15

1 Ndivyo afanyavyo mtu anayemcha Bwana; mtu ashikaye sheria zake atampata Hekima.
2 Hekima atakuja kumlaki kama mama, atamkaribisha kama bibi arusi wake.
3 Atamlisha chakula cha maarifa, atamnywesha maji ya Hekima.
4 Mtu huyo atamwegemea hekima na hataanguka; atamtegemea na hataaibishwa.
5 Hekima atamtukuza juu ya jirani zake; na katikati ya mkutano atamwezesha kusema.
6 Mtu huyo atapata furaha na fahari ya shangwe, na jina lake kukumbukwa daima.
7 Lakini wapumbavu hawawezi kumpata Hekima wenye dhambi hawatamwona.
8 Hekima yu mbali na wenye kiburi, na waongo hawataweza kamwe kumfikiria.
9 Mwenye dhambi hafai kuimba nyimbo za sifa, maana hajapelekewa kutoka kwa Bwana.
10 Nyimbo za sifa yabidi ziimbwe kwa hekima, hapo Bwana atazifanikisha.

Kuchagua kwa hiari
11 Usiseme: “Bwana ndiye aliyesababisha nianguke”, maana yeye hawezi kusababisha jambo analochukia.
12 Usiseme: “Yeye ndiye aliyenipotosha”, maana yeye hahitaji msaada wa mwenye dhambi.
13 Bwana anayachukia machukizo yote; hata wale wanaomcha wanayachukia hayo.
14 Bwana ndiye aliyemwumba binadamu mwanzoni, akampa uwezo wa kujiamulia mambo yake mwenyewe.
15 Ukitaka, unaweza kuzitii amri, kuishi kwa uaminifu au la, ni chaguo lako.
16 Bwana ameweka mbele yako moto na maji: Nyosha mkono wako, ujichukulie upendacho.
17 Binadamu amewekewa mbele yake uhai na kifo; kile atakachochagua atapewa.
18 Maana hekima ya Bwana ni kuu. Yeye ni mwenye nguvu na anaona yote.
19 Bwana huwaangalia kwa wema wale wanaomcha; yeye anajua kila kitu afanyacho binadamu.
20 Yeye hajamwamuru yeyote kutomcha Mungu, wala hajamruhusu mtu yeyote kutenda dhambi.

Generic placeholder image