4

1 Mwanangu, usimpunje maskini mahitaji yake, usimtamanishe bure mtu aliye fukara.
2 Usimhuzunishe mtu mwenye njaa, au kumkasirisha mtu mwenye shida.
3 Usimzidishie matatizo mtu mwenye taabu, wala usicheleweshe sadaka yako kwa maskini mwombaji.
4 Usikatae kumsaidia mwombaji aliye na taabu, wala usimpe kisogo maskini.
5 Usiepe kumwangalia mtu fukara, usimpe nafasi ya kukulaani.
6 Maana akikulaani katika uchungu alio nao, Muumba wake ataisikia sala yake.
7 Ifanye jumuiya ya watu ipendezwe nawe; inama kichwa kwa heshima mbele ya wakuu.
8 Tega sikio, umsikie mtu maskini, na kuitikia salamu yake kwa upole.
9 Mkomboe anayedhulumiwa makuchani mwa mdhalimu, wala usiyumbeyumbe unapotoa hukumu.
10 Uwe baba kwa walio yatima, na kama mume kwa mama zao wajane. Hapo utakuwa mwana wa Mungu Mkuu naye atakupenda kuliko akupendavyo mama yako.

Hekima ni Mwalimu
11 Hekima huwatukuza wanawe, na kuwasaidia wale wanaomtafuta.
12 Ampendaye Hekima, anapenda maisha; wamtafutao Hekima mapema, watajazwa furaha.
13 Anayeambatana naye atapata heshima, na Bwana atapabariki mahali anapokwenda.
14 Wanaomtumikia Hekima, wanamtumikia Mungu Mtakatifu; Bwana huwapenda wale wanaompenda Hekima.
15 Anayemtii Hekima atayahukumu mataifa, anayemsikia Hekima ataishi kwa usalama.
16 Aliye mwaminifu atampata Hekima, na wazawa wake wataendelea kuwa naye.
17 Maana ingawa atampitisha kwanza katika njia za taabu na kumletea hofu na hali ya woga, akimjaribu kwa nidhamu mpaka amwamini, na kumpima kwa kumletea maafa;
18 baadaye humjia moja kwa moja na kumfurahisha na kumjulisha siri zake.
19 Lakini mtu huyo akikosea, ataondoka kwake, na kumwacha kwenye maangamizi yake mwenyewe.
20 Chukua tahadhari wakati ufaao na kuepa uovu, wala usijiletee aibu kwako mwenyewe.
21 Maana kuna aibu inayoongoza katika dhambi, lakini kuna aibu ambayo huleta sifa na heshima.
22 Usioneshe ubaguzi kwa hasara yako au upendeleo na kujiangamiza wewe mwenyewe.
23 Usiache kusema wakati unaofaa, wala usifiche hekima yako.
24 Maana hekima yako yajulishwa kwa yale unayosema, na busara yako kwa maneno unayotamka.
25 Usiupinge ukweli, bali uwe na tahadhari juu ya kutojua kwako.
26 Usione aibu kuungama dhambi zako, usijaribu kupinga mkondo wa mto.
27 Usikubali kutawaliwa na mtu mpumbavu, wala kumpendelea mtawala.
28 Pigania ukweli hata mpaka kifo, naye Bwana Mungu atakupigania.
29 Usiwe ovyo katika usemi wako, wala mzembe katika matendo yako.
30 Usiwe kama simba nyumbani kwako, wala mwenye kuwatuhumu watumishi wako.
31 Usiwe mtu wa kupokea tu, wala kuwa mgumu wa kuwapa wengine.

Generic placeholder image