17

1 Bwana aliumba binadamu kwa udongo na hukohuko udongoni binadamu atarudi.
2 Aliwapangia binadamu siku za kuishi, na kuwapa mamlaka juu ya vitu vyote duniani.
3 Aliwapa nguvu kama zake mwenyewe, aliwaumba kwa mfano wake.
4 Alivifanya viumbe vyote vimwogope binadamu, akawapa binadamu mamlaka juu ya wanyama na ndege. [ 5Bwana aliwapa milango mitano ya maarifa, lakini pia aliwapa mlango wa sita, yaani akili na mlango wa saba, yaani uwezo kwa kutumia kufikiri. Kwa njia ya milango hiyo wanaweza kutafsiri yale yanayowajia.]
6 Aliwapa binadamu ndimi, macho na masikio, akawapa na moyo wa kuweza kufikiri.
7 Aliwajaza maarifa na akili, akawaonesha yaliyo mema na mabaya.
8 Alisimika jicho lake ndani yao, ili kuwawezesha kuona uzuri wa kazi zake,
[ 9 na akawaruhusu kujivunia maajabu yake milele.]
10 wapate kulisifu jina lake takatifu, na kutangaza ukuu wa kazi zake.
11 Aliweka mbele yao elimu, na kuwajalia sheria ya uhai.
12 Alifanya nao agano la milele, na kuwafunulia maamuzi yake.
13 Macho yao yakaona utukufu wake, na masikio yao yakasikia utukufu wa sauti yake.
14 Aliwaambia, “Msifanye uovu wowote;” akawaamuru namna ya kuishi na jirani zao.

Mungu ni Hakimu
15 Bwana anaiona mienendo ya binadamu; hawawezi kujificha mbele yake. [ 16Tabia yao tangu utoto unaelekea uovu. Hawana nguvu ya kuigeuza mioyo yao iliyo kama mawe iwe mioyo ya mtu.]
17 Aliweka mtawala juu ya kila taifa, lakini Israeli ni mali yake Bwana binafsi. [ 18Israeli ni mzaliwa wake wa kwanza, ambaye anamlea na kumpa nidhamu, bila kumwacha.]
19 Matendo yote ya watu ni wazi kwa Bwana kama jua, kila wanachofanya anakiona mbele yake.
20 Maovu ya binadamu hayawezi kufichika mbele yake, dhambi zao ziko wazi mbele ya Bwana. [ 21Lakini Bwana ni mwenye neema na anavijua viumbe vyake; hivyo anavihurumia na kamwe hajavitupa.]
22 Sadaka kwa maskini ni kama mhuri kwake, yeye huthamini wema wa mtu kama mboni ya jicho lake.
23 Baadaye atatokea na kuwalipiza waovu; watapata kila mmoja wanachostahili.
24 Lakini wale wanaotubu atawajalia wamrudie, na huwatia moyo wale waliokata tamaa.

Wito wa toba
25 Mgeukie Bwana na kuacha dhambi zako; omba mbele yake na uache makosa yako.
26 Mrudie Mungu Mkuu na kuachana na uovu; uchukie kwa moyo wote kufanya machukizo.
27 Huko kuzimu nani atamwimbia sifa Mungu Mkuu? Ni wale tu walio hai wanaoweza kumshukuru.
28 Waliokufa na wasiokuwako tena hawawezi kumsifu; ni wale walio hai na wazima ndio wanaoweza kumsifu Bwana.
29 Jinsi gani huruma ya Bwana ilivyo kuu, na jinsi anavyowasamehe wanaomrudia!
30 Sisi binadamu hatuwezi kuwa na kila kitu; maana sisi sote ni viumbe vyenye kufa.
31 Ni kitu gani kingaacho kama jua? Hata hivyo, jua nalo hupatwa. Binadamu aliye kiumbe hufikiria tu maovu.
32 Bwana hulikagua jeshi lote la mbinguni, lakini binadamu ni mavumbi tu na majivu!

Generic placeholder image