26

1 Heri mume aliye na mke mwema siku za maisha yake zitaongezwa maradufu.
2 Mke mwaminifu ni furaha ya mumewe; mumewe ataishi kwa amani miaka yote.
3 Mke mwema ni baraka kubwa; baraka anayopewa mume amchaye Bwana.
4 Mtu kama huyo, awe tajiri au maskini, daima ana furaha moyoni; na wakati wote ni mwenye uso mkunjufu.
5 Moyo wangu unayaogopa mambo matatu, na la nne linanitisha: Uvumi mbaya mjini, genge la waovu, na mashtaka ya uongo. Hayo yote ni mabaya kuliko kifo.
6 Lakini daima kuna masikitiko na huzuni moyoni mke anapomwonea wivu mke mwenzake, na ulimi wake kumshambulia kila mtu.
7 Mke mwovu ni kama nira inayokwaruza shingoni; kujaribu kumtawala ni sawa na kushika nge.
8 Mke aliyelewa husababisha hasira, hawezi kuficha aibu yake.
9 Mwanamke malaya huonekana katika macho yake, naye hujulikana kwa kope zake.
10 Uwe mkali kwa binti aliye na ukaidi, la sivyo, akipata nafasi tu, ataitumia kujiumiza mwenyewe.
11 Jihadhari na macho yake yasiyo na haya, wala usishangae akikukosea.
12 Kama vile msafiri mwenye kiu afunuavyo kinywa chake na kunywa maji yoyote ayaonayo, ndivyo na binti huyo atakavyoketi kila mahali na kujifunua kwa kila mwanamume apitaye hapo.
13 Mke mzuri humfurahisha mumewe, na ujuzi wake humfanya awe na nguvu.
14 Mke mkimya ni zawadi kutoka kwa Bwana, hakuna bei ya kufaa kulingana naye.
15 Mke mwenye kiasi hupendeza zaidi na zaidi, hakuna kipimo kinachoweza kumpima mke mwenye tabia nzuri.
16 Kama vile pambazuko la jua katika anga la Bwana ndivyo ulivyo uzuri wa mke mwema na nyumba yake nadhifu.
17 Kama vile taa iwakavyo juu ya kinara kitakatifu, ndivyo ulivyo uzuri wa uso wake na umbo lake.
18 Na kama nguzo za dhahabu juu ya vikalio vya fedha ndivyo ilivyo miguu yake mizuri, juu ya nyayo imara.
[19 Mwanangu, hifadhi nguvu za ujana wako, wala usiwape wageni nguvu zako.
20 Jitafutie nchini kote eneo lenye rutuba, ukapande humo mbegu yako mwenyewe, ukitumainia kuwa na ukoo wako bora.
21 Hivyo watoto wako mwenyewe wataishi, watakuwa mashuhuri, wakiwa na matumaini ya malezi bora.
22 Mwanamke malaya ni kama mate; mke mtembezi ni kama mlingoti wa kifo.
23 Mwanamke asiyemcha Mungu amepangiwa mume mkosefu, lakini mwema amepangiwa mume mcha Mungu.
24 Mke asiye na aibu hufurahi kujiaibisha, lakini mke mwenye kiasi ana haya hata mbele ya mumewe.
25 Mwanamke mkaidi ni sawa na mbwa, lakini mwenye haya humcha Bwana.
26 Mke anayemheshimu mumewe kila mtu atamwona ana hekima, lakini anayemdharau kwa majivuno wote watamwona kuwa mwovu. Heri mume aliye na mke mwema maana siku za maisha yake zitakuwa maradufu.
27 Mke wa makelele, mwenye kueneza uvumi, ni kama tarumbeta ya vita; na mume aliyejifunga na mke wa namna hiyo maisha yake ni vita.]

Mambo yaletayo huzuni
28 Yako mambo mawili yanayonihuzunisha moyoni na jambo la tatu lanikasirisha: Askari ambaye amefilisika, watu wenye akili wanaodharauliwa, na mtu anayeacha unyofu na kutenda dhambi. Huyo Bwana atamwadhibu kwa upanga.
29 Ni vigumu kwa mfanyabiashara kuepa makosa, na mchuuzi kuepa dhambi.

Generic placeholder image