22

1 Mtu fidhuli aweza kulinganishwa na jiwe chafu; kila mtu akimwona hufyonya kwa sababu ya aibu yake.
2 Mtu fidhuli aweza kulinganishwa na marundo ya mavi; kila mtu anayeyagusa huyakungutia mbali.
3 Ni balaa kuwa baba wa mtoto asiye na nidhamu; na kuzaliwa kwa binti asiye na nidhamu ni hasara.
4 Msichana mwenye busara hupata mume, lakini atendaye kwa aibu humhuzunisha baba yake.
5 Msichana asiye na adabu atamwaibisha baba yake na mumewe, naye atadharauliwa na wote wawili.
6 Kama vile muziki katika matanga ndivyo hadithi isiyo ya wakati wake. Kuadhibu na kupa nidhamu ni jambo la hekima daima. [ 7Watoto waliolelewa vizuri hawaonyeshi hali nyonge ya kuzaliwa kwa wazazi wao. 8Watoto ambao hawalelewi vema, watovu wa adabu na wenye kiburi ni doa kwa jamaa yao.]
9 Amfundishaye mpumbavu ni kama anayeunga vigae, au anayemwamsha mtu kutoka usingizi mzito.
10 Amwambiaye mpumbavu hadithi anamwambia mtu anayepepesuka; na mwishowe huyo atasema: “Ni nini?”
11 Mwombolezee aliyekufa maana hana mwanga; na mwombolezee mpumbavu maana hana akili. Usimwombolezee mno aliyekufa maana amepumzika; lakini mpumbavu, maisha yake ni mabaya kuliko kifo.
12 Matanga hufanywa kwa muda wa siku saba; lakini matanga ya mpumbavu na asiyemcha Mungu hudumu maisha yake yote.
13 Usiongee mno na mtu mpumbavu; na usimtembelee mtu asiye na akili. Mwepe ili aweze kuepa taabu; naye atakapojikunguta wewe hutachafuka. Mwepe nawe utapata amani, wala hutachoshwa na kichaa chake.
14 Ni kitu gani kizito kuliko risasi? Kitu hicho jina lake ni “Pumbavu!”
15 Kubeba mchanga, chumvi na chuma ni rahisi kuliko kumvumilia mpumbavu.
16 Boriti lililofungwa imara kwenye nyumba halitangolewa kwa mtetemeko wa nchi. Kadhalika na moyo ulioimarika katika mashauri ya busara hautakuwa na woga wakati wa hatari.
17 Moyo ulioimarishwa na mawazo ya busara ni kama mnara imara uliotiwa nakshi.
18 Mawe madogo juu ya ukuta hayatabaki hapo upepo ukivuma. Kadhalika na moyo wa fikira za kipumbavu; hautaweza kustahimili matukio ya kutisha.
19 Ukilijeruhi jicho machozi yatatoka; ukiujeruhi moyo utaondoa urafiki.
20 Ukiwatupia ndege jiwe utawafukuza; na ukimkaripia rafiki utavunja urafiki.
21 Hata kama umekwisha mnyoshea rafiki yako upanga usife moyo maana inawezekana kurudisha urafiki.
22 Kama umetamka kitu dhidi ya rafiki yako usiogope maana upatanisho unawezekana. Lakini kutukana na kuwa na kiburi, kusema siri na kushambulia wengine ghafla, ni vitu ambavyo hufukuza marafiki wa mtu.
23 Mfanye jirani yako akuamini wakati wa umaskini wake, ili ufurahi pamoja naye wakati atakapopata fanaka. Msaidie wakati anapopata mateso, ili upate sehemu yako katika mali atakayopewa.
24 Moshi ni dalili ya moto, mvuke na moshi wa tanuri hutangulia moto; kadhalika nayo matusi ni dalili ya mauaji.
25 Sitaona aibu kumlinda rafiki wala sitajificha mbali naye.
26 Lakini ikiwa nitaumia kwa sababu yake yeyote atakayesikia habari hiyo atamwepa.

Sala ya kuomba ulinzi dhidi ya maovu
27 Nani ataniwekea mlinzi mdomoni mwangu, na kuupiga mhuri wa busara, ili unizuie nisije nikakosa, ulimi wangu usije ukaniangamiza!

Generic placeholder image