41

Kifo
1 Ewe kifo! Kukukumbuka ni uchungu mkubwa, kwa mtu anayeishi kwa amani na mali zake; kwa mtu asiye na wasiwasi, anayefanikiwa kila kitu, na aliye bado na nguvu za kufurahia chakula chake.
2 Ewe kifo! Hukumu yako ni jambo jema sana kwa fukara na ambaye nguvu zake zinamwishia, kwa mtu mzee sana mwenye wasiwasi juu ya kila kitu, mtu mwenye uchungu na ambaye ameishiwa na uvumilivu.
3 Usiogope maamuzi ya kifo; kumbuka waliokutangulia na watakaokufuata.
4 Hiyo ni kauli ya Bwana kwa viumbe vyote. Kwa nini basi kupinga alichopenda kuamua Mungu Mkuu? Kuishi miaka kumi au mia au elfu, hiyo si hoja huko ahera.
5 Watoto wa wenye dhambi ni chukizo; hurandaranda katika makao ya wasiomcha Mungu.
6 Urithi wa watoto wa wenye dhambi utapotea, na wazawa wao wataishi katika aibu daima.
7 Watoto watamlaani baba asiyemcha Mungu, kwa sababu ya aibu aliyowaletea wanawe.
8 Ole wenu, nyinyi msiomcha Mungu, nyinyi ambao mmeiacha sheria ya Mungu Mkuu!
9 Mkifanikiwa, mapato yenu yatatoweka; mkijikwaa, hamtaweza kuinuka tena; na mtakapokufa, laana ndiyo mtakayopata.
10 Chochote kilichotoka mavumbini hurudi mavumbini, wabaya huanza na laana na kuishia maangamizini.
11 Watu huomboleza juu ya miili ya marehemu, lakini jina baya la wenye dhambi litafutiliwa mbali.
12 Ulipe hadhi jina lako kwani litakubakia, litadumu kuliko hazina elfu moja za dhahabu.
13 Wakati wa furaha ni wa muda tu, lakini jina zuri hudumu milele.

Kuwa na haya
14 Wanangu, zingatieni mafundisho yangu mkae na amani. Hekima iliyofichika na hazina isiyoonekana, je hivyo vina faida gani?
15 Afadhali mtu anayeficha ujinga wake, kuliko yule anayeficha hekima yake.
16 Kwa hiyo uyaheshimu maneno yangu; maana si vizuri kuona haya juu ya kila kitu na si kila hali inakubaliwa kuwa sawa na wote.
17 Uone haya juu ya kufanya machafu mbele ya wazazi, juu ya kusema uongo mbele ya mkuu au mtawala,
18 juu ya kukosa mbele ya hakimu au mwamuzi, juu ya kufanya uovu mbele ya jumuiya,
19 juu ya kumdanganya mwenzako wa kazi au rafiki, juu ya wizi mahali unapoishi.
20 Uone haya juu ya kukosa uaminifu mbele ya Mungu na agano lake, juu ya utovu wa adabu wakati wa kula,
21 juu ya kuwa mchoyo unapoombwa kitu, juu ya kukaa kimya unaposalimiwa,
22 juu ya kumwangalia mwanamke malaya, juu ya kukataa kumsaidia mtu wa jamaa,
23 juu ya kumnyanganya mtu mali yake, juu ya kumkodolea macho mke wa mwenzako,
24 na juu ya kumshawishi mtumishi wake wa kike; tena usiende karibu na kitanda chake.
25 Uone haya kutumia lugha chafu mbele ya rafiki, na wala usimkaripie mtu unayempa zawadi.
26 Uone haya juu ya kurudia na kusema fununu, na kutoa siri za watu.
27 Hiyo ndiyo kuwa na haya halali, ambayo kila mtu anapenda.

Generic placeholder image