamba Simoni alikuwa kuhani mkuu mahali pa hayati nduguye, na kwamba alikuwa anaitawala vizuri Yudea na miji yake,
18 wakaandika upya, katika vipande bapa vya shaba, mkataba wa urafiki waliokuwa wamefanya awali na Yuda na Yonathani, ndugu zake, wakampelekea maandishi hayo.
19 Makala hayo yalisomwa mkutanoni huko Yerusalemu.
20 Ifuatayo ni nakala ya barua iliyotoka kwa Wasparta: “Watu wa Sparta na watawala wao kwa kuhani mkuu Simoni, viongozi na makuhani wa Wayahudi, na kwa ndugu zetu Wayahudi wote: Salamu.
21 Wajumbe mliowatuma kwa watu wetu wametuarifu habari za sifa na utukufu mlio nao. Ujio wao umekuwa furaha kwetu.
22 Tumeandika yale waliyosema katika taarifa zetu za hadhara kama ifuatavyo: ‘Numenio mwana wa Antioko na Antipateri mwana wa Yasoni, wawakilishi rasmi wa Wayahudi, walikuja kwetu kufanya upya mkataba wao wa urafiki.
23 Watu wetu walifurahi, wakawapokea hao wajumbe kwa heshima, na nakala ya taarifa yao wakaiweka katika hifadhi ya taifa ya kumbukumbu, ili watu wa Sparta wawe na rekodi. Kuhani Mkuu Simoni amenakiliwa makala hiyo.’”
24 Baada ya hayo, Simoni alimtuma Numenio Roma kupeleka zawadi ya ngao kubwa ya dhahabu, yenye uzito wa kilo 500, ili kuuthibitisha ushirika kati ya Wayahudi na Waroma.
25 Wayahudi waliposikia hayo yote, wakajiuliza wenyewe: “Tutamshukuru jinsi gani Simoni na wanawe?
26 Maana Simoni, ndugu zake, na familia nzima ya baba yake, walisimama imara, wakapiga vita, wakawafukuza maadui za Israeli na kuleta uhuru wake.” Basi, wakaandika rekodi yake juu ya vipande vya shaba na kuviweka katika nguzo juu ya mlima Siyoni.
27 Hii ni nakala ya yale yaliyoandika: “Siku ya kumi na nane mwezi wa Eluli, mwaka 172, yaani, katika mwaka wa tatu wa utawala wa Simoni, kuhani mkuu,
28 katika mkutano mkuu wa makuhani, raia wa kawaida, maofisa na wazee wa nchi, mambo yafuatayo yalitangazwa kwetu:
29 Kila mara vita vilipotokea nchini mwetu, Simoni mwana wa Matathia, kuhani wa ukoo wa Yoaribu, na nduguze walijitoa mhanga kuwapinga maadui wa taifa letu, ili kulinda hekalu letu na sheria yetu. Hivyo wamelipatia taifa letu fahari kubwa.
30 Yonathani aliwaunganisha watu wetu, na akawa kuhani mkuu kabla hajafa.
31 Maadui wa Wayahudi walipoamua kuivamia nchi yetu na kuliteka hekalu,
32 akatwaa mamlaka na kuipigania nchi yake. Alitumia kiasi kikubwa cha fedha yake mwenyewe kununulia silaha na kulipia mishahara ya askari wa taifa lake.
33 Aliimarisha miji ya Yudea, na Beth-zuri, mji ulioko mpakani, ambako kabla yake silaha za maadui zilikuwa zimehifadhiwa. Huko akaweka kikosi cha askari.
34 Pia aliimarisha bandari ya Yopa, na mji wa Gazara ulio mpakani na Ashdodi, ambao kabla yake ulikuwa umekaliwa na maadui. Akawaweka Wayahudi mjini Gazara, na kuupatia chakula kadiri ya mahitaji ya watu.
35 Wananchi walipoona uzalendo wa Simoni na jitihada zake za kuliletea utukufu taifa lake, wakamfanya kiongozi wao na kuhani mkuu. Walifanya hivyo kwa sababu ya yote aliyokuwa ametekeleza, na kwa sababu ya haki na uaminifu alioonesha kwa taifa lake. Kwa kila njia alitafuta kuwafanikisha watu wake.
36 “Chini ya utawala wake watu wa mataifa mengine walifukuzwa nchini Yudea. Askari wa maadui walitimuliwa kutoka eneo lililo kaskazini ya hekalu, ambako walikuwa wamejijengea ngome; kutoka huko ngomeni askari hao walizoea kwenda kutia unajisi sehemu za hekalu.
37 Simoni akawaweka Wayahudi wakae katika ngome hiyo, akaiimarisha kwa usalama wa nchi, akaimarisha ulinzi wa Yerusalemu na kuongeza urefu wa kuta za mji.
38 “Kwa sababu ya hayo yote, mfalme Demetrio akauthibitisha ukuhani mkuu wake,
39 akampa hadhi ya kuitwa ‘Rafiki ya Mfalme’ na kumfanyia heshima kubwa.
40 Demetrio alifanya hivyo kwa sababu alikuwa amesikia kwamba Waroma waliwaita Wayahudi rafiki zao, washirika wao na ndugu, na kwamba walikuwa wamewapokea wajumbe wa Simoni kwa heshima.
41 “Kwa hiyo, Wayahudi na makuhani wao wanafurahi kwamba Simoni na wazawa wake ni viongozi na makuhani wakuu wao, mpaka nabii wa kweli atakapotokea.
42 Simoni atatawala nchi yao, ataliangalia hekalu na kuwateua maofisa wa kulishughulikia na kuwaweka watu watakaoiongoza nchi na kutunza silaha na ngome.
43 Watu ni lazima wamtii katika kila jambo. Mikataba yote ya kiserikali itaandikwa kwa jina lake, naye atakuwa na haki ya kuvaa mavazi ya kifalme pamoja na bizimu ya dhahabu.
44 “Hapana mtu, awe kuhani au nani, atakayekuwa na haki ya kisheria ya kutangua kipengele chochote cha maamuzi haya, kugeuza au kubadili amri yoyote ya Simoni, kuitisha mkutano wowote nchini bila ya ruhusa yake, au kuvaa mavazi ya kifalme pamoja na bizimu ya dhahabu.
45 Yeyote atakayekiuka au atakayedharau kanuni hizi atastahili adhabu.”
46 Wananchi, kwa kauli moja, walikubali kumpa Simoni haki ya kutekeleza mambo kufuatana na kanuni hizo.
47 Simoni aliitikia na kukubali kuwa kuhani mkuu, kamanda wa majeshi, na mkuu wa Wayahudi na wa makuhani.
48 Iliamuriwa kwamba tangazo hilo liandikwe katika vipande vya shaba na kuwekwa mahali pa kuonekana na wote katika eneo la hekalu,
49 na kwamba nakala zake ziwekwe katika hazina ya hekalu, ambako Simoni na wanawe wataweza kuziona.

Generic placeholder image