39

1 Lakini anayepania kujifunza sheria ya Mungu Mkuu, hutafuta hekima ya watu wa kale, na kushughulikia waliyosema manabii.
2 Huyahifadhi mazungumzo ya watu mashuhuri, na kupambanua magumu ya mifano.
3 Hutafuta maana zilizofichika za methali, na methali za kutatiza kwake si kitu.
4 Huyo huwatumikia wakuu, na huonekana mbele ya watawala; husafiri nchi za kigeni na amepata kujua wema na ubaya wa watu.
5 Asubuhi huamka kwa moyo na bidii na kutafuta kumwomba Bwana aliyemuumba; humwekea Mungu Mkuu maombi yake, hufungua kinywa kusali, na kuomba msamaha kwa dhambi zake.
6 Kama Bwana aliye mkuu anataka atamjaza mtu huyo busara, naye atabubujika maneno ya hekima na kumshukuru Bwana katika sala.
7 Ataelekeza mashauri na maarifa yake vizuri, na kutafakari juu ya siri zake Bwana.
8 Ataonesha maarifa yake aliyojifunza, na kuionea fahari sheria ya agano la Bwana.
9 Watu wengi watasifu maarifa yake, nayo hayatasahaulika kamwe. Kumbukumbu lake halitatoweka, na jina lake litakumbukwa vizazi vyote.
10 Mataifa yatatangaza hekima yake, nayo jumuiya ya watu itasema sifa zake.
11 Ataishi maisha marefu ataacha jina maarufu kuliko wengi; na akifariki, kwake itakuwa imetosha. Wimbo wa kumsifu Mungu
12 Bado nina ya kusema niliyoyafikiria, nami nimejaa kama mwezi mpevu.
13 Nisikilizeni enyi watoto wema, mkachanue kama waridi lililopandwa kando ya kijito.
14 Toeni harufu nzuri kama ya ubani, na kuchanua maua kama yungiyungi. Tawanyeni angani harufu yenu na kuimba wimbo wa sifa; msifuni Bwana kwa ajili ya matendo yake yote.
15 Tangazeni ukuu wa jina lake, mshukuruni kwa nyimbo za sifa, mwimbieni kwa vinywa vyenu na vinubi. Mnapomshukuru mwimbieni hivi:
16 “Vitu vyote vimeumbwa na Bwana, maana vyote ni vizuri sana. Kila anachoamuru kitafanyika wakati wake.”
17 Usiulize “Hiki ni kitu gani?” au, “Kwa nini hiki?” Maana tutajifunza vyote wakati wake Bwana. Kwa neno lake maji huacha kutiririka yakajirundika kwa tamko la kinywa chake maji yalikaa ghalani mwake.
18 Kwa amri yake kila anachopenda hufanyika, hakuna awezaye kupunguza uwezo wake wa kuokoa.
19 Matendo ya viumbe vyote ni wazi mbele yake, hakuna kiwezacho kujificha mbele yake.
20 Yeye huona tangu milele hata milele, na hakuna kitu cha ajabu kwake.
21 Usiulize “Hiki ni kitu gani?” au, “Kwa nini hiki?” maana kila kitu kimeumbwa kwa matumizi yake.
22 Baraka zake huijaza nchi kavu kama kwa mto, huzilowanisha kama kwa mafuriko.
23 Ghadhabu yake itayafukuza mataifa, kama ageuzavyo maji mazuri kuwa ya chumvi.
24 Kwa wanaomcha njia zake zimenyoka, hali kwa waovu njia zake zina vikwazo.
25 Tangu mwanzoni Mwenyezi-Mungu aliumba vitu vyema kwa ajili ya walio wema, lakini kwa watu wabaya aliumba vitu vibaya na vyema.
26 Mahitaji ya msingi kwa maisha ya mtu ni maji, moto, chuma na chumvi; unga, maziwa, asali, divai, mafuta na mavazi.
27 Hivi vyote ni vizuri kwa wamchao Mungu, lakini hugeuka kuwa maovu kwa wenye dhambi.
28 Kuna pepo zilizoumbwa kuwaadhibu watu, nazo zikikasirika zinaadhibu vikali. Wakati wa hukumu zitaonesha nguvu yake, na hivyo kuituliza hasira ya Muumba wao.
29 Moto, mvua ya mawe, njaa na maradhi; hivi vyote vimeumbwa kuwaadhibu watu.
30 Meno ya wanyama wakali, nge na nyoka na upanga unaowaadhibu wasiomcha Mungu kwa maangamizi.
31 Vyote vitafurahi kutekeleza amri za Bwana; vitakuwa tayari duniani kumhudumia, na wakati utakapowadia havitaiasi amri yake.
32 Kwa hiyo nimekuwa na hakika ya hayo tangu mwanzo; nimeyawaza na kuwazua, nikayaandika.
33 Kazi zote za Bwana ni njema, naye huwapatia watu mahitaji yao yote wakati wake.
34 Usiseme: “Kitu hiki ni kibaya kuliko kile,” maana faida ya kila kitu itaonekena wakati wake.
35 Sasa basi, imba sifa kwa moyo wote, na kulisifu jina la Bwana.

Generic placeholder image