38

Dawa na ugonjwa
1 Mpe daktari heshima anayostahili, kwa sababu ya huduma zake kwako, kwa vile naye aliumbwa na Bwana.
2 Maana kipaji chake cha kuponya chatoka kwa Mungu Mkuu; naye hupata zawadi kutoka kwa mfalme.
3 Ujuzi wa daktari humfanya maarufu, naye huheshimiwa miongoni mwa wakuu.
4 Bwana aliumba dawa zote kutoka ardhini, na mtu mwenye busara hawezi kuzidharau.
5 Je si kwa kijiti maji yaligeuzwa kuwa mazuri ili Mungu awaoneshe watu nguvu yake?
6 Bwana aliwapa watu maarifa na ujuzi, ili atukuzwe katika kazi zake za ajabu!
7 Kwa dawa huwaponya watu na kuondoa maumivu;
8 mchanganya dawa hutengeneza mchanganyiko wake. Kazi za Bwana hazina mwisho; afya yote duniani hutoka kwake.
9 Mwanangu, ukiugua usiwe mzembe juu ya ugonjwa, bali mwombe Bwana naye atakuponya.
10 Acha makosa yako, uamue kutenda mema, na kutakasa moyo wako dhambi zote.
11 Mtolee Bwana tambiko ya harufu nzuri, na tambiko ya ukumbusho ya unga safi. Umiminie tambiko zako mafuta, kadiri unavyoweza kupata.
12 Kisha mengine mwachie daktari; maana Bwana ndiye aliyemuumba; usikubali akuache maana unamhitaji.
13 Kuna wakati ambapo kupona kwawategemea madaktari.
14 Maana nao pia wanamwomba Bwana ili awape mafanikio katika uchunguzi wao, na katika kuponya ili kuokoa maisha.
15 Mtu anayetenda dhambi dhidi ya Muumba wake, mwache aanguke mikononi mwa daktari.

Matanga
16 Mwanangu, mlilie mtu aliyekufa; lia kwa uchungu, kuonesha huzuni yako. Uuzike mwili wake kwa heshima ipasavyo, wala usipuuze mazishi yake.
17 Lia kwa uchungu na kwa moyo, hudhuria matanga kama anavyostahili marehemu, omboleza siku mbili tatu usije ukasemwa; kisha ufarijike kutokana na huzuni yako.
18 Maana huzuni huweza kusababisha kifo, na huzuni ya moyo hunyonya nguvu za mtu.
19 Mtu akiondolewa duniani huzuni imekwisha, lakini maisha ya maskini, huulemesha moyo.
20 Usiruhusu moyo wako kutawaliwa na huzuni; ifukuze huzuni, ukifikiria mwisho wako.
21 Usisahau kwamba hakuna kurudi nyuma, humsaidii marehemu chochote na unajidhuru mwenyewe.
22 Kumbuka, utakufa kama alivyokufa, jana yeye, kesho wewe.
23 Marehemu anapowekwa kupumzika kaburini, nako kumkumbuka kuachwe; nawe usiendelee kumlilia roho yake ikisha ondoka.

Shughuli
24 Nafasi humwezesha msomi kujifunza hekima, aliye na shughuli chache aweza kupata hekima.
25 Atakuwaje na hekima mtu anayeshughulika tu na jembe? Fahari yake ni kuongoza ng'ombe, kuwafanya wakokote plau, na mazungumzo yake yote ni juu ya mifugo!
26 Mawazo yake ni kupiga mifuo shambani, na kuwalisha ndama wake.
27 Kadhalika na kila mfanyakazi na fundi, ambaye hufanya kazi usiku na mchana; na wanaonakshi mihuri wakibuni daima mbinu mpya; hufanya bidii kunakshi mifano mizuri, na kukesha wakiikamilisha kazi yao.
28 Kadhalika na mfuachuma kwenye fuawe yake; hufikiria cha kufanya na chuma chake, miali ya moto hudhoofisha mwili wake, akilivumilia joto la tanuri; sauti ya nyundo yake huziba masikio yake, macho yake hukodolea chombo afuacho. Moyo wake umepania kuikamilisha kazi yake na huwa mwangalifu kukamilisha nakshi yake.
29 Kadhalika na mfinyanzi kazini mwake, hulizungusha gurudumu kwa mguu wake, kila siku yu macho juu ya kazi yake na hukesha kutimiza idadi itakiwayo.
30 Huupondaponda udongo kwa mkono wake huufinyanga kwa miguu yake, hutia maanani sana kumaliza kazi yake, na huwa mwangalifu kusafisha kinu chake.
31 Wote hao huitegemea mikono yao, na kila mmoja ana ujuzi wa kazi yake.
32 Bila wao mji haujengeki; na watu hawawezi kuutembelea wala kuishi huko.
33 Hata hivyo, hawafikii hali ya kuwa halmashauri ya watu, wala hawapewi hadhi katika kikao cha hadhara. Hawawi mahakimu wala kuelewa hukumu zinazotolewa.
34 Hawawezi kueleza mafunzo au maamuzi ya sheria, wala hawajaonekana wakitumia methali.
35 Lakini huufanya ulimwengu ulioumbwa utengemae, na dua lao lahusu mambo ya shughuli zao!

Generic placeholder image