49

Yosia
1 Kumkumbuka Yosia ni kama mchanganyiko wa ubani, ambao umechanganywa na fundi stadi, ni mtamu kama asali kwa kila mtu, ni kama muziki kwenye karamu ya pombe.
2 Aliongozwa sawa kuwaongoa watu, akayangolea mbali machukizo yao ya uovu.
3 Alikuwa mwaminifu kabisa kwa Bwana! Wakati watu walipokuwa waovu, yeye aliimarisha utendaji wa mema.

Yeremia
4 Isipokuwa Daudi, Hezekia na Yosia, wafalme wengine walitenda dhambi sana, maana waliiacha sheria ya Mungu Mkuu, wafalme wa Yuda, mpaka wa mwisho.
5 Uwezo wao waliwaachia watu wengine, na heshima yao wakawapa taifa la kigeni
6 ambalo liliuteketeza kwa moto mji mteule wa hekalu, likaiacha mitaa yake kuwa mitupu, kulingana na neno la Yeremia.
7 Maana walimtesa Yeremia, ingawa alikuwa amewekwa wakfu kuwa nabii kabla ya kuzaliwa, angoe, aharibu na kuangamiza, na pia ajenge tena na kupanda.

Ezekieli
8 Ezekieli ndiye aliyeona maono ya utukufu, ambayo Mungu alimwonesha juu ya gari la viumbe wenye mabawa.
9 Maana Mungu aliwakumbuka maadui zake kwa tufani, lakini akawatendea mema wale walioishi maisha yao vizuri.

Manabii kumi na wawili
10 Mifupa ya manabii kumi na wawili na iimarike huko kaburini; maana waliwatia moyo watu wa Yakobo, na kuwakomboa kwa kuwapa tumaini thabiti.

Zerubabeli na Yoshua
11 Tutamsifu Zerubabeli namna gani? Yeye alikuwa pete ya mhuri katika mkono wa kulia!
12 Kadhalika na Yoshua mwana wa Yozadaki. Wakati wao, walijenga madhabahu, na kusimika hekalu takatifu ambalo utukufu wake wadumu milele.

Nehemia
13 Ukumbusho wa Nehemia ni wa kudumu. Yeye alitujengea tena kuta zilizoanguka, akasimika tena malango na mifumo, na kujenga upya nyumba zilizoharibiwa.

Wazee wa kale
14 Duniani hakuna aliyeumbwa kama Henoki alivyokuwa, maana yeye alichukuliwa kutoka duniani.
15 Na pia hakuna mtu aliyezaliwa duniani kama Yosefu alivyokuwa; na mifupa yake inatunzwa.
16 Shemu na Sethi waliheshimiwa na watu wao, naye Adamu anaheshimika kuliko viumbe vyote hai duniani.

Generic placeholder image