32

Karamu
1 Kama ukifanywa msimamizi wa karamu usivimbe kichwa, ila ujifanye kama wengine karamuni; wahudumie vizuri kwanza kisha ukae.
2 Ukisha timiza wajibu wako, keti mahali pako, ujifurahishe pamoja na wengine na kupewa shada la heshima kwa kazi yako njema.
3 Ikiwa wewe ni mzee kwa umri zungumza; lakini ongea kwa busara, usikatishe muziki.
4 Kama kunatolewa vinywaji usirefushe mazungumzo yako. Usioneshe elimu yako wakati usio wake.
5 Muziki kwenye karamu ya pombe ni kama mhuri wa kito juu ya dhahabu.
6 Muziki mtamu pamoja na pombe ni kama mhuri wa zumaridi juu ya dhahabu.
7 Ikiwa wewe ni kijana, ongea kama ni lazima; lakini si zaidi ya mara mbili na iwe umeombwa.
8 Ongea wazi, useme mengi kwa machache; onesha kuwa wajua mengi ila hupendi kusema.
9 Ukiwa miongoni mwa wakuu usijifanye sawa nao, usiseme maneno ya porojo wakati mwingine anaongea.
10 Kama umeme unavyotangulia ngurumo, ndivyo heshima inavyotangulia mtu anayejiheshimu.
11 Ondoka karamuni wakati unaofaa, usiwe wa mwisho; nenda nyumbani upesi wala usingojengoje.
12 Jifurahishe na kufanya unachotaka, lakini usitende dhambi kwa maneno ya majivuno.
13 Kwa ajili ya mambo haya mtukuze Mungu aliyekuumba na kukuridhisha kwa zawadi zake nzuri.

Uchaji
14 Amchaye Bwana, hukubali kukosolewa naye, na anayemtafuta mapema atapata baraka zake.
15 Anayeitafuta sheria, ataridhika kuipata, lakini mnafiki atapata kikwazo.
16 Wamchao Bwana watajua kutenda sawa, na matendo yao yatangaa kama mwanga.
17 Wenye dhambi hawakubali kukosolewa; hupata kisingizio kufanya watakavyo.
18 Mwenye busara hapuuzi maoni ya mtu, lakini mtu fidhuli na mwenye majivuno haogopi kitu.
19 Usifanye chochote bila kufikiri, nawe hutalazimika kujuta baada ya kufanya kitu.
20 Usifuate njia yenye vikwazo vingi, usije ukajikwaa juu ya mawe.
21 Usiwe na imani mno na njia iliyonyoka,
22 ila uwe mwangalifu sana juu ya njia yako.
23 Uchukue hadhari katika kila kitendo, maana hii ndiyo maana ya kuzishika amri.
24 Anayeiamini sheria atazitii na amri, na anayemtegemea Bwana hatapata madhara.

Generic placeholder image