29

Kukopa na kulipa
1 Mwenye huruma humkopesha jirani yake; kumsaidia jirani ni kutimiza amri.
2 Mkopeshe jirani yako anapohitaji msaada, na ukimkopa jirani yako, mlipe mara.
3 Tekeleza neno lako na kuwa na imani naye, nawe utapata mahitaji yako kila wakati.
4 Wengi hudhani mikopo ni zawadi, na kuwaaibisha hao waliowasaidia.
5 Mtu atabusu mkono wa mtu mwingine mpaka amkopeshe, na kunongoneza juu ya mali ya jirani yake. Lakini wakati wa kulipa mkopo atachelewa, atalipa kwa maneno mengi matupu na kudai kukosekana kwa wakati.
6 Kama anaweza kulipa, atamlipa labda nusu, kwani mkopaji anadhani mkopo si wa kulipa. Kama hawezi kulipa, mkopaji amemwibia, na hivyo amemfanya kuwa adui yake bure. Atamlipa laana na matukano; badala ya kumheshimu atamlipa madharau.
7 Kwa sababu hiyo, wengi hukataa kukopesha, wanaogopa kudhulumiwa bure.

Ukarimu
8 Hata hivyo, uwe na uvumilivu kwa mtu aliye maskini, wala usimfanye angoje mno kupata msaada wako.
9 Msaidie maskini kwani hiyo ni amri, kama anahitaji, usimwache aende mikono mitupu.
10 Tumia fedha yako kumsaidia ndugu au rafiki, wala usiiache ipate kutu mafichoni na kupotea.
11 Tumia utajiri wako kama alivyoamuru Mungu Mkuu nawe utapata faida kubwa kuliko dhahabu.
12 Jaza hazina yako misaada kwa maskini, hiyo itakuokoa wakati wa maafa.
13 Hiyo itakupigania dhidi ya adui yako, vizuri kuliko kwa ngao kubwa na mkuki mzito.

Dhamana
14 Mtu mwema atamwekea jirani yake dhamana, lakini mtu asiye na aibu atamwacha.
15 Usisahau wema wa mdhamini wako, maana ameyahatarisha maisha yake kwa ajili yako.
16 Lakini mtu mwenye dhambi ataharibu mali ya mdhamini wake, mtu asiye na shukrani atamwacha yule aliyemwokoa.
17 Kutoa dhamana kumewaangamiza matajiri wengi, na kuwatikisa kama kwa mawimbi makubwa.
18 Kutoa dhamana kumewafanya watu wengi maarufu kuwa wakimbizi, wakatangatanga miongoni mwa mataifa mengine.
19 Mwenye dhambi anayekubali kuwa mdhamini atajuta, atatafuta faida na kujikuta amekabiliwa na sheria.
20 Msaidie jirani yako kadiri unavyoweza, lakini uchukue hadhari usije ukaanguka katika maafa.

Nyumba na ukarimu
21 Mahitaji ya maisha ni maji, chakula na mavazi, na nyumba unakoweza kujificha.
22 Afadhali maisha ya maskini mwenye nyumba yake mwenyewe, kuliko chakula cha fahari nyumbani kwa wengine.
23 Ridhika na kidogo ulicho nacho, nawe hutakemewa kuwa unaishi kwa jasho la wengine.
24 Ni fedheha kutangatanga nyumba moja hata nyingine, popote ulipo mgeni huwezi kufungua kinywa chako;
25 wewe utakuwa mgeni na kuonja kunyenyekeshwa, tena utasikia maneno yatakayokuumiza:
26 “Mgeni, njoo hapa na kuandaa meza! Na kama una chochote, nipe nile.
27 Mgeni, nenda zako umwachie nafasi mtu maarufu. Ndugu yangu anakuja kwangu, nahitaji nyumba yangu.”
28 Mambo ya kutukanwa kuhusu malazi na mkopo, hayavumiliki kwa mtu mwenye akili zake.

Generic placeholder image