25

Watu wanaostahili kusifiwa
1 Moyo wangu wafurahia mambo matatu; mambo yaliyo mazuri mbele ya Bwana na wanaadamu: Ndugu wanaopatana vizuri, jirani wenye uhusiano mwema, na mke na mume wanaoishi kwa furaha.
2 Moyo wangu wawachukia watu wa aina tatu, watu ambao nachukizwa sana na maisha yao: Maskini mwombaji mwenye kiburi, tajiri ambaye ni mwongo, na mzee mzinzi asiye na akili.
3 Kama hukuokota chochote cha funzo ulipokuwa kijana, utawezaje, basi, kupata chochote katika uzee wako?
4 Ni jambo zuri mno kwa mzee mwenye mvi kuamua vema, na mwenye umri mkubwa kujua namna ya kushauri!
5 Ni jambo la kupendeza mno hekima katika wazee, na mawaidha yafaayo na mashauri kutoka kwa watu mashuhuri!
6 Uzoefu mwingi wa maisha ni taji ya wazee, kumcha Bwana ndiyo fahari yao.
7 Najua mambo tisa ambayo nayathamini sana moyoni; naam, na jambo la kumi nitawaambieni pia: Mtu anayefurahi kwa sababu ya watoto wake, mtu aishiye hata akawaona maadui zake wanaangamia;
8 mwanamume aliye na bahati ya kuishi na mke mwenye akili, ambaye halimi shambani kwa ng'ombe pamoja na punda, mtu ambaye hajakoseshwa na ulimi wake, mtu asiyemtumikia mtu ambaye hastahili,
9 mtu aliye na bahati ya kupata rafiki amini, na mtu ambaye watu hufurahia kumsikiliza.
10 Jinsi gani alivyo mkuu mtu aliyepata hekima! Lakini hakuna aliye mkuu kuliko yule amchaye Bwana!
11 Kumcha Bwana ni muhimu kuliko mambo yote. Mtu amchaye Bwana hana kifani!
[12 Kumcha Bwana ni mwanzo wa kuandamana naye.]

Mke mwema na mke mbaya
13 Hakuna jeraha baya kama jeraha la moyoni! Hakuna ubaya mbaya kuliko ubaya wa mwanamke!
14 Hakuna pigo baya kama la mtu mwenye chuki. Hakuna kisasi kibaya kama kisasi cha adui.
15 Hakuna sumu mbaya kama sumu ya nyoka, na hakuna hasira mbaya kama hasira ya adui.
16 Afadhali kuishi na simba na nyoka kuliko kuishi na mwanamke mwovu.
17 Uovu wa mwanamke humbadilisha sura, uso wake ukawa kama uso wa dubu.
18 Mumewe akila chakula kwa jirani hawezi kujizuia kupiga kite kwa uchungu.
19 Hakuna uovu mbaya kuliko uovu wa mke wa mtu; huyo atapatwa na balaa la wenye dhambi.
20 Kama vile ilivyo shida kwa miguu ya mzee kupanda mlima uliojaa mchanga, ndivyo ilivyo kwa mume mpole kuishi na mke mwenye makelele.
21 Usinaswe na uzuri wa mwanamke, wala usimtamani mwanamke kwa mali yake.
22 Ni ghadhabu, aibu na fedheha mume kulishwa na mkewe.
23 Moyo wa huzuni, kukosa raha na kuvunjika moyo, husababishwa na mke mwovu. Mikono na magoti hafifu ya mumewe husababishwa na mke asiyemfurahisha mumewe.
24 Dhambi ilianza kwa mwanamke, na kwa sababu yake sote lazima tufe.
25 Kama vile huachi maji yavuje, vivyo hivyo usikubali mke mwovu aseme apendavyo.
26 Kama hapendi kufuata kama unavyomwagiza, basi mtenganishe nawe.

Generic placeholder image