46

Yoshua
1 Yoshua, mwana wa Nuni alikuwa shujaa vitani, na alimfuata Mose katika unabii. Alikuwa, kama jina lake, mkombozi mkubwa wa wateule wa Mungu, akawalipiza kisasi adui waliopigana nao, ili kuwapatia Waisraeli urithi wao.
2 Jinsi gani alivyokuwa na fahari alipoinua mikono yake, na kunyosha upanga wake dhidi ya miji!
3 Nani kabla yake aliyekuwa imara hivyo? Maana yeye alipigana vita vya Bwana.
4 Je, jua halikusimamishwa kwa mkono wake? Je, siku haikurefushwa kuwa kama siku mbili?
5 Yoshua, alimwomba Mungu Mkuu, Mwenye Nguvu, wakati maadui walipomsonga kila upande.
6 Naye Bwana, aliye mkuu, akamjibu, akapeleka mvua ya mawe yenye nguvu. Bwana alilishambulia lile taifa na kwenye mtelemko wa Beth-horoni akawaangamiza waliompinga. Hivyo mataifa yakaziona vizuri silaha zake, kwamba alikuwa anapigana mbele ya Bwana, maana alimfuata Mungu Mkuu kwa moyo wake wote.
7 Katika siku za Mose, Yoshua alikuwa mwaminifu yeye na Kalebu, mwana wa Yefune, walisimama imara kuupinga umati, wakawazuia watu wasitende dhambi, na kunyamazisha manunguniko yao.
8 Kati ya watu laki sita waliokuwa safarini, ni hao wawili tu waliobakizwa, wakawaongoza watu kwenye nchi yao wenyewe, nchi iliyotiririka maziwa na asali.
9 Bwana alimpa Kalebu nguvu, nayo ilibaki naye hadi uzeeni. Hivyo alikwenda mpaka nchi ya milima na wazawa wake wakaiteka kuwa urithi wao,
10 hata watu wote wa Israeli wakaona kwamba ni vizuri kumfuata Bwana.

Waamuzi
11 Kisha kulikuwa na waamuzi, kila mmoja maarufu kikwake, ambao hawakudanyanyika kuabudu sanamu na kumwacha Bwana. Walikumbukwa daima kwa sifa.
12 Miili yao na ipate nguvu huko makaburini, na majina yao hao waliomcha Bwana yadumu kwa njia ya wazawa wao.

Samueli
13 Samueli alipendwa na Bwana. Akiwa nabii wa Bwana alianzisha ufalme, akawapaka mafuta watawala wa watu wake.
14 Aliiamua jumuiya ya watu kulingana na sheria ya Bwana, naye Bwana akawalinda watu wa Yakobo.
15 Kwa uaminifu wake alithibitishwa kuwa kweli nabii, na kwa maneno yake akawa mwonaji wa kutegemewa.
16 Alimwomba Bwana, Mwenye Nguvu, wakati aliposongwa na maadui kila upande, akamtolea Bwana tambiko ya kondoo mchanga.
17 Kisha Bwana alinguruma kutoka mbinguni, akaifanya sauti yake isikike kwa kishindo kikubwa.
18 Aliwafutilia mbali viongozi wa watu wa Tiro, na watawala wote wa Wafilisti.
19 Kabla ya usingizi wake wa mwisho, Samueli alishuhudia mbele ya Bwana na mteule wake, kwamba hakuwahi kuchukua mali ya mtu yeyote, hata kama ni jozi ya viatu. Hakuna mtu yeye aliyemshtaki.
20 Hata baada ya kufariki aliendelea kutoa unabii akamfunulia mfalme mwisho wake; alitoa sauti kutoka kaburini, alitoa unabii kufutilia mbali uovu wa watu.

Generic placeholder image