44

Sifa kwa wazee
1 Sasa, na tuwasifu watu mashuhuri, wazee wetu na vizazi vilivyopita.
2 Bwana aliwapa fahari kubwa, akawafanya wakuu tangu siku za kale.
3 Walikuwako wale waliotawala falme zao, watu mashuhuri kwa nguvu zao; washauri waliojaa busara, watangazaji wa unabii.
4 Wengine waliongoza mataifa kwa mawazo yao, wakawa wenye maarifa ya elimu kwa faida ya watu, wenye hekima katika maneno na mafundisho yao.
5 Walitunga nyimbo kwa ufundi, wakabuni mashairi na kuyaandika.
6 Walikuwa matajiri wenye mali tele, waliishi kwa utulivu katika makazi yao.
7 Hao wote waliheshimika katika vizazi vyao, wakawa wenye fahari nyakati zao.
8 Baadhi yao waliacha jina jema duniani, na watu wakatangaza sifa zao mpaka leo.
9 Wako na wengine ambao hawakumbukwi, ambao wametoweka wakawa kama hawakuishi. Walikuwa kana kwamba hawakupata kuzaliwa, kadhalika na watoto wao baada yao.
10 Lakini wale wengine walikuwa watu wema, ambao matendo yao adili hayajasahaulika.
11 Mali yao hubaki na wazawa wao, na huo ndio urithi wao.
12 Wazawa wao huzingatia agano, na kwa ajili yao wataendelea kufanya hivyo.
13 Nasaba yao itadumu milele, na fahari yao haitafutika.
14 Miili yao ilizikwa kwa amani, na majina yao yanadumu kizazi hata kizazi.
15 Watu watasimulia hekima yao, na jumuiya ya watu itatangaza sifa zao.

Henoki na Noa
16 Henoki alimpendeza Bwana, akachukuliwa mbinguni. Yeye alikuwa mfano bora wa toba vizazi vyote.
17 Noa alionekana mkamilifu na mwadilifu; yalipokuja maangamizi, akawa mwanzo mpya wa binadamu. Maana kwake watu waliachwa duniani, tufani ilipokuja.
18 Bwana alifanya naye agano la milele, kwamba viumbe vyote wasifutiliwe mbali kwa ile tufani.

Abrahamu, Isaka na Yakobo
19 Abrahamu alikuwa mzee maarufu wa mataifa mengi, hakuna aliyekuwa na fahari kama yeye.
20 Alishika sheria ya Mungu Mkuu, na Bwana akafanya agano naye, akakamilisha katika mwili wake alama ya agano hilo, naye Abrahamu alipojaribiwa, akaonekana kuwa mwaminifu.
21 Hivyo Bwana akamhakikishia kwa kiapo kwamba mataifa yatabarikiwa kwa njia ya wazawa wake; kwamba wazawa wake watakuwa wengi kama mavumbi ya nchi. Kwamba watakuwa wengi kama nyota, na urithi wao tangu bahari hadi bahari, tangu mto Eufrate mpaka miisho ya dunia.
22 Vilevile Bwana alimpa Isaka uthibitisho ule ule kwa ajili ya Abrahamu, baba yake. Baraka za watu wote na agano lake,
23 aliziweka juu ya Yakobo. Alimwimarisha Yakobo kwa baraka zake, akampa ile nchi iwe yake mwenyewe, na kuigawa miongoni mwa makabila kumi na mawili.

Generic placeholder image