28

1 Anayelipiza kisasi naye atalipizwa na Bwana, na Bwana atathibitisha kuwa mtu huyo ana dhambi.
2 Msamehe jirani yako maovu aliyokutendea, nawe unapoomba, utasamehewa dhambi zako.
3 Kama mtu akidumisha hasira dhidi ya mtu mwingine, atawezaje kumtaka Bwana amwonee huruma?
4 Kama hamwonei huruma binadamu mwenzake, je, ni sawa kumwomba Bwana amsamehe dhambi zake?
5 Kama yeye ambaye ni kiumbe tu anashikilia hasira, nani atamsamehe yeye dhambi zake?
6 Kumbuka mwisho wa maisha yako uache uadui; kumbuka maangamizi na kifo, uzingatie amri.
7 Kumbuka amri, na usimkasirishe jirani yako. Likumbuke agano la Mungu Mkuu, uache ujinga.

Mabishano
8 Epa ugomvi, nawe utapunguza kutenda dhambi. Maana mtu mwenye hasira huchochea ugomvi.
9 Mwenye dhambi huwasumbua marafiki na kuweka uadui kati ya watu waishio kwa amani.
10 Kadiri ulivyo na kiasi cha kuni, ndivyo na moto utakavyowaka. Kadiri ubishi unavyozidi, ndivyo na ugomvi utakavyowaka. Kadiri mtu alivyo na nguvu ndivyo atakavyozidi kuwaka hasira. Kadiri mtu anavyozidi kuwa tajiri, ndivyo anavyozidi kuwa na ghadhabu.
11 Kugombana kwa ghafla huwasha moto, na ugomvi wa ghafla humwaga damu.
12 Ukipuliza kaa la moto litawaka zaidi, ukilitemea mate litazimika; hayo yote mawili ni matokeo ya kinywa chako.

Mazungumzo machafu
13 Alaaniwe mtu mchongezi na mdanganyifu, maana amewaangamiza wengi wanaoishi kwa amani.
14 Uchongezi umevunja amani ya wengi, na kuwatawanya kutoka taifa hata taifa lingine; uchongezi umeangamiza miji yenye nguvu, na kuangusha nyumba za wakuu.
15 Uchongezi umewafanya wake waaminifu wawakimbie waume zao, na kuwanyanganya matunda ya jasho lao.
16 Yeyote anayemsikiliza mchongezi hatatulia moyoni, wala hataishi kwa amani.
17 Pigo la mjeledi hubakiza kovu, lakini pigo la ulimi huvunjavunja mifupa.
18 Watu wengi wameuawa kwa upanga, lakini ni wengi zaidi waliouawa kwa ulimi.
19 Heri mtu ambaye amekingwa mbali na ulimi, mtu ambaye hajakabiliwa na hasira yake. Mtu ambaye hajabeba nira yake, na kufungwa kwa pingu zake.
20 Maana nira yake ni nira ya chuma, na pingu zake ni pingu za shaba.
21 Kifo kiletwacho na uchongezi ni kifo kibaya, kuzimu ni afadhali kuliko uchongezi.
22 Lakini uchongezi hauwezi kuwatawala wamchao Mungu, hao hawatachomwa na miali yake.
23 Makuchani mwake wataanguka wale wanaomwacha Bwana; watakuwa chini ya mamlaka yake. Uchongezi utawaka ndani yao, wala hautazimishwa. Utawavamia hao kama simba, utawararuararua kama chui.
24 Hakikisha umeweka ua wa miiba kuzunguka mali zako, umefungia ndani fedha na dhahabu yako.
25 Hakikisha umeizungushia mali yako ua wa miiba, pima maneno yako kama vile kwa mizani, na kinywa chako ukiwekee mlango na kufuli.
26 Jihadhari usije ukakosa kwa kinywa chako, la sivyo utaanguka mbele ya huyo anayekuotea.

Generic placeholder image