51

Utenzi wa shukrani
1 Nakushukuru, ee Bwana na Mfalme, nakusifu, ee Mungu, Mwokozi wangu. Nalitukuza jina lako.
2 Maana wewe umekuwa mlinzi na msaidizi wangu. Umeukomboa mwili wangu kutoka kwenye maangamizi, kutoka kwenye mitego ya watu wadanganyifu, na kutoka kwa watu wasemao uongo. Mbele ya maadui zangu ulikuwa upande wangu; umekuwa msaada wangu, umenikomboa.
3 Kwa ukuu wa huruma yako na jina lako, umenikomboa makuchani mwa maadui waliotaka kuniangamiza, kutoka kwa wale waliotafuta maisha yangu, kutoka katika mateso mengi niliyoyavumilia;
4 kutoka katika moto ulionisonga pande zote, moto ambao mimi sikuuwasha;
5 kutoka katika vilindi vya kuzimu, kutoka kwa wanaosema machafu na uongo, na kutoka masengenyo ya ulimi mwovu.
6 Nilikuwa kwenye nimekaribia kabisa kifo, na maisha yangu yalikuwa karibu na chini kuzimu.
7 Nilikuwa nimezungukwa kabisa, sikuwa na yeyote wa kunisaidia. Nilitazama nipate msaada wa binadamu, lakini hakuna aliyenisaidia.
8 Kisha nikakumbuka huruma zako, ee Bwana, na kazi zako za tangu zamani, kwamba wewe wawakomboa wale wanaokutegemea, na huwaokoa makuchani mwa maadui zao.
9 Nami nikapeleka juu kwako ombi langu, nikakuomba uniokoe kutoka kwenye kifo.
10 Namlilia Bwana: “Wewe u Baba yangu! Usiniache katika siku ya mateso, ambapo hakutakuwa na msaada dhidi ya adui.
11 Nitalisifu jina lako daima, nitakuimbia nyimbo za sifa na shukrani.” Ombi langu lilipokelewa,
12 maana uliniokoa nisiangamie, ukanisalimisha wakati mbaya. Kwa hiyo nitakushukuru na kukusifu, nitalisifu jina la Bwana.

Shairi la kumtafuta Hekima
13 Nilipokuwa bado mdogo, kabla sijaanza kusafiri, kwa sala yangu nilitafuta hadharani nimpate Hekima.
14 Nikiwa nimesimama nje ya hekalu nilimtafuta, nami nitamtafuta mpaka mwisho.
15 Tangu kuchanua kwake mpaka kuiva, nilimfurahia sana moyoni mwangu. Nyayo zangu zilifuata njia nyofu; tangu ujana wangu nimezifuata njia zake.
16 Nilitega sikio langu kidogo nikampokea Hekima, nami nikajipatia mafunzo mengi.
17 Nilizidi kuendelea kwa hekima, naye atakayenipa hekima nitamtukuza.
18 Maana niliamua kuishi kulingana na hekima, nikawa na hamu sana ya kutenda mema, na wala sitaaibishwa kamwe.
19 Nilijishughulisha sana nipate hekima, nikawa mwangalifu sana kuhusu mwenendo wangu. Nilinyosha mikono yangu mbinguni kuomba, nikalalamika kwa vile sikumjua Hekima.
20 Niliielekeza nafsi yangu kwa Hekima, nami nikampata kwa kujitakasa. Kutoka kwake nilipata maarifa tangu mwanzo, nami najua kwamba sitaachwa bila msaada wake.
21 Moyo wangu ulipania kumtafuta Hekima, ndiyo maana sasa nimepata utajiri mkubwa.
22 Bwana alitunukia zawadi ya kuwa na ulimi, nami nitautumia kumsifu yeye.
23 Njoni kwangu enyi msiojua kitu, ingieni na kukaa shuleni kwangu.
24 Kwa nini mnalalamika kuwa hamna mambo haya, na kwa nini mioyo yenu inaona kiu?
25 Nilifungua kinywa changu na kusema: “Jipatieni hekima bila kununua.”
26 Inamisheni shingo zenu chini ya nira yake, na kuacha mioyo yenu ipate mafunzo; Hekima anapatikana karibu sana.
27 Oneni wenyewe kwamba nimefanya kazi kidogo, lakini nimejipatia amani kubwa.
28 Jipatieni mafundisho kwa fedha nyingi, nanyi mtajipatia nayo dhahabu nyingi.
29 Mioyo yenu na ifurahie huruma ya Bwana, wala msiaibishwe kamwe wakati mnapomsifu.
30 Fanyeni kazi yenu kabla ya wakati uliopangwa, naye Mungu awapeni tuzo lenu wakati wake!

Generic placeholder image