45

Mose
1 Kutoka wazawa wa Yakobo Bwana akamtokeza mtu mwema aliyepata kibali mbele ya watu wote, akapendwa na Mungu na watu. Huyo alikuwa Mose ambaye ni furaha kumkumbuka.
2 Bwana alimfanya mwenye utukufu sawa na malaika, na mwenye nguvu hata akaogopwa na maadui zake.
3 Kwa neno la Mose, Bwana alikomesha yale maajabu, alimfanya atukuke mbele ya wafalme. Bwana alimpa Mose amri kwa ajili ya watu wake, akamwonesha sehemu ya utukufu wake.
4 Kwa uaminifu na upole wake, Bwana alimweka wakfu, akamteua miongoni mwa binadamu wote.
5 Bwana alimjalia Mose kusikia sauti yake, akamwongoza katika lile giza kubwa. Alimpa amri zake ana kwa ana, sheria ya uzima na maarifa, ili kuwafunza watu wa Yakobo agano lake, kuwafundisha Waisraeli maagizo yake.

Aroni
6 Bwana alimwinua Aroni, ndugu yake Mose, mtu mtakatifu kama Mose, wa kabila la Lawi.
7 Alifanya naye agano la milele akampa ukuhani wa watu wake. Alimpatia mavazi ya fahari, akamvalisha joho la utukufu.
8 Bwana alimvika Aroni ukamilifu mkuu, akamwimarisha kwa ishara za mamlaka: Suruali, joho na vazi la kizibao kitakatifu.
9 Alimzungushia makomamanga, na kengele nyingi za dhahabu, zitoe sauti anapotembea, sauti zake zisikike hekaluni, kama ukumbusho kwa watu wake.
10 Alimvika vazi takatifu la dhahabu, buluu na rangi zambarau lililotariziwa na fundi stadi, akampa vitu vya kuonesha kauli ya kweli.
11 Alimvika sufu nyekundu, iliyotengenezwa na fundi wa nakshi, na vijiwe vya thamani vilivyochongwa kama mhuri na kutiwa dhahabu, vyote vimetengenezwa na mhunzi wa vito; vimeandikwa kwa ukumbusho wa idadi ya makabila ya watu wa Israeli.
12 Kwenye kilemba chake alitia taji ya dhahabu, iliyochongwa kama mhuri wa kuwekwa wakfu. Hiyo ilinakshiwa kwa ufundi mkubwa, kazi nzuri ya msanii, nzuri mno kuitazama na imepambwa sana.
13 Hakukuwa na vitu vizuri kama hivyo kabla yake, wala hakuna mgeni aliyewahi kuvaa vitu kama hivyo. Ni wazawa wake peke yao waliovivaa vitu hivyo milele,
14 tambiko atakazotolea zitateketezwa nzima, nazo zitatolewa daima mara mbili kila siku.
15 Mose alimweka Aroni wakfu, na kumpaka mafuta matakatifu. Agano la milele lilifanywa naye na wazawa wake, kwamba watamtumikia Bwana kama makuhani na kuwabariki watu kwa jina lake.
16 Bwana alimteua Aroni kati ya watu wote, amtolee Bwana tambiko, afukize ubani wa ukumbusho wenye harufu nzuri, na kuwafanyia watu upatanisho.
17 Alimkabidhi Aroni amri zake, akampa mamlaka ya kuweka sheria na kuamua, kuwafundisha watu wa Yakobo maamuzi yake na kuwaangazia kuhusu sheria yake.
18 Watu wa nje waliafikiana kumpinga Mose, wakamwonea wivu kule jangwani. Hao walikuwa Dathani, Abiramu na wenzao, na Kora pamoja na kundi lao wakiwaka hasira.
19 Bwana alipoyaona hayo hakupendezwa, na kwa ghadhabu yake kali akawaangamiza. Alitenda maajabu dhidi yao akawateketeza kwa ndimi za moto.
20 Kisha akamwongezea Aroni fahari yake, na kumpa urithi wake mwenyewe: Haki juu ya matoleo ya malimbuko.
21 Chakula chao kinatokana na tambiko za Bwana; Bwana alimpatia vitu hivyo Aroni na wazawa wake.
22 Lakini Aroni hakuwa na sehemu yake ya urithi nchini, hakuwa na fungu lake miongoni mwa watu; maana tambiko zake Bwana ndio urithi wake.

Finehasi
23 Finehasi, mwanawe Eleazari, ni wa tatu kwa fahari, maana alikuwa na hamu kubwa ya kumcha Bwana, akasimama imara wakati watu walipoasi, akawa tayari kwa wema wake moyoni, na kuwaombea Waisraeli msamaha wa dhambi.
24 Kwa hiyo Bwana akafanya naye agano la amani, kwamba atakuwa kiongozi wa mahali pa ibada na watu wake, yeye na wazawa wawe na heshima ya ukuhani milele.
25 Kulikuwa pia na agano lingine na Daudi, mwana wa Yese, wa kabila la Yuda, urithi wa ufalme wake ulikuwa kwa mtoto hata mtoto, hali ukuhani wa Aroni ulirithiwa na wazawa wake wote.
26 Bwana akujalie hekima moyoni mwako, uwaamue watu wake kwa haki, ili ustawi wao usiangamie na fahari yao idumu vizazi vyao vyote.

Generic placeholder image