10

Aleksanda Epifane amfanya Yonathani kuhani mkuu
1 Mwaka 160, Aleksanda Epifane, mwana wa Antioko wa Nne, aliwasili Tolemai na kuuteka mji huo. Watu wakamkaribisha, naye akawa mfalme wao.
2 Mfalme Demetrio alipopata habari hizo, alikusanya jeshi kubwa, akaondoka kwenda kupambana na Aleksanda Epifane.
3 Wakati huo Demetrio alimpelekea Yonathani barua ya kirafiki iliyojaa maneno ya amani na mabembelezo,
4 akitumaini kumpata Yonathani awe upande wake na kufanya mkataba wa amani na Wayahudi kabla Aleksanda hajafanya mkataba nao dhidi yake.
5 Demetrio alifikiri kwamba Yonathani angekumbuka mabaya yote ambayo yeye alikuwa ametenda kwake, kwa nduguze, na kwa taifa zima la Wayahudi.
6 Na hivi Demetrio akamfanya Yonathani mshirika wake katika vita, akampa mamlaka ya kuunda jeshi na kulipatia silaha. Pia aliamuru kwamba Yonathani akabidhiwe wale mateka waliokuwa wamefungiwa katika ngome ya Yerusalemu.
7 Yonathani akaenda Yerusalemu na kuisoma barua hiyo mbele ya watu waliokuwa ngomeni.
8 Watu hao waliogopa sana waliposikia kwamba mfalme alikuwa amempa mamlaka Yonathani ya kuunda jeshi.
9 Walimkabidhi Yonathani wale mateka, naye akawarudisha kwa wazazi wao.
10 Yonathani alifanya makao yake makuu Yerusalemu, akaanza kuujenga upya na kuutengeneza mji huo.
11 Aliwaamuru wajenzi kutumia mawe ya mraba kujengea kuta za mji na ukuta wa kuuzunguka mlima Siyoni. Hilo lilitekelezwa.
12 Wageni waliokuwa katika ngome zilizojengwa na Bakide wakatoroka;
13 kila mmoja aliacha kazi yake na kurudi nchini kwake.
14 Lakini baadhi ya Wayahudi waliokuwa wametupilia mbali sheria walikuwa bado Beth-zuri; mji huo ulikuwa ndio kimbilio lao la mwisho.
15 Mfalme Aleksanda alipata habari zote kuhusu ahadi ambazo Demetrio alikuwa amempa Yonathani, kuhusu Yonathani mwenyewe, vita alivyokuwa amepiga, matendo yake ya ujasiri, na matatizo aliyokuwa ameyapata pamoja na nduguze.
16 Alijua kwa hakika kwamba hangempata mtu mwingine kama Yonathani. Hivi mfalme Aleksanda akaamua kumfanya Yonathani rafiki na mshirika wake.
17 Hii ni barua aliyomwandikia Yonathani:
18 “Mfalme Aleksanda kwa rafiki yake Yonathani: Salamu!
19 Nimesikia kwamba wewe ni mtu shujaa. Hivi una haki ya kuwa rafiki wa mfalme.
20 Basi, leo nimekuteua uwe kuhani mkuu wa taifa lako, na utaitwa ‘Rafiki ya Mfalme.’ Wewe utakuwa mshirika wetu utakayetupatia msaada.” Pamoja na barua hiyo, mfalme alimpelekea Yonathani vazi la urujuani na taji ya dhahabu.
21 Mwezi wa saba wa mwaka 160, wakati wa sikukuu ya vibanda, Yonathani akavaa mavazi hayo ya kuhani mkuu. Aliunda jeshi na kulipatia silaha nyingi.

Yonathani amsaidia Aleksanda Epifane
22 Demetrio aliposikia hayo, alifadhaika moyoni na kusema:
23 “Tumefanya nini sasa? Tumemwachilia Aleksanda atutangulie katika kujiimarisha kwa kufanya urafiki na Wayahudi!
24 Basi, nami pia nitawaandikia Wayahudi barua ya kirafiki. Nitaahidi kuwapa zawadi na nyadhifa mbalimbali, ili wanipatie msaada itakapobidi.”
25 Hivyo akaandika: “Mfalme Demetrio kwa taifa la Wayahudi: Salamu!
26 Tunayo furaha kusikia ya kuwa mmezingatia mkataba wetu, mmebaki waaminifu kwetu, na kwamba hamjajiunga na maadui zetu.
27 Kama mtaendelea hivyo kubaki waaminifu kwetu, tutawapeni zawadi kubwa.
28 Tutawaondoleeni kodi nyingi na kuwapa marupurupu mbalimbali.
29 “Kwa barua hii nafuta kwa Wayahudi wote kodi ya kichwa, na kodi ya chumvi, na kodi nyingine maalumu.
30 Zaidi ya hayo, kuanzia leo nawaondoleeni wajibu wa kunilipa mimi theluthi moja ya mavuno yenu ya nafaka, na nusu ya mavuno ya matunda. Toka sasa na kuendelea sitadai malipo hayo kutoka Yudea au zile wilaya tatu za Samaria na Galilaya zilizounganishwa na Yudea.
31 Yerusalemu na vitongoji vyake itatambuliwa kama mji mtakatifu, na hautawajibika kulipa kodi yoyote ile.
32 Toka leo sina mamlaka juu ya ngome ya Yerusalemu; naiweka chini ya kuhani mkuu, ambaye anaweza kumchagua na kumweka yeyote amtakaye kuilinda ngome hiyo.
33 Nawaachilia Wayahudi wote walio wafungwa wa kivita popote pale katika ufalme wangu. Wote hao wanasamehewa kodi, hata kodi ya mifugo yao.
34 Hapana Myahudi yeyote, popote pale katika ufalme wangu, atakayelipishwa kodi yoyote siku za Sabato, sikukuu za mwezi mwandamo, na sikukuu nyinginezo. Aidha, kodi hazitakusanywa siku tatu kabla au baada ya sikukuu hizo.
35 Siku hizo hapana mtu atakayeruhusiwa kudai malipo kwenu au kuwasumbueni kwa namna yoyote ile.
36 “Wayahudi wasiozidi 30,000 wanaweza kujiandikisha katika jeshi la mfalme, na watalipwa kama askari wengine wa mfalme.
37 Baadhi yao wanaweza kuwekwa katika ngome kuu za mfalme, na wengine kupewa nyadhifa mbalimbali katika serikali. Viongozi wao na maofisa wao watakuwa Wayahudi wenzao, na wataruhusiwa kufuata sheria na desturi zao, kama mfalme alivyoruhusu kwa watu wa Yudea.
38 “Zile wilaya tatu za nchi ya Samaria zilizounganishwa na Yudea, zitahesabiwa kuwa sehemu ya Yudea, na kuwekwa chini ya mamlaka ya kuhani mkuu peke yake.
39 Mapato ya mji wa Tolemai na ardhi yake yatatumika kulipia gharama za kuendeshea hekalu la Yerusalemu.
40 Pia naahidi kutoa kila mwaka zawadi ya vipande 15,000 vya fedha kutoka akiba inayohusika katika hazina ya mfalme.
41 Jumla ya fedha yote ya msaada kutoka serikalini, ambayo tumeshindwa kulipa miaka hii ya nyuma, italipwa mara, na kuendelea kulipwa kuanzia sasa kwa ajili ya huduma ya hekalu.
42 Zaidi ya hayo, hatutadai tena vile vipande 5,000 vya fedha kila mwaka kutokana na mapato ya hekalu. Fedha hiyo yawahusu makuhani wanaotumikia hekaluni.
43 Yeyote mwenye deni kwa mfalme, au mwenye deni lolote lile, akikimbilia katika hekalu la Yerusalemu au katika eneo lolote la hekalu hilo, ni lazima aachiliwe huru, na kupewa mali yake iliyo popote pale katika ufalme wangu.
44 “Gharama za kujenga upya na kulitengeneza hekalu zitalipwa kutoka hazina ya mfalme.
45 Hali kadhalika, gharama za kujenga upya na kuziimarisha kuta za Yerusalemu, pia kuta za miji miteule katika Yudea, zitalipwa kutoka hazina ya mfalme.”
46 Yonathani na watu wake waliposikia mapendekezo hayo ya mfalme Demetrio, walikataa kuyaamini au kuyapokea, kwa sababu walikumbuka jinsi alivyokuwa amewatenda vibaya na kuwanyanyasa bila kifani.
47 Hivi wakashikamana na Aleksanda, kwa vile alikuwa wa kwanza kutoa mapendekezo ya amani; wakabaki washirika wake mpaka alipokufa.
48 Mfalme Aleksanda aliunda jeshi kubwa, akajipanga kupambana na Demetrio.
49 Lakini majeshi ya wafalme hao wawili yalipokutana vitani, jeshi la Aleksanda liligeuka na kukimbia. Demetrio akalifukuza na kushinda vita.
50 Hata hivyo, Aleksanda alipigana kufa na kupona mpaka jua kuzama, naye Demetrio akauawa siku hiyo.
51 Ndipo Aleksanda akatuma wajumbe kwa Tolemai wa Sita, mfalme wa Misri, kusema hivi:
52 “Nimerejea kwenye ufalme wangu na kukalia kiti cha enzi cha wazee wangu. Nimemshinda Demetrio na kupindua serikali, na sasa nchi imo mikononi mwangu.
53 Nilipigana vita na Demetrio, nikamshinda yeye na jeshi lake, na nimeutwaa ufalme wake.
54 Sasa niko tayari kufanya urafiki nawe. Nipatie binti yako nimwoe, nami nitakupa wewe na binti yako zawadi mnazostahili.”
55 Mfalme Tolemai akajibu: “Hiyo ilikuwa siku ya furaha, uliporejea nchini kwako na kukalia kiti cha enzi cha wazee wako!
56 Nakubaliana na mapendekezo yako, lakini tuonane kwanza mjini Tolemai. Huko tutaelewana, nami nitakuoza binti yangu.”
57 Hivi, mwaka162, Tolemai na binti yake, Kleopatra, wakaondoka Misri na kuwasili Tolemai.
58 Mfalme Aleksanda akakutana nao, naye Tolemai akamwoza binti yake Kleopatra kwa Aleksanda. Harusi ilisherehekewa hapo Tolemai kwa fahari na desturi za kifalme.
59 Kisha, mfalme Aleksanda akamwandikia Yonathani aje waonane.
60 Yonathani akaenda Tolemai kwa fahari na kukutana na hao wafalme wawili. Aliwapa zawadi za fedha na dhahabu, na kuwapa zawadi nyingi maofisa wakuu waliokuwa wamefuatana na wafalme hao. Kila mmoja alipendezwa na kuvutwa na Yonathani.
61 Wakati huo huo kikundi cha Wayahudi waasi kikataka kumletea ghasia Yonathani. Kikatoa lawama na mashtaka dhidi yake, lakini mfalme Aleksanda hakukitegea sikio.
62 Ila alitoa amri Yonathani avuliwe nguo zake na kuvishwa mavazi ya kifalme, ya urujuani. Hayo yakatendeka.
63 Pia mfalme akamketisha Yonathani mahali pa heshima pembeni mwake. Kisha akawaambia maofisa wake: “Nendeni na Yonathani katikati ya mji, mkatangaze kwamba ni marufuku mtu yeyote yule kumshtaki Yonathani kuhusu jambo lolote lile; asithubutu yeyote kumuudhi kwa sababu yoyote ile.”
64 Tangazo hilo lilipotolewa, na wale wote waliopanga kumlaumu na kumshtaki Yonathani walipoona jinsi alivyokuwa ametukuzwa na kuheshimiwa kwa kuvikwa mavazi ya kifalme, wakakimbia.
65 Mfalme akazidi kumpa heshima Yonathani kwa kumworodhesha katika kundi la kwanza la “Marafiki wa Mfalme,” na kumfanya jenerali na mkuu wa mkoa wake.
66 Ndipo Yonathani akarejea Yerusalemu, mwingi wa furaha na fanaka.

Ushindi wa Yonathani dhidi ya Apolonio
67 Mwaka 165 Demetrio wa Pili, mwana wa Demetrio wa Kwanza, aliondoka Krete na kuwasili katika nchi ya wazee wake.
68 Mfalme Aleksanda alipopata habari hiyo, alifadhaika sana, akarejea Antiokia.
69 Naye Demetrio akamteua Apolonio kuwa mkuu wa mkoa wa Siria Kuu. Apolonio akaunda jeshi kubwa, akapiga kambi karibu na Yamnia, na kupeleka kwa Yonathani, kuhani mkuu, ujumbe ufuatao:
70 “Wewe ndiwe peke yako uwezaye kuja kujaribu kutushambulia. Lakini kwa nini unaendeleza uasi huu huko milimani wakati hapana mtu yeyote anakuunga mkono?
71 Kama kweli unaliamini jeshi lako, teremka huku chini kwenye tambarare, tupimane nguvu. Hali halisi ni kwamba vikosi vya miji viko nyuma yangu.
72 Utatambua mimi ni nani na marafiki zangu ni akina nani, na utagundua kwamba huwezi kufua dafu mbele yetu. Waliokutangulia wamekwisha pigwa mara mbili katika ardhi yao wenyewe;
73 unawezaje wewe kutazamia kuwashinda wapandafarasi wangu na wanajeshi wa aina hii nilio nao hapa katika nchi tambarare? Kumbuka, huku chini hakuna kokoto wala jiwe la kujificha nyuma yake, na hakuna njia ya kutorokea.”
74 Yonathani alipopata ujumbe huo kutoka kwa Apolonio, alikasirika sana. Akachagua askari 10,000 kutoka Yerusalemu, na nduguye, Simoni, pia akaleta askari. Vikosi hivyo
75 vikapiga kambi nje ya Yopa. Watu wa mji huo walikataa kuwaingiza ndani askari hao kwa sababu mlikuwa na kikosi cha askari wa Apolonio. Yonathani akaanza mashambulizi.
76 Watu wa mjini wakashikwa na hofu, wakafungua milango ya mji. Yonathani akauteka mji wa Yopa.
77 Apolonio aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliwachukua wapandafarasi 3,000 na jeshi kubwa la askari wa miguu, akaenda Ashdodi, kama vile alikuwa anaendelea na safari. Kumbe, wakati huo huo, akijivunia nguvu ya wapandafarasi wake, akasonga mbele hadi chini kwenye tambarare.
78 Yonathani akamfuatia Apolonio hadi Ashdodi, na mapambano yakaanza.
79 Apolonio, kumbe alikuwa amewaacha nyuma kwa siri wapandafarasi 1,000.
80 Mpaka wakati huo Yonathani hakutambua kwamba ameotewa. Mara jeshi lake likawa limezungukwa, na mishale ya adui ikawaporomokea kama matone ya mvua toka asubuhi mpaka jioni.
81 Hata hivyo, askari wa Yonathani walisimama imara, kama alivyokuwa amewaamuru, na wapandafarasi wa adui wakaanza kuchoka.
82 Halafu, hao wapandafarasi walipokwisha nguvu kabisa, Simoni akatokeza katika uwanja wa mapambano na vikosi vyake. Akawashambulia na kuwashinda askari wa miguu wa adui, nao wakachomoka mbio.
83 Wapandafarasi, ambao kwa sasa walikuwa wametawanyika katika uwanja mzima wa mapambano, wakakimbilia Ashdodi, ambako walijificha katika hekalu la mungu wao, Beth-dagoni.
84 Lakini Yonathani akauchoma moto mji wa Ashdodi na hekalu la Beth-dagoni, akawaunguza na kuwaua wote waliokimbilia huko. Halafu akaichoma moto miji ya jirani na kuteka nyara.
85 Siku hiyo watu wapatao 8,000 waliuawa kwa upanga au kwa moto.
86 Baada ya hayo, Yonathani akaondoka na kwenda kupiga kambi Askaloni. Wakazi wa mji huo wakatoka nje na kumkaribisha kwa sherehe na shangwe.
87 Yonathani na watu wake wakarejea Yerusalemu na mateka wengi.
88 Mfalme Aleksanda aliposikia hayo yote, alimpatia Yonathani heshima kubwa zaidi.
89 Alimpelekea bizimu ya dhahabu, ambayo kwa kawaida hupewa jamaa za mfalme tu. Pia alimpa mji wa Ekroni na viunga vyake.

Generic placeholder image